Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ali Salim Khamis

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mwanakwerekwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia na kunipa afya njema na niwatakie Waislam wote duniani Ramadhan Kareem. Pia niwape pole wale wote ambao wamepatwa na maafa, ajali iliyotokea kule Karatu Arusha na wale wote waliopata majanga ya mafuriko hasa Visiwa vya Zanzibar ambapo pia kulitokea upepo mkali ulioezua majumba zaidi ya 70 na mvua ambazo zilisababisha maafa makubwa na majumba mengi kuharibika kutokana na mafuriko hayo ya mvua. Kwa hiyo, nawapa pole wote ambao wamefikwa na maafa haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba utumie busara yako ya kiti kama vile ambavyo tuliwafariji hawa ambao walipatwa na tetemeko kule Bukoba na watoto wetu kule Karatu tukajitolea Wabunge ile posho yetu ya siku moja basi ningeomba busara yako itumike ili siku hii ya leo basi ichangie maafa ambayo yametokea kule Zanzibar, ukilinganisha sasa hivi kuna maradhi ya mlipuko ya kipindupindu, ningeomba busara yako ya Kiti itumike ili kuweza kudumisha muungano wetu Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo, leo nataka nijikite katika jambo moja tu ambalo linahusiana na hii Tume ya Pamoja ya Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kwanza Tume hii ya Pamoja, ipo kikatiba, tokea mwaka 1977 jambo hili liliridhiwa katika Katiba yetu lakini kwa masikitiko makubwa tokea 1977 jambo hili lilipopitishwa katika Katiba yetu limekuja kutungiwa sheria mwaka 1996, miaka 19 baadaye. Kama hiyo haitoshi, jambo hili baada ya kupitishiwa sheria kuundwa kwa Tume yenyewe imekuja kuundwa mwaka 2003 miaka saba baadaye, baada ya kupitishwa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ni jambo la masikitiko na ni jambo la aibu kwamba leo tumeunganisha nchi zetu hizi kwa ajili ya mustakabali wa vizazi vyetu na jamii zetu kutokana na nchi zetu hizi ambazo zimeungana. Ukija katika masuala ya Muungano, yameelezwa katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano na naomba leo niyasome ili kuweka Hansard vizuri, inaonekana pengine baadhi ya watu hatuna uelewa wa haya mambo ya Muungano, lakini ukiisoma Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano mambo haya 22 inaonesha wazi kwamba mambo yote katika nchi hii ni ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo haya ya muungano, ni Katiba ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, pili ni mambo ya nchi za nje, ulinzi na usalama, Polisi, mamlaka ya mambo yanayohusiana na hali ya hatari, uraia, uhamiaji, mikopo na biashara ya nchi za nje, utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na idara ya forodha, bandari, mambo yanayohusiana na usafirishaji wa anga, posta na simu, mambo yote yanayohusiana na sarafu na fedha, leseni ya viwanda na takwimu, elimu ya juu, maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa na motokaa na mafuta ya aina ya petrol, Baraza la Taifa la Mitihani ya Tanzania, usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, utabiri wa hali ya hewa, takwimu, Mahakama ya Rufaa, uandikishaji wa vyama vya siasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiyataja maeneo haya yote ukizungumzia ukusanyaji wa kodi ni jambo la Muungano, kwa hiyo kodi zote zinazokusanywa hapa ndani ya nchi hii ni mambo ya muungano. Leo kuna tozo mbalimbali zinazotozwa ambazo hizi si za kodi zimeainishwa pia katika taasisi mbalimbali. Kwa mfano, Ofisi ya Rais ni ya Muungano lakini yenyewe inakusanya tozo ambazo hizi zinatakiwa zije katika Mfuko wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu hii ni sehemu ya ofisi ya Muungano, lakini Msajili wa Vyama vya Siasa, Mahakama ya Rufaa kama ilivyotajwa huku lakini kuna mashirika mbalimbali, mashirika ya ndege na kadhalika, mpaka leo hii mwongozo umetoka kwamba iwekwe akaunti ya pamoja kati ya nchi hizi mbili ili kutunza haya mapato ya Jamhuri ya Muungano na kuzinufaisha hizi nchi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi leo miaka 40 umri wa mtu mzima, zimeundwa Tume chungu nzima. Ukiangalia utafiti huu ambao umefanywa na Tume ya Katiba kuna tume zimeundwa zaidi ya 11 humu ndani ya book hili ambalo limetolewa kuna Tume ya Mark Bomani, na Tume ya Shellukindo na wengine ambao imeelezea jinsi ya kuifanya Tanzania iondokane na hizi kero za Muungano. Hata hivyo, mpaka leo hii cha ajabu na cha kusikitisha suala hili halijapatiwa ufumbuzi miaka 40, halafu tunaambiwa kwamba Serikali hii ni Serikali sikivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali hii kumbe yale ambayo yametokea kwa nchi hii kwa ajili ya mchanga wa madini kwamba, nchi hii imedhulumiwa na wawekezaji hakuna tofauti na dhuluma ambayo Zanzibar imefanyiwa muda wote huu wa makusanyo ya Muungano hayakuwekwa katika sehemu ya Muungano ili kunufaisha hizi nchi mbili, hakuna tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia kwa ratio ya asilimia 21 katika mgao katika mambo ya muungano, ukiangalia hii trilioni 1.4 ambayo ameitaja Rais, siku ile Tume ilivyowasilisha taarifa yake, Zanzibar tulitakiwa tupate karibu bilioni 66. Sasa ina maana sio ninyi tu mnaoathirika pia Zanzibar nayo inaathirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tulivyokwenda kwenye uchaguzi mwaka 2015 tulisema kwamba, Zanzibar hii itajitegemea kwa uchumi wa huduma na hii Tanganyika ina rasilimali, madini, kilimo na kadhalika. Leo ukiangalia nchi kama Malaysia imestawi katika uchumi kwa sababu ya Singapore. Singapore haina resource ya aina yoyote lakini imewekeza katika huduma, leo Malaysia inanufaika kupitia Singapore. Sasa sisi tunakwenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu liangalieni hili, ikiwa jambo hili halitapatiwa ufumbuzi wa haraka basi inaonesha wazi kwamba wenzetu wa Tanganyika hamko tayari kulipatia ufumbuzi jambo hili na inabidi sasa tukazungumze lugha nyingine kule kwetu kwa ajili ya kuwaambia Wazanzibari Muungano huu imetosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.