Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DANIEL N. NSANZUNGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kwa namna ya pekee nikushukuru wewe mwenyewe binafsi kwa namna ambavyo unatuongoza katika kikao hiki kwamba Wabunge tunahitajiana na Muungano wetu huu ni muungano wa watu wa sehemu zote mbili na lazima wote tuvumiliane, tuheshimiane na tupendane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kusema ninachotaka kusema naomba kwanza nioneshe masikitiko yangu kabisa kwa Wizara hii. Mheshimiwa Waziri nilikuwa nasoma hotuba yako yote, katika maeneo yaliyoathirika na ujio wa Wakimbizi Mkoa wa Kigoma tangu mwaka 1958 tumepokea Wakimbizi, lakini hotuba yote hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais, hakuna hata sentensi moja inazungumzia uharibifu wa mazingira uliosababishwa na ujio wa Wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imenishangaza sana na Mheshimiwa Waziri sijui nina hakika ulisahau maana huwezi kufanya hivyo. Waheshimiwa Wabunge, Mkoa wa Kigoma tuna mazingira ya peke yetu kabisa, hayafanani na mahali pengine. Ujio wa Wakimbizi tumechukua dhima hii kwa niaba ya Taifa letu, lakini naona juhudi zinazofanywa na Serikali ni juhudi hafifu katika hatua zote za kukabiliana na uharibifu wa mazingira ambao umefanywa na ujio wa wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina haja ya kushika mshahara wa Waziri baadaye ingawaje nimejiandaa kuukamata, ningependa nipate maelezo ni kitu gani kama Serikali inafanya kwa mazingira ambayo yameharibika kwa miaka 40 iliyopita na iko mito ambayo iko mbioni kupotea, Mheshimiwa Waziri wewe unajua Mto Makere sasa hivi umepotea, ule mto hautumiki tena. Chepechepe ya Malagarasi ambayo ni ardhi oevu na imetamkwa na UNESCO iko katika hatari ya kupotea kwa sababu ya harakati za binadamu na nyingi zikisababishwa na wakimbizi.
Ningeomba Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha hotuba yako ili tusigombanie mshahara wako ueleze ni hatua gani za makusudi zimefanywa kwa Mkoa wa Kigoma, Mkoa wote tumeathirika katika jambo hili, uhalifu ni mwingi, ujambazi ni mwingi, maradhi ya kuambukiza ni mengi kwa sababu ya ujio wa wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni shahidi, juzi ulikuwa Kigoma umeona mambo ya ajabu katika makambi ya wakimbizi, tunaomba jambo hili Mheshimiwa Waziri utueleze hatua gani zimefanyika katika ku-mitigate janga na mazingira vis-a-vis ujio wa wakimbizi katika Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kwa ruhusa yako niliseme kidogo ni hili la Muungano. Hili jambo linazungmzwa, nina bahati nzuri nilishiriki katika harakati za muafaka tu, nilishiriki najua harakati zake. Mheshimiwa Waziri, CCM tumeshinda Uchaguzi Zanzibar, CCM tumeshinda Bara, lazima sasa wakati umefika Chama cha Mapinduzi na Serikali zetu mbili tufungue milango ya mazungumzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya kisiasa hayaondolewi na uchaguzi, migogoro ya Kijeshi haiondolewi na uchaguzi, migogoro ya kiusalama haiondolewi na uchaguzi, migogoro ya kiusalama ya kisiasa inaondolewa na mazungumzo. Tufungue milango tuzungumze. Sisi ndiyo wa kupoteza, wana CCM ndiyo wenye mali, hawa wenzetu hawana mali sisi ndiyo tuna dhima ya kulinda mali hii. Nina hakika na naamini bila kutia mashaka kabisa kwamba hatuwezi kuiacha Zanzibar kama ilivyo, lazima tuzungumze ili hatimaye Muungano huu uweze kuwa na hatima ambayo itatusaidia kusonga mbele. Muungano tunauhitaji sana, acha kunipotosha wewe hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa niliseme ni athari pana za mazingira. Nitoe ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, nchi yetu inakabiliwa na jangwa na wewe umeeleza vizuri kwenye kitabu chako. Nchi yetu inaathiriwa na kuzurura ovyo kwa mifugo kila pembe za nchi yetu. Wakati umefika jambo hili la uharibifu wa mazingira, jambo hili la nchi yetu kuingia katika athari na hatari ya jangwa haliwezi kuondolewa na Wizara moja, ni vizuri Ofisi ya Makamu wa Rais, iongoze harakati hizi za kukaa pamoja ili jambo hili lipate suluhu ya kudumu ili wakulima na wafugaji sasa watulie na athari hizi za tabianchi ziweze kutazamwa kwa ujumla wake kama Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ni makubwa sana kila mahali kuna shida, naamini kabisa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano mnaweza kuwa ndiyo vinara, mkasikia will kuhakikisha kwamba tatizo hili la mazingira mnatazama kwa ujumla wake kama Serikali na kamwe siyo Wizara moja moja kama ambavyo tunaiona inatokea sasa hivi, kuna migogoro katika maeneo mengi sana na yote inatishia uhai wa mazingira ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo umelizungumza katika ukurasa wa 41, Mheshimiwa Waziri umezungumza kwamba kuna mwongozo umeutoa wa elimu ya hifadhi ya mazingira, ingekuwa vizuri hizo nakala 1,050 ambazo umesema zimesambazwa basi nakala chache Wabunge tuko siyo chini ya 400, Wabunge wote tupate nakala ya huo mwongozo wa elimu ya mazingira kama ulivyoeleza kwamba mmeusambaza katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo muhimu sana ili na Waheshimiwa Wabunge waweze kufanya kazi hii katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niwaombe wenzetu wa NEMC, katika hotuba yako umezungumza majukumu makubwa sana ya NEMC, ukaguzi wa viwanda, ukaguzi wa majosho, ukaguzi katika hifadhi zetu za wanyama, ukaguzi wa mahoteli. Naomba kupitia kwako wawekezaji wengi wanalalamikia muda mwingi ambao unatumiwa na NEMC katika ukaguzi wao, matokeo yake wawekezaji wengi wamekuwa wakinung‟unika sana na manung‟uniko yao ni pamoja na urasimu usiokuwa na sababu kabisa za wenzetu wa NEMC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumza na wenzetu wa NEMC wako wasomi wazuri tu wakiongozwa na Dkt. Baya, ni wazuri sana, shida yao ni rasilimali fedha, rasilimali watu. Huwezi ukazungumzia uwekezaji wenye nguvu kama taasisi hizi zinazopaswa ku-facilitate uwekezaji bado ni dhaifu. Wenzetu wa NEMC wapeni nguvu, waongezeeni fedha ili kaguzi zao katika miradi mbalimbali ya uwekezaji uweze kwenda na iende kwa wakati. Kuchelewa unajua wawekezaji hawa lengo lao kubwa ni wakati, haiwezekani mtu anajenga kiwanda chake au hoteli anahitaji miezi mitatu ya ukaguzi, anawasubiri NEMC, anajenga service station anahitaji miezi mitatu, minne kusubiri NEMC haiwezekani! Tumezungumza nao wanasema shida yao kubwa ni resources, hawana fedha za kutosha na waongezewe wataalam wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nitaunga mkono hoja hii kama nitasikia hatua ambazo zinafanyika za ku-mitigate masuala ya wakimbizi katika Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, na-reserve jambo hili la kuunga mkono hoja hii mpaka nitakapopata maelezo mazuri kuhusu hatua ambazo zinafanyika kwa Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru na sina haja ya kugombana na Waziri kwenye mshahara wake, nitaunga mkono nitakaporidhika na maelezo yake. Ahsante sana.