Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

MHE. HASNA S. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Kigoma Kusini nishukuru kwa kunapata nafasi ya kuchangia Wizara hii nyeti, Wizara ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze sana kwanza kwa kumpongeza Waziri aliyewasilisha makadario ya bajeti ya Wizara hii kwa kushirikiana na Mheshimiwa Naibu Waziri. Natambua kwamba uwezo wanao na wanaweza kufanya kazi vizuri katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuzungumzia suala la Jimboni kwangu, naomba nimpongeze sana Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, kwa hatua nzuri aliyochukua ya kuunda Tume. Leo tumesikia hapa taarifa ya upande wa pili unaonesha masikitiko kwamba Rais ameanza kwa kazi ndogo walitaka aanze na mikataba lakini tarehe 29/03/2017 sote tunatambua kwamba Mheshimiwa Rais aliunda Tume na ikafanya kazi yake chini ya Profesa Mruma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wote ni mashahidi, Mheshimiwa Rais alitumia uwazi, akaitoa ile taarifa kwa uwazi kwenye vyombo vya habari, wananchi walioko vijijini, wanaotumia redio walisikia, wenye kuona luninga waliona na akasoma taarifa. Kwa mfano kwenye yale makontena 277 kwa taarifa aliyoitoa Mheshimiwa Rais wetu ilionyesha kwamba Watanzania kupitia hayo makontena 277 tunapoteza takribani bilioni 676. Halafu leo tunasema hii ni kitu kidogo wakati pesa hizi zinazopotea tungezipeleka kwenye majimbo yetu, Serikali ingeelekeza kwenye kujenga hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kwenye makontena hayo wakati Mheshimiwa Rais anatoa taarifa imeonekana pia tuna upotevu wa copper na sulphur. Kwa mfano, nilikuwa naangalia kwenye taarifa ya copper inaonesha kwamba kwenye kila kontena tuna tani 20 za copper zinazopotea. Ukijumlisha yale makontena yote 277 unapata tani 1440.4 zenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni
17.9. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonishangaza sisi wote tunafahamu wakati sisi wageni hatujaingia Bungeni siku za nyuma tulikuwa tukiangalia Bunge tunawasikia wapinzani wanaisema Serikali ya Chama cha Mapinduzi inakumbatia mafisadi na wanasema Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaachia rasilimali za nchi zinaibiwa. Leo Mheshimiwa Rais amewasikia kwamba wapinzani walikuwa na vidonda sasa anajaribu kuona ni jinsi gani anaponyesha vile vidonda walivyokuwa navyo siku za nyuma. Raha ya donda, ukiwa na kidonda chochote lazima kipate dawa, iwe ni dawa ya kizungu, iwe ni dawa ya kienyeji lakini lazima kipate dawa. Mheshimiwa Rais analeta dawa kwa kuanza na haya makontena 277 lakini tunasema kwamba angeanza na mikataba, angeanza na mikataba wapinzani hao hao wangesema Rais kakurupuka, anaanzaje na mikataba kabla ya kufanya uchunguzi. Sasa ameanzia makontena ndugu zangu ili kubaini hivi kweli huu mchanga unapopelekwa nje tunaibiwa au hatuibiwi? Kamati imetueleza kuwa tunaibiwa na Mheshimiwa Rais ametuambia anajiandaa kutoa taarifa ya pili kwa nini jamani tusimpe muda tukaisikiliza na ile taarifa ya pili ili tuweze kuona inatuletea nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka siku za nyuma wakati wa makelele ya ufisadi, tunaibiwa rasilimali zetu, Baba Askofu, Mwadhama Kadinali Pengo wa Jimbo la Dar es Salaam Katoliki aliwahi kuhoji, hivi hawa wanaopiga kelele kwamba Watanzania wanaibiwa rasilimali zao zinatoroshwa, wanaongea kwa uchungu wa dhati au wanaongea kwa sababu wamekosa fursa na wao ya kuiba? Mimi nilifikiri kwenye suala hili tusimame kama Watanzania, tusimame kama nchi, tuache itikadi zetu, tumpe moyo Rais. Kama hatumpi moyo atafikia wapi kuwaza kuichambua na mikataba, kutoa fursa ili Bunge nalo tuletewe hiyo mikataba tuipitie na tumsaidie Rais kubadilisha yale ambayo tunaona ni upungufu?

Kwa hiyo, naomba sana tuwe na subira ndugu zangu, mambo mazuri hayahitaji haraka. Tume imetoa taarifa ya kwanza tusubiri taarifa ya pili na nina imani Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni mtu makini na atatupa taarifa ya pili na kwa taarifa zilizoko huko nje ni kwamba Watanzania wamefurahi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku ile Rais anatoa taarifa kaka yangu Mheshimiwa Tundu Lissu hapa alihojiwa na waandishi wa habari akasema wao kama Upinzani wamekuwa wanapiga kelele siku nyingi sana lakini Serikali haichukui hatua, leo Serikali inachukua hatua tunasema nini sasa, si tuipongeze? Halafu jamani ndugu zangu tujenge utamaduni wa kupongeza au kukosoa Serikali pale ambapo inapostahili, sio kila kitu tupinge. Hata nyumbani kwako inawezekana kabisa ukirudi mke unamnunia lakini siku akikupikia chakula kizuri si ni lazima umsifie, umwambie kwamba leo mke wangu umenipikia chakula kizuri ili kesho apate nafasi ya kwenda kununua zaidi na aweze kukupikia zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumpongeza Rais na hiyo jitihada aliyofanya, naomba sasa niende kwenye Jimbo langu. Jimbo langu lina vijiji 61 tuna umeme kwenye vijiji kumi tu.

Kwenye REA Awamu ya Pili tulipata vijiji kumi vya Kandaga, Mlela, Kazuramimba, Kalenge, Uvinza na Mwamila lakini kwenye Awamu hii ya Tatu ya REA pia tumepangiwa vijiji kama 11. Rai yangu, naomba Waziri ambaye amewasilisha hapa waweze kushirikiana na Naibu Waziri na Mkurugenzi wa REA Tanzania Ndugu Msofe waone ni jinsi gani wanatusaidia wananchi wa Uvinza ili basi tuweze kuongezewa vijiji. Ni jambo la aibu kuona tangu uhuru vijiji 61 tuna umeme kwenye vijiji kumi tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawapongeza kwanza wametufikiria kwa mara ya kwanza tunapata umeme mpaka Kijiji cha Malagarasi kwenye Kata ya Mganza. Najua huu ni mwanzo mwema ndiyo hatua sasa ya kupeleka umeme kwenye Tarafa yangu ya Nguruka. Kwa maana utoke pale Malagarasi uende Mlyabibi, Bweru mpaka Nguruka. Nina imani kwa sababu Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu itayapokea haya na kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.