Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mambo kama manne hivi, nitazungumzia kwanza suala la road licence na motor vehicle, lakini nitazungumzia pia udhaifu na uchakavu wa fedha zetu, vilevile udhaifu wa EFD receipts na utozwaji kodi mara mbili pale unaposhusha mizigo Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema nikaweza kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Fedha. Vilevile niungane na wenzangu kuwatakia waislamu wenzangu wale ambao tunafunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani na wasiofunga pia Mwenyezi Mungu awafanye wavae vizuri kusudi tuweke swaumu zetu sawa. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Baada ya kusema hayo niseme tu kwamba palikuwa na utaratibu hapo zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa taarifa ya makusanyo ya fedha kila mwezi, lakini mpaka sasa hivi hatujui utaratibu umepotelea wapi. Hili tunaliona ni tatizo, namshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha utaratibu ule uendelee, kila mwezi TRA inapokusanya fedha tupewe taarifa za mapato ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia road licence, hii ni kodi ambayo inalipwa kwa vyombo vinavyotumia barabara. Baada ya wananchi kulalamika tulibadilisha tukaletewa motor vehicle lakini sasa kinachotushanganza motor vehicle inakuwa inalipwa hata kwa vyombo ambavyo vimeshakufa zamani au vimepata ajali na havipo barabarani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali motor vehicle badala ya kushikwa katika vyombo ambavyo hata vimekufa au havipo barabarani basi sasa hivi motor vehicle tuiingize kwenye mafuta ili iwe chombo kinachotumia mafuta moja kwa moja kiwe kinalipa kodi ya Serikali, lakini kulipisha kodi chombo ambacho pengine kama ni gari limeshakufa au lipo garage miaka mingi au limeshatengenezwa majiko ya kupikia huko lakini bado linatozwa kodi, hii ni dhuluma ya mchana kweupe. Kwa hiyo, naishauri Serikali tuingize kodi ya motor vehicle kwenye mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kodi nyingine naishukuru Serikali kwamba imeondoa motor vehicle katika pikipiki, lakini cha kushangaza pikipiki imewekewa kuna kitu kinaitwa fire extinguisher.Ukienda TRA unalipishwa shilingi 10,000 unapotoa shilingi 10,000 kwanza unaelekezwa ukalipie Max Malipo, risiti unapewa Max Malipo lakini hupewi hiyo fire extinguisher yenyewe. Sasa hii nayo ni dhuluma ya Serikali kwa wananchi wa Tanzania. Kwa hiyo, ndugu zangu wa bodaboda na wamiliki wa pikipiki nafikiri mtaona jinsi gani Wabunge tunavyowatetea katika Bunge letu hili. Kwa hiyo, naishauri Serikali fire extinguisher katika pikipiki nayo iondolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia kuzungumzia suala hili la motor vehicle na road licence jirani zetu Kenya hapa hawana. Kenya unalipia insurance ime-contain vitu vyote, lakini Tanzania kuna kodi lukuki mpaka tunawachanganya Watanzania, tunawachanganya wafanyabiashara. Naomba ikibidi hili suala la motor vehicle viondolewe pia. Vilevile pia tuige kwa wenzetu kwa sababu kama ikiwa kumbe unapolipa insurance unaweza ukawa umelipia vitu vyote na sisi tungeiga mfano wa wenzetu Kenya kwa sababu ni jirani zetu na katika baadhi ya mambo ni kama walimu wetu. Kwa hiyo, nafikiri hilo litakuwa limeeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kuzungumzia ni suala la wafanyabiashara kulipishwa kodi kabla hawajafanya biashara, hii nayo mimi naona ni dhuluma ya wazi. Ilikuwa kwanza Watanzania kuna kitu unataka kufanya biashara unaambiwa ufanyiwe assessment, wakati kodi inatakiwa ulipe baada ya kupata faida, Watanzania walipolalamika wakaletewa kitu kinaitwa hiyo assessment lakini unailipa kabla hujafanya biashara. Sasa wenzetu Kenya unapewa tax holiday ya karibu miezi sita, ina maana ufanye biashara, uwe umejiweka vizuri lakini wakati huo huo unapitiwa katika vitabu vyako, na sisi tuombe Tanzania tuwaige wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiingii akilini mtu kabla hajafanya biashara unamlipisha kodi, hii ni dhuluma vilevile kwa wafanyabiashara. Kwa hiyo, naiomba Serikali iwaache wafanyabiashara pale wanapotaka