Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

Hon. Sixtus Raphael Mapunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kuipongeza Wizara kwa hotuba nzuri ambayo kwa kweli ukiitizama kwa kina inatoa matumaini ya Taifa letu kwenda kwenye nchi ya viwanda hasa ukizingatia msingi mkuu wa Taifa la viwanda unatokana na Wizara hii ya Nishati na Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 kipindi cha kampeni, Rais wetu mpendwa wakati anajinadi alipofikia kuongelea suala la sekta ya madini alijipambanua pasipokuwa na kificho kwenye changamoto kubwa tano zinazoikabili Wizara ya Nishati na Madini au katika ujumla wake sekta ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu mpendwa alizunguka nchi nzima akasema, toka tumeingia ubia na wabinafsishaji na hawa wenzetu, tukawapa migodi wakashirikiana na sisi tumepita kwenye changamoto kubwa zifuatazo:-

(i) Kunyanyaswa kwa wachimbaji wadogo, sambamba na kulipwa fidia ndogo wawekezaji wanapotwaa maeneo. (Makofi)

(ii) Sekta ya madini ina usimamizi mbovu unaopelekea Serikali kukosa mapato. (Makofi)

(iii) Sekta ya madini inakutana na changamoto ya kutoroshwa kwa madini kwa njia mbalimbali kunakoipotezea Serikali mapato. (Makofi)

(iv) Sekta ya madini inakutana na changamoto ya mikataba mibovu inayoipunja Serikali mapato. (Makofi)

(v) Sekta ya madini inakutana na tatizo la matumizi mabaya ya misamaha ya kodi ambayo wawekezaji wamepewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais akamalizia kwa kusema mkinipa ridhaa ya kuongoza nchi hii, nitahakikisha haya mambo matano nakwenda kuyafanyia kazi. Watanzania wakamuamini wakampatia Urais, akaingia ofisini toka siku kwanza kipindi cha hotuba yake hapa Bungeni akasema nchi yetu tajiri, nchi yetu ina rasilimali nyingi, tukizitumia rasilimali zetu vizuri nchi yetu itakuwa donor country. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina uhakika aliyasema haya kwa sababu alikuwa anaijua Tanzania vizuri. Akajipa muda wa kutosha, akai-study hiyo sekta ya madini akaja kugundua kuna makinikia yanatoweka nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yote niliyoyasema yapo kwenye changamoto namba tatu niliyosema sekta ya madini inakutana na utoroshwaji wa madini, kwa namna yoyote ile iwe hoja ya kisheria, iwe hoja ya mahusiano, hoja ya kutoroshwa kwa madini yetu Watanzania Rais alikwishaisema na akafanyia kazi. Leo hii namshangaa Mtanzania yeyote yule anayehoji modality au namna Rais alivyoitengeneza Tume ya kwenda kuyakamata na kuyachunguza yale makontena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu mmoja anaitwa Edmund Burke na baadaye Abraham Lincoln na Martin Luther the King waliwahi kusema, evils will prevail if good people do nothing. Changamoto zote za madini tunazoziona zitaendelea kuwepo kama watu wazuri hawatafanya kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, alichokifanya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni ile segment ya watu wazuri wanapofanya jambo ambapo kuna uovu. Kinachonishangaza mnataka uovu tuutengenezee modality? Unavyokwenda kumkamata mwizi unataka umtaarifu mwizi kesho nitakuja kukukamata, ujiandae pamoja na mtu wa kukuwekea dhamana ili ukifika Mahakamani tukutoe, jamani! Hivi kweli sisi ni wazalendo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonikwaza zaidi hii ajenda kwa muda mrefu pioneers walikuwa wale pale. Pioneers wa ajenda hii kwa muda mrefu walikuwa wale pale, tutawataja kwa majina.

Mheshimiwa Naibu Spika, waliosema hizi changamoto tano wale kule, Mheshimiwa Mnyika umewahi kusema, Mheshimiwa Mwita Waitara umewahi kusema, Mheshimiwa Tundu Lissu amewahi kusema, hawa ndiyo waliosema hayo mambo matano. Tena wakasema mnakaa na hii mikataba ya nini si vunjeni, hawakusema wale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilichowafanya leo wabadili gia angani ni nini? Hawa watu wana tatizo la uzalendo, niwaombe ndugu zangu tuwe wazalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu yeyote anayeona shaka ambapo kuna evils and good people they are doing something halafu akawatilia mashaka, kwa kweli napata shida sana kuwaelewa. Nilichotarajia kutoka kwao, kwanza wangesema tunakushukuru Rais, tumesema kwa miaka mingi hakuna aliyewahi kutusikiliza wewe umetusikiliza halafu ndiyo twende yale mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mnyika amekuja hapa ana hoja ya mikataba it is true, mikataba ni tatizo hakuna mtu anayepinga na Rais alishasema mikataba ni tatizo. Nilichotegemea waseme makinikia ndiyo foundation ya mjadala ya mikataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakwenda kwenye kujadili mkataba ukiwa na evidence tunaibiwa kwa kiasi gani, ninyi wawekezaji rekebisheni hapa kwa sababu tumethibitisha pasipokuwa na shaka lolote mnatuibia. Sasa mnataka twende tujadili terms za mikataba hatuna kitu mikononi?

TAARIFA....

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Ahsante sana Mheshimiwa Bashe, kwanza naipokea taarifa yako kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna siku hapa niliwahi kusema story ya jongoo na mwana jongoo.Katika misingi ileile ya habari ya jongoo na mwanajongoo. Unapotaka kutatua matatizo katika sekta hii ya madini lazima uwe na sehemu ya kuanzia. Hivi mnataka tuanzie wapi kwenye hili?

TAARIFA ....

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba unilindie muda wangu wameuchezea sana. Hii taarifa ngoja niipe maelezo mazuri ili iwe taarifa iliyokamilika kwa sababu haijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wowote wa kisheria kuna mhimili unaitwa mhimili wa Bunge ndiyo unaotunga sheria na mfumo wowote wa kuongoza nchi katika namna yoyote ile chimbuko lake ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Upungufu wowote unaoonekana ninyi mlikuwepo na sisi tulikuwepo. Ajenda ya sheria zote zilizopitishwa humu ndani ninyi mlikuwepo sisi tulikuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, my concern is not about the past, my concern ni sasa tunapoanza kupiga hatua. Tumeliona tