Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia kuwa na afya njema na kupata fursa hii ya kuchangia katika mjadala huu muhimu sana. Pili, nitoe mkono wa Baraka na kuwatakia Ramadhan Mubarak Waislam wote na hasa wa Jimbo la Kinondoni na Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili la Ramadhan vile vile niseme kwamba katika kupeana mkono wa baraka, ndugu zetu, kwa taarifa nilizonazo Zanzibar na hasa Pemba kuna uhaba mkubwa wa nafaka, kwa maana ya viazi mbatata pamoja na mihogo. Mheshimiwa Mwijage kwa sababu ni Waziri wa Biashara anasikia hili achukue fursa kuwahakikishia wafanyabiashara wetu wa bara wanajitahidi kupeleka vyakula haraka iwezekanavyo ili kupunguza ugumu huu na Ramadhan iwe nyepesi kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mwijage kwa usomaji mzuri wa taarifa ya bajeti na niombe mzee wa uchumi wa diplomasia kama wakati mwingine akiwa anamu-opt anaweza akafanya mambo yakawa mepesi sana, ameisoma vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati yangu, Mheshimiwa Dotto Biteko, kiongozi kijana, kamati yake iko makini na amesoma ripoti nzuri sana ambayo hata wachangiaji imewasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nizungumze, mimi mbunge wa Mjini na sina tatizo sana na REA I, II na III lakini mimi nina tatizo kubwa sana la bei ya umeme, tuna tatizo umeme ni bei juu sana. Bei juu ya umeme inatokana na gharama ya uzalishaji ambayo TANESCO wanaipata bila kusahau gharama za usambazaji. Hata hivyo, tuna umeme wa maji ambao gharama yake ni shilingi 36 tofauti na umeme wa gesi ambao ni shilingi 147na umeme wa mafuta tunaambiwa shilingi 368.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Wizara ya Fedha, Waziri Kivuli alisema kwamba umeme unanunuliwa kwa shilingi 500 na TANESCO wanauuza kwa shilingi 280.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia gharama hizi za uzalishaji kama tungetumia umeme wa maji na umeme wa gesi, gharama zetu za umeme zingeshuka kwa chini ya asilimia 50 ya sasa. Umeme wetu unakwenda juu sana, ni kwa sababu ya haya makampuni yanayozalisha umeme kwa njia ya dharura tuliyoingia mikataba, umeme wa mafuta, ni makampuni ambayo yananyonya sana nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna makampuni haya yanajulikana Songas, Dowans, Pan African; ni makampuni ambayo yanazalisha umeme kwa gharama kubwa na leo nimepata nafasi ya kuwauliza watendaji wetu, je, tukiacha kutumia umeme wa mafuta tukitumia umeme wa maji na gesi na njia nyingine hatuwezi ku-survive? Wanasema tunaweza, lakini tuna kikwazo kikubwa cha mikataba, mikataba tuliyoingia na makampuni ya uzalishaji umeme ni ya ajabu sana, ni mikataba ambayo mimi nashindwa, mikataba gani tunaingia, wataalam wetu wanaingiaje kwenye mikataba ambayo haina room ya kutoka? Hii ni ndoa ya aina gani? Au ndiyo ile ndoa wanayosema ya Kikatoliki?

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunatamani na tunafikiria wataalam wetu wanapoingia kwenye mikataba waweke na mlango wa dharura wa kutoka, lakini leo mikataba yetu hii ukiingia, ukitoka, unapelekwa mahakamani. Nina habari kwamba Dowans wamesimamishiwa mkataba na wako mbio wanakwenda mahakamani na kuna hatari tukalipishwa pesa nyingi. Sasa kwa utaratibu huu nafikiri tatizo liko kwa watendaji na wataalam wetu. Inakuwaje mikataba tukiingia hatuwezi kutoka? Nafikiri hili jambo si sawa na kwa kweli umeme umekuwa ghali lakini sababu kubwa ni huu umeme wa mafuta ambao hatuwezi kujitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Songas tungeweza kuachana nao, hatuwezi kwa sababu ya mikataba. Leo Dowans mnataka tuachane nao, hatuwezi kwa sababu ya mikataba. Leo Pan African tunataka kuachana nao hatuwezi kwa sababu ya mikataba. Hivi hii ni mikataba gani ambayo hawa wataalam wanaingiaje mikataba ambayo hatuna room ya kutoka? Napata taabu sana mimi hapa na kwa kweli kwa utaratibu huu nchi hii tutakuwa tunasokota kamba nyuma inaungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, TANESCO ina deni kubwa linalofikia kiasi cha bilioni 800, inadaiwa. Kama TANESCO inadaiwa zaidi ya bilioni mia nane, lazima umeme upande na ili ushuke lazima tutoke kwenye mikataba hii. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri aje kutueleza ni namna gani tutatoka kwenye hii mikataba ya kinyonyaji, mikataba ambayo inapandisha bei ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nimuunge mkono dada yangu, Mheshimiwa Najma leo amezungumza jambo zuri sana kuhusu Zanzibar. TANESCO inawa-treat ile Kampuni ya Umeme Zanzibar kana kwamba ni mtumiaji wa kawaida, wanamuuzia umeme kana kwamba wanamuuza Mr. Juma, Mr. Ali, hawazingatii kwamba yule naye anakwenda kufanya biashara. Wanamtozea mpaka Kodi ya VAT wakati na yeye alipaswa atengeneze aweze kuuza aweke na kodi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono, ni vizuri wakapewa huo u-agency, au kama itashindikana wao wana uwezo wa kununua umeme wenyewe, wanunue kutoka katika makampuni yanayozalisha umeme wafanye transfer kwenda kwao Zanzibar ili na wao liwe ni shirika ambalo linaweza kujinunulia umeme kwa watengenezaji umeme na badala yake lisiwe shirika ambalo linapitisha umeme halafu linatozwa bei ya mtumiaji wa kawaida, hii siyo fair. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka nilizungumze, tulikuwa katika bajeti ya maji, wachangiaji wengi hapa walivyochangia walionesha kwamba ili bajeti yetu ya maji ipate pesa nyingi tuongeze tozo kwenye mafuta, shilingi hamsini na mimi nilisema kuongeza tozo ya shilingi hamsini kwenye mafuta tafsiri yake hatumsaidii mwananchi wa kawaida, kwa sababu yeye atakwenda kuilipia hii kwenye upatikanaji wa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikapendekeza kwamba, tuna hawa jamaa zetu wa EWURA, wao wanasimamia vinasaba na juzi tu hapa kulikuwa na mchakato wa kumpata mzabuni wa vinasaba. Tenda imefanywa, makampuni yamejitokeza, makampuni matatu yaka-qualify kwa kutumia vigezo walivyoviweka EWURA na Makampuni yaliyo-qualify ilikuwa ni SICPA, SGS na kampuni nyingine ambayo jina lake sikulipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya makampuni ukiangalia tenda waliyoweka hii kampuni ambayo inaonekana imeshinda tenda bei yake ni kubwa. Nilipendekeza hapa, ni vizuri sasa watu wa EWURA wakaisaidia nchi kutafuta mkandarasi ambaye ame-tender kwa gharama ya chini iliā€¦ (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.