Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Fedha kuhusu Mpango wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na suala zima la kilimo na ningegusia moja kwa moja mlinganisho uliopo kwenye kilimo na uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na uchumi wa kati, hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda kama hatutawekeza ipasavyo kwenye kilimo. Viwanda vyote ambavyo tunavikusudia vinahitaji malighafi kutoka kwa wakulima, wakulima hawa lazima tuwawezeshe ili waweze kuzalisha kisasa na waweze kuzalisha kwa tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozalisha ili uchumi uweze kukua hautakua kwa maneno mazuri tutakayokuwa tunayazungumza, wala hautakua kwa kauli mbiu nzuri, kama hivi sasa tunasema uchumi wa viwanda. Tuzungumze Watanzania wote uchumi wa viwanda, havitapatikana viwanda kama hakuna mikakati kwa sababu kauli mbiu nzuri za namna hii zilishawahi kupatikana huko nyuma kwamba kilimo uti wa mgongo na kauli mbiu nyingine, kulikuwa na kauli mbiu nyingi sana katika kilimo, lakini mwisho wa siku bado kilimo chetu kimeendelea kubaki kuwa kilimo cha kutumia jembe la mkono na kilimo kile cha kizamani primitive way. Kwa hiyo, hatuwezi kuendelea kwa kutumia kaulimbiu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri nakushukuru unanisikiliza kwa makini nataka niseme jambo moja, katika suala la korosho ambalo ni zao ambalo kwa sasa linatuingizia kama Taifa kipato kizuri, tunahitaji tuwekeze kwenye viwanda ili korosho zetu tuweze kuzibangua hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia takwimu ambazo yuko mzungumzaji alikuwa anasema hapa na nilijaribu kum-crush kwamba siyo takwimu sahihi. Tanzania kwa kusaidia tu na kuweka sawa, Tanzania mwaka jana tulizalisha tani 250,000 za korosho na ni nchi miongoni mwa wazalishaji wakubwa tu wa korosho na kwa bahati nzuri korosho ya Tanzania ni moja ya korosho bora duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye mitandao wameandika kabisa best cashewnuts producers ni Tanzania na Mozambique. Ni korosho tamu, zenye mafuta na ni korosho ambazo zinapendwa sana. Kwenye soko la dunia zikifika korosho za Tanzania na Msumbiji zingine zinasubiri ili ziweze kuuzwa. Sasa nini ninachokusudia kusema? Ninachokusudia kusema ni kwamba, hii thamani ya korosho ya sasa shilingi 3,900 mpaka shilingi 4,000 bado haikidhi haja wala haifikii kiwango ambacho wakulima wanapaswa kukipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nimejaribu kuangalia leo soko la dunia bei ya korosho ghafi ni shilingi ngapi, ni kuanzia dola tano mpaka dola 13 lakini korosho iliyobanguliwa yaani zile cashewnuts canals nilizokuwa nazisema mara ya kwanza, leo zinacheza kwenye dola 25 mpaka dola 29. Ni korosho ambazo tayari zimeshakuwa processed, maana yake ni zaidi ya shilingi milioni 50 lakini huko mbali. Katika soko la ndani pekee hivi sasa korosho iliyobanguliwa ukifika pale Mtwara inauzwa kati ya shilingi 25,000 na shilingi 30,000 maana yake ni zaidi ya dola 12 mpaka dola 15. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokusudia kusema ni kwamba kama tuna mipango iliyokuwa madhubuti, tunaweza tukabangua korosho zetu, tukategemea soko la ndani na soko la nje, tukapata kipato kikubwa zaidi. Ndiyo maana wasioelewa ukiingia leo kwenye mtandao ukatafuta kujua wauzaji wa korosho kwenye soko la dunia hautaiona Tanzania, you will never see it! Utaona tu pale Brazil, utaiona India, utaiona Vietnam, utaiona Ivory Coast, utaiona Canada, kwa sababu wao siyo kwamba wana mikorosho mingi bali wao wana viwanda ambavyo wana-process korosho zao na wanaweza kuzipeleka kwenye soko la dunia, bali Tanzania ni wazalishaji lakini hatupeleki korosho zetu kwenye soko la dunia, we are not recorded anywhere kwamba tunauza korosho kwenye soko la dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninaomba sana hivi ni viwanda ambavyo tunavipoteza, tungeweza kuwekeza kwenye korosho kwa kuweka vile viwanda, kuvifufua vilivyopo, tungeweza kupata kipato kikubwa. Wanatushinda Msumbiji ambao wamepigana vita miaka mingi, leo Msumbiji wanabangua more than 80 percent ya korosho zao, sisi hatujafikia hata asilimia 20, maana yake bado tuko chini kwenye suala la ubanguaji wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo Mheshimiwa Waziri naomba sana mpango tunapopanga kwamba tunataka kwenda kwenye uchumi wa kati na uchumi wa viwanda basi tuhakikishe kwamba tunakuwa na mipango madhubuti lakini siyo maneno matamu yanayoweza kusikika na kufurahisha wasikilizaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ninataka nilichangie ni suala la miradi mikubwa ambayo ilizungumzwa kwenye mpango wa mwaka jana. Mheshimiwa Waziri tunakumbuka kwamba mwaka jana kwenye hotuba yako ya mpango ulizungumzia suala la mradi wa gesi wa Lindi (Liquidfied Natural Gas) nataka kujua umefikia wapi? Taarifa zilizopo mpaka sasa ambazo wananchi wa Lindi, Wabunge na wawakilishi wa wananchi tunajua kwamba ule mradi ndiyo umekufa kifo cha mende, sasa tunataka tujue kwamba mradi ule umekufa au umeendelea na kama unaendelea umefikia wapi, kwa sababu taarifa tulizonazo ambazo inawezekana isiwe rasmi ni kwamba wale jamaa Wentworth Resources na wenzao wameshafunga hata ofisi zao pale London, kwamba shughuli za kuendelea ku-negotiate na ile miradi imeishia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama siyo hiyo njoo ututoe hofu, kwa sababu wale wananchi walifanyiwa tathmini ya kutaka kulipwa fedha zao, watu wameacha kuendeleza mashamba yao, watu wameacha kuendeleza nyumba zao, basi njoo tuambie watalipwa lini na mradi ni lini utaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia kwenye hotuba ya mpango kwa sababu mradi huu ni moja ya miradi mikubwa inawezekana Watanzania hawajui, Mheshimiwa waziri uje utueleze, mradi huu ni mkubwa kama unavyoonekana mradi wa standard gauge, ni mradi mkubwa sana ambao utatumia trillions of shillings, kama tutaupata utatusaidia sana katika kukuza kipato na pato letu la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka niseme ni suala la kuwekeza kwenye uvuvi. Mheshimiwa Waziri katika hotuba hii nimejaribu kuangalia uvuvi namna ulivyouzungumza it is just like a minor issue. Kuna nchi ambazo zinaendesha bajeti zao kwa kutegemea uvuvi tu, na sisi Mwenyezi Mungu ametujalia tuna bahari kuanzia Tanga mpaka unafika Mtwara, bahari ambayo ina samaki wengi na sasa Watanzania wameacha kupiga mabomu, kuua samaki kwa kutumia mabomu na samaki leo wako wengi sana. Mimi miezi miwili hapa niliyokuwa Jimboni pale Mchinga tumekula samaki wengine kama ingekuwa ni binadamu tungeona mpaka mvi, samaki waliozeeka tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni kiashiria kwamba samaki wako wengi lakini uwezo wa wavuvi wetu kwenda kuvua kwenye Bahari Kuu imekuwa ni changamoto. Leo Mheshimiwa Waziri anatambua kwamba mapato pekee tunayoyapata kutoka kwenye uvuvi wa Bahari Kuu ni kutegemea leseni tu, kama tunategemea leseni wakati meli moja ya uvuvi na ninamuona hapa Naibu Waziri wa Uvuvi anajua ni mtaalam, meli moja ya uvuvi ikienda pale Bahari Kuu wana uwezo wa kuvua samaki kwa siku mbili wenye thamani zaidi ya shilingi bilioni moja, bilioni mbili. Lakini sisi tunachukua ushuru wa shilingi milioni 30, milioni 40 na tunafikiria kwamba ndiyo inatosha kabisa!