kufanya biashara kwanza wafanye biashara, baadaye Maafisa waTRA wakakague vitabu vyao ndiyo watoze kodi, lakini Tanzania tunakwenda kinyume kabisa, matokeo yake biashara nyingi zinafungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi hapa tulisikia taarifa ya Wizara ya Fedha, kwamba kuna biashara zaidi ya 300 Dar es Salaam zimefungwa, yaani katika mafanikio ya Wizara ya Fedha ni pamoja na kufungia biashara 300 ambazo hazilipi kodi. Mimi nasema haya sio mafanikio, haya ni matatizo. Hizi biashara zinapofungwa zimeondoa Watanzania wangapi katika ajira, zimewafanya watu wangapi maskini? Hata mfanyabiashara mwenyewe anakuwa hana kipato tena, ina maana unahatarisha maisha yake kwa kumkosesha kupata mkate wake wa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya wananchi kulalamika sana, kuna kitu kililetwa kinaitwa presumptive tax. Hii TRA waliiweka kwamba yeyote anayeuza kuanzia shilingi milioni nne mpaka shilingi milioni saba na nusu anatakiwa alipe shilingi 150,000 kwa mwaka, na anayeuza shilingi milioni 16 mpaka shilingi milioni 20 alipe shilingi 862,000. Sasa mtu analipaje fedha zote hizi kabla hajafanya biashara? Naishauri Serikali, kwanza tuwaache wafanyabiashara wafanye biashara halafu ndiyo tushike hizi kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine pia twende mbali zaidi, hizi assessment zinakuwa ni kubwa sana, naishauri Serikali tungetumia ile third law of demand, in the high price low demanded, in the low price high demanded. Sasa sisi hatuendi huko, matokeo yake tunakosa fedha nyingi katika makusanyo ya kodi kwa sababu kodi zetu sio rafiki kwa wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kuzungumzia ni EFD machines. Mashine hizi kwa kweli ni utaratibu mzuri, lakini hapa kwetu Tanzania utaratibu huu tumeukosea. Kwanza, haioneshi kuwa mfanyabiashara aliuza kwa mkopo kwa mteja au anaporudishiwa mali endapo ina dosari risiti ile inamsaidiaje, mwisho wa mwaka anapofanya mahesabu inakuwa ni usumbufu na matatizo makubwa. Vilevile EFD machines zinafutika haraka, sio za madukani tunaponunua bidhaa wala kwenye ATM unapokwenda kutoa fedha benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi ambao tunatunza vitabu vyetu vya mahesabu ikiwa risiti ndani ya siku nne mpaka saba imefutika, mimi nasema huu ni sawasawa na utapeli, kwa sababu kama inavyosemekana kwamba unapokuwa una risiti ndiyo unajua pia takwimu zako za makusanyo zikoje, sasa sisi risiti zetu mbovu. Niliwahi kuwauliza wataalam wa TRA wakasema quality ya zile karatasi za risiti zipo grades tatu, sasa kwa nini tuweke grades tatu kama sio utapeli huu, kwa nini tusiweke grade moja tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, risiti za EFD machines ikibidi zibadilishwe ziwe za plastic material kwa sababu zitakuwa hazifutiki, kama vile ambavyo fedha ya Msumbiji ilivyo, ni ya plastic, hata uichovye kwenye maji haifutiki. Kwa hiyo, nashauri EFD machine receipts ziwe za plastic. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu udhaifu wa fedha zetu, fedha zetu za Tanzania zinatia aibu, nchi kama sisi wenye historia kubwa na pana duniani lakini ukishika shilingi 50, ukishika shilingi 100 ya coin, ukishika shilingi 500 ya noti, ukishika shilingi 1,000, ukishika 2,000 aibu tupu. Pesa ya noti ikipita kwa muuza mkaa, ikaenda kwa muuza samaki, ikiingia kwa muuza juisi hapo ndipo wabillahi taufiq na mchezo umekwisha! pesa imeoza, haifai hata kumzawadia mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, narudi tena, tuitazame dola material yake ilivyo, tuitazame Riyal ya Saudi Arabia jinsi ilivyo, lakini pia tuiangalie pesa ya nchi kama Msumbiji ambayo tumechangia katika kuitetea kupata uhuru, leo wana fedha bora kuliko fedha yetu ya Tanzania, hii ni aibu. Kwa hiyo naishauri Serikali, tuboreshe material ya fedha zetu tunazotumia kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nizungumzie suala la mafao ya wazee wetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki atakapokuja Mheshimiwa Waziri atuambie, deni la wastaafu wa Afrika Mashariki litakwisha lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunisikiliza.