Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ajali Rashid Akibar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai mpaka jioni hii ya leo, ili tuje tushiriki katika mjadala huu wa kuchangia Wizara hii muhimu. Nakushukuru wewe mwenyewe kwa kuweza kutupa nafasi hii na kutoa mchango mdogo kama huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo wamezungumza Wabunge wenzangu, nami nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mpango kwa hii graph ya maendeleo ambayo inaonesha kabisa kwamba asilimia saba kwa kweli kwa uchumi kukua ni asilimia kubwa sana. Kwa kweli kwa hili, Mheshimiwa Mpango amejitahidi sana, namshukuru sana katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni juu ya Kiwanda cha Newala ambacho ameahidi kwamba, anafikiria kukichukua kukirejesha tena Serikalini. Nampongeza sana na achukue kile kiwanda sio asubiri tena aangalie uwezekano akakichukue kesho na aangalie namna gani auaweza akakigawa. Kwa sababu, vile viwanda vilikuwa vingi, Mkoa wa Mtwara na Kusini kote kulikuwa na viwanda zaidi ya 10 ambapo Serikali ilikuwa imekopa fedha nyingi sana na vile viwanda vilivyopo Newala ilikuwa ni Mkopo wa Benki ya Dunia kupitia waliokuwa wajenzi Itaro Fame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mtu yule anapewa kwa bei poa kabisa, Serikali ilikuwa imeingia kwenye deni kubwa ambalo kwa kweli ilikuwa inalilipa, lakini yule mtu mpaka leo hajafanya uzalishaji wowote wa msingi na anachokifanya yeye ni ghala tu. Sasa sio Newala tu, angalia maeneo mengine ambayo kuna viwanda kama vile, wale watu ambao tumewapa vile viwanda hawavitumii kwa yale makusudio ambayo tumewapa na badala yake wanatumia kwa madhumuni mengine. Hivyo viwanda ni vingi sana na ni kweli akichukua hatua Mheshimiwa Waziri tutamwona kwamba, sasa kweli amekuja kivinginevyo, nampongeza katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nishauri, Mheshimiwa Waziri aangalie uwezekano hizi taasisi kutoa fedha, kwa mfano; CAG anampa fedha kidogo sana na zile taasisi ambazo ni muhimu ambazo anadhani kwamba tunawapa mabilioni ya fedha, lakini huyu msimamizi wa fedha anampa fedha kiasi kwamba anashindwa kwenda kufanya ile kazi. Je, haitakuwa kazi ngumu sana kwa sababu, mtu umempa nyama lakini yule Mkaguzi wa kwenda kukagua kile kiwanda hana uwezo wa kwenda kumfikia yule mtu kwenda kukagua? Kwa kweli, Mheshimiwa Waziri naomba afanye jitihada zozote ili hii Ofisi ya CAG aweze kuisaidia iweze kupata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nimepata athari vilevile kutokana na huu ukata. Toka enzi za Waziri Maghembe akiwa Waziri wa Maji, yeye likuja akaahidi pale akasema kwamba, atatupa mradi wa maji kutoka Mitema kwenda kwenye Kijiji cha Chihangu, Chilangala, Miyuyu, Mikumbi na pale maji yatakwenda kwa gravitation force hadi yafike Nnyambe. Kwa hiyo, kile chanzo cha maji kilichopo Mbwinji kikachukuliwa kikapelekwa Masasi hadi Nachingwea. Hatuna tatizo kuhusu maji kwenda Nachingwea, tatizo ni hapa toka akiwa Waziri Maghembe yule Mheshimiwa Maghembe hakuonekana tena mpaka leo kuna Waziri mwingine, kile chanzo wale watu hawajapata maji na yale maji sasa kule eneo lingine yanatoka. Kwa hiyo, wanajiuliza, hawa watu wamekuja kuchukua chanzo hiki cha maji, halafu wao waliahidi kabisa kwamba, wataleta fedha kwa ajili ya kuchukua maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kinachohitajika pale ni fedha tu kwa sababu, yale matenki alishajenga Mwalimu Nyerere yako pale Mikumbi, Miyuyi, kwa hiyo maji kutoka Mitema pale ni mabomba tu, ni kununua tu kwa kutumia fedha hadi kufika Mikumbi kupitia Chihangu. Sasa vinginevyo Mheshimiwa Waziri atakuwa ananigombanisha mimi na wananchi wangu. Sio mimi tu, vilevile wale wananchi watakuwa wanagombana kati ya kijiji na kijiji, wilaya na wilaya na mkoa na mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitaki wananchi wangu waende wakagombane na wananchi wa Masasi, kwa sababu wale wananchi wa Masasi ni ndugu zetu, ila nimwombe Mheshimiwa Waziri, hebu akae na Waziri mwenzake wa Maji, ni namna gani watawapelekea maji wale wananchi wa Newala ili wapate maji, tuangalie uwezekano wa kulitatua tatizo hili, kuliko hii ambayo sasa hivi inakuja kiduchukiduchu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuongea na Waziri wa Maji amesema kwamba tutaangalia uwezekano wa kumpata Mkandarasi, lakini hatutawaleteeni fedha; hatuhitaji fedha sisi tunachohitaji ni huduma. Mheshimiwa Waziri hebu aliangalie hilo kama limekaaje, kama limekaa vibaya, vinginevyo huu ushauri wangu utakwenda at negative attitude.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nimshauri ni kuhusu wafanyabiashara na huu ugawaji wa TIN Number; inawezekana hawa TRA wanamdanganya Mheshimiwa. Mimi mwenyewe haya yamenikuta, nilienda nikasajili kampuni ambayo ilikuwa mimi mwenyewe ni Mkurugenzi pamoja na watoto wangu wanne, jumla tukawa watano, tulivyokwenda kusajili nikategemea kwamba, nitapata TIN Number bure, lakini tulivyokwenda pale tulipewa masharti kwamba, wewe ni lazima uwe na TIN Number ya kampuni, lakini na wewe mwenyewe uwe na TIN Number na Wakurugenzi wawili wawe na TIN Number.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kampuni tukailipia 1,000,000/= na kila mtu ambaye ni Mkurugenzi mle akalipia laki tano na biashara hatujafungua. Mheshiiwa Waziri haoni kama hapo ni double taxation? Hilo nimelifanya Dar-es- Salaam. Double taxation ipo nchi hii, inaonesha si kwamba unapewa tu TIN Number. Unapewa TIN Number ya kampuni ambayo ni Limited Liability Company na Wakurugenzi wote wanalipia laki tano, laki tano kutokana na ile TIN Number na biashara na duka sijafungua mpaka leo. Kwa hiyo, tunakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mheshimiwa Waziri angekuwa na alternative, hawa ni watu wake, hebu awaache wafanye biashara waingie kwenye dema, hana sababu ya kuwatafutia manati hawa watu wake, wanakuwa wengi halafu baadaye anawatoza tozo kidogo kidogo. Hiyo namwambia kabisa kwamba inawezekana ndiyo maana wale wafanyabiashara wa Kariakoo wamekimbia. Mimi ni mfanyabiashara wa Kariakoo, asituone tumekaa hapa, sisi wengine ni Wamachinga. Hicho kitu ninachomwambia na inawezekana ile milango ndiyo maana wale watu wamefunga, wamekimbia wanaogopa double taxation ya TIN Number. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inafika 2,500,000/= mtu hujafungua biashara. Mheshimiwa Waziri asifikirie kwamba, wananchi wake anaowadai kodi wana hela, hawa wananchi wengi milioni mbili ni hela nyingi sana, hebu afikirie, don’t look far, asifikirie mbali sana akadhani kwamba wananchi wake wana hela, hawa watu anaowaongoza ni maskini sana wana mtaji wa Sh.500,000/=, Sh.1,000,000/= na Sh.2,000,000/
=. Huyo mwenye Sh.2,000,000/= ndio ana mtaji mkubwa sana. Kwa hiyo, anapofikiria kumtoza mtu kodi ya Sh.2,000,000/= in advance na hajafungua duka asitarajie yeye akapata kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Mheshimiwa Waziri aache watu wa Kariakoo wafanye biashara kama walivyokuwa wanafanya then anawatoza kodi, tena sio nyingi, hata akiwaambia kwamba, walipe laki tano atapata pesa nyingi tena za kutisha. Hayo mambo yapo, lakini inawezekana watu wanashindwa kumweleza au yeye mwenyewe aende kufanya utafiti pale Kariakoo, hayo mambo atayakuta kule, nadhani atakuja kuniambia ni kweli, sasa hayo mambo ni mazuri, hao watu wanamdanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, hebu kama tunaingia kweli kwenye sekta ya viwanda, tuangalie namna gani wenzetu Wachina wameendelea. Kwa sababu, wale wenzetu walikuwa na mfumo wa Commune, ile Commune mwaka 1967 ilikuwa inakopa duniani, lakini leo ndio shareholder wa Exim Bank ambako leo tunataka kwenda kukopa. Mheshimiwa Waziri aangalie jinsi ya kukaa na Jeshi, kwa maana JKT aangalie pilot areas ambako wanaweza wakapeleka vijana wa JKT wakawa wanalima, lakini wakawa wanazalisha, viwanda vilevile tukawa tumekaa na mtu wa viwanda tunaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tutakuwa tumetengeneza ajira, maana leo ukiwa na pilot area kama 10 na kila pilot area kuna vijana 8,000 utakuwa umeshaajiri vijana 8,000 x 10 utakuwa umeajiri vijana 80,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.