Mheshimiwa Waziri kama kuna jambo ambalo tunapaswa tuliwekee msingi na msisitizo ni kuwekeza katika bandari ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwekeza katika bandari ya uvuvi tutapata mapato makubwa, kwanza wale wavuaji wataleta samaki wao bandarini tutawa-charge ile kodi, lakini pia kutakuwa na viwanda vya uchakataji ambavyo vitaajiri vijana wengi. Jambo hili liendane sambamba na kuwawezesha wavuvi wetu wa ndani waweze kuwa na capacity ya kwenda kuvua kwenye Bahari Kuu, kwenye kina kirefu cha maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo Mheshimiwa Waziri suala la uvuvi halipaswi kuwa ni suala ambalo linazungumzwa kana kwamba ni suala la utani au kama suala dogo. Uvuvi ni sawa na madini, uvuvi ni sawa na kilimo na uvuvi ni sawa na kitu kingine kama tutawekeza vizuri tunaweza tukapata pesa nzuri na itakayotosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kilimo. Suala la uhakika wa bei ya mazao ya wakulima. Mwaka jana tulisisitiza sana na tuliona Waziri Mkuu wa India alikuja hapa akasaini mkataba na Serikali ya Tanzania juu ya suala la zao la mbaazi, lakini jambo hili linakwenda sambamba na uzalishaji wa zao la ufuta. Nimesikia hapa kwenye taarifa kwamba ufuta sasa umepanda kutoka tani 2,000 na mpaka kufika tani 8,000, lakini wakulima wa ufuta wenyewe hawajui uhakika wa soko la mazao yao. Tunaendelea pale pale kwamba kwenye vichwa vyetu tumejijenga na mentality kwamba mazao ya kuyasafirisha na kupeleka nje ya nchi, kuwatafuta Wahindi wako wapi ili tuwasafirishie, kuwatafuta Wavietnam wako wapi tukawauzie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusiwe na mipango mikakati kwamba huu ufuta uwe processed ndani ya nchi, tukawa tunakula mafuta ya ufuta, na imethibitishwa na madaktari kwamba mafuta ya ufuta ni miongoni mwa mafuta mafuta mazuri ambayo hayana lehemu nyingi.
Tunaweza tukaondoa magonjwa ya pressure at the same time tutakuwa tunaongeza kipato cha wakulima na pato letu la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri ni kuhusu suala la uwekezaji kwenye sekta ya afya. Hatuwezi kuwa na rasilimali watu ambao watakuwa more productive kwenye nchi kama afya zao zitakuwa ni zenye utata. Hivi sasa nilikuwa nasoma hapa ripoti ya ongezeko la ugonjwa wa saratani nchini (cancer), taarifa kutoka Hospitali yetu ya Ocean Road ni kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambayo kiwango kikubwa cha wagonjwa wa kansa wamekuwa wakiongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jirani zetu wa Uganda walikuwa wametuzidi miaka fulani hapa, wameweka mikakati mambo yamekuwa mazuri tumewazidi sisi sasa, Kenya na wenyewe mambo wameweka vizuri kidogo tumewazidi. Katika huu Ukanda wa Afrika Mashariki Tanzania ndiyo tuna orodha kubwa, tuna percentage kubwa ya watu kuugua saratani kuliko nchi yoyote nyingine. Sasa Mheshimiwa Waziri jambo hili ni baya, kwa sababu ugonjwa huu kwanza unatisha jamii lakini pia ni ugonjwa ambao matibabu yake ni very expensive. Kwa hiyo, tunahitaji kuwekeza kama Taifa kuhakikisha kwamba tunatengeneza mechanism nzuri za kufanya prevention ya ugonjwa ama kutoa elimu, ama kuhamasisha jamii kuachana na baadhi ya vyakula au na vitu vingine ili tuwe na jamii ambayo itakuwa na afya njema iweze kuwa productive kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala la afya lisiwe tu suala la kulipigia ngonjera kuja kusema tumewekeza dawa kiasi gani, linahitaji kuwekewa mikakati kuhakikisha kwamba tunapambana madhubuti kabisa na huu ugonjwa wa saratani ambao kwa sasa unatishia kwa kiwango kikubwa sana maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa fursa hii.