Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze na kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia uzima na kuniwezesha kusimama hapa kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na timu yake yote ya Watendaji kwa kazi kubwa ya kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Ukusanyaji wa fedha ni jambo moja, lakini kutumia vizuri na kwa wakati ni jambo lingine ambalo ni muhimu zaidi katika maendeleo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo yanayotumia fedha nyingi tukiacha mishahara ya Watumishi wa Serikali, lakini asilimia zaidi ya 60 hadi 70 zinatumika katika manunuzi ya umma. Eneo hili limekuwa na changamoto kubwa sana tena kwa muda mrefu na kwa miaka mingi. Manunuzi ya umma hayaendani na thamani ya fedha ambazo zinatumika katika kununua bidhaa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni wakati sasa nilitarajia kuona katika taarifa ya Waziri pia, kwamba, tatizo hili ama changamoto hii ya muda mrefu imeweza kuangaliwa kwa kiwango gani na utatuzi wake ukoje kwa sababu ni eneo muhimu sana katika rasilimali fedha ambazo hatunazo katika nchi yetu ambazo zinatosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Tunaiomba Serikali wakati inaainisha iweze kutupa ni namna gani sasa inaenda kuhakikisha kwamba, fedha zinazotolewa katika manunuzi zinakwenda sambamba na ubora wa bidhaa zinazotumika hasa katika maeneo ya ujenzi katika nyumba za Serikali zinazojengwa, na katika barabara, eneo ambalo limekuwa changamoto kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wizara ya Fedha. Tunaambiwa kwamba, takwimu zinasema hadi kufikia Februari, 2017 Wizara ilipokea shilingi trilioni 27.4 ambayo ni sawa na asilimia 3.5 tu ya fedha zote za maendeleo ambazo zimeidhinishwa na Bunge. Tena isitoshe katika hizo fedha trilioni 27 tuliona kwamba, trilioni 1.9 ni fedha za ndani na fedha trilioni 25.4 na zaidi kidogo ni fedha za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunaona kwamba, hata Wizara ya Fedha yenyewe sehemu kubwa ya fedha inazotumia kwa miradi yake ni fedha za kutoka nje, hili ni suala ambalo kidogo ambalo halipendezi katika taratibu zetu za Serikali. Tunajua uncertainity za fedha za nje, fedha za wafadhili ambazo zinaweza zikakwama hapa na pale. Tunaiomba Serikali na kuishauri Serikali iweze kubuni mikakati mbalimbali ya kuweza ku-raise fedha za ndani, ili ziweze kutekeleza miradi yake ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima la mafungu ya Wizara ya Fedha. Katika Mafungu nane yaliyo chini ya Wizara ya Fedha, ukisoma taarifa ya Waziri ni Mafungu matatu tu yaliletewa fedha ambazo ziko zaidi ya asilimia 60, lakini asilimia 50 na kwenda chini ndio mafungu yaliyobakia, sasa hii ni hatari. Tunataka kujua pengine ni vizuri Waziri atuambie ni nini tatizo la Hazina kuchelewesha utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo miradi iliyo chini ya Wizara ya Fedha na hata miradi mingine ya miradi ya maendeleo katika nchi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imekuwa changamoto, wananchi wengi wanalalamika kwamba, kwa nini Serikali na Bunge inaidhinisha fedha za kutosha, lakini hazifiki kwa wakati na zinafika chini ya kiwangi kilichoidhinishwa na Bunge. Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 ipo sasa hivi, inaeleza kwamba ni vema fedha zilizoidhinishwa na Bunge ziweze kutolewa kwa wakati, ili miradi ya maendeleo iweze kutekelezwa kwa wakati. Hili limekuwa tatizo sugu, tunaiomba Wizara ya Fedha wakati inahitimisha ituambie ni changamoto gani ya Hazina kutotoa fedha kwa wakati, ikiwepo hata zile za kufadhili miradi ambayo iko chini ya Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kupata ufumbuzi wa kuchelewesha fedha za miradi, nashauri kwamba Wizara haijafanya kazi kubwa zaidi katika ukusanyaji wa maduhuli. Ukusanyaji wa maduhuli ni jambo jema, ni jambo la muhimu sana, lakini pamoja na hilo la pili ni kuhakikisha kwamba, Deni la Taifa halipandi. Vilevile kuhakikisha kwamba, thamani ya shilingi yetu haishuki. Mambo haya matatu ambayo ni jukumu la Wizara ya Fedha ihakikishe kwamba, uchumi wa Taifa unapanda, sambamba na kuhakikisha kwamba, inasimamia maeneo haya matatu ambayo nimeyaeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia isimamie kikamilifu kushuka kwa thamani ya shilingi, hili nimelizungumzia na ninadhani hilo likisimamiwa vizuri tunaweza kuwa na maendeleo ya uhakika katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri, ukurasa wa 76, imeandikwa utaratibu wa mikakati ya kupunguza umaskini, inaeleza kufanya uchambuzi na tathmini ya miradi ya kuondoa umaskini ngazi ya Wilaya na vijiji. Sina hakika anamaanisha nini, lakini najua kulikuwa na MKUKUTA namba I,II na III ambazo hazikufanya vizuri sana katika nchi yetu. Pamoja na nia njema ya Serikali ya kuhakikisha kwamba inaondoa umaskini baina ya watu wake, lakini bado maeneo mengi, harakati nyingi ambazo zimeainishwa na Serikali katika kuondoa umaskini hayajafanya vizuri. Nitoe mfano mdogo tu wa asilimia 10 ambayo inatolewa na Halmashauri katika kuwapa mitaji wanawake na vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Halmashauri nyingi zinatoa hizi fedha kama kuondoa lawama, lakini ukiangalia kwa undani kabisa, ukienda kuulizia, hizi fedha hazijaonesha impact hata kidogo, haijulikani kapewa nani? Haijulikani riba ilikuwa shilingi ngapi? Haijulikani wamenufaika watu gani? Hata hivyo, Halmashauri zinaenda kutenga na kuzitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali katika harakati mbalimbali za kuondoa umaskini, iweze kuangalia kwa undani, iweke utaratibu mzuri na hasa tunakoelekea kupata zile milioni 50 za kila kijiji, Serikali iweke utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kila mtu ananufaika na hizi fedha ili tuone umaskini unapungua katika nchi yetu kwa nia njema ya Serikali ya kuwezesha wananchi kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie njia ambayo mimi naiamini kwamba, kwa sababu suala la utoaji mikopo, naomba labda ku-declare interest, mimi nimetoa mikopo kwa takribani zaidi ya miaka 20 kwa watu maskini na kwa ufanisi. Hivyo, naomba pamoja na nia hiyo, lakini njia ambayo ina uhakika na endelevu ni kuwawezesha wakulima, kwa sababu mkulima anaweza akalima kwa kupata fedha kuliko mtu maskini ambaye anapata mlo mmoja kwa siku, ukamwambia chukua mtaji huu kafanye biashara, hataweza kufanya biashara, atazila hizo fedha na matokeo yake hayataonekana, lakini mkulima atachanganya shughuli yake ya kila siku, atalima na ukimhakikishia soko la uhakika kwa bidhaa zake anaweza akaondoa tatizo la kipato chake, akapata mapato kwa ajili ya familia yake na hatimaye kuondoa umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo na ufugaji ndio sekta ambayo inagusa maisha ya watu wengi. Kwa hivyo, naona kwamba, Serikali ikielekeza uwezeshaji wa wakulima na wafugaji kuwapa mitaji ili waboreshe kilimo chao, si kwa namna ya mikopo yenye riba ambazo tunaziona, pale ndio mahali ambapo tunaona Serikali itaweza kuondoa umaskini kwa uhakika baina ya wananchi wake, kuliko sasa hivi kuwapa mitaji ya mikopo ambayo hatuna hakika inamlenga nani hasa, ikimlenga mtu ambaye ni maskini anayepata mlo mmoja kwa siku hatafanya kaziā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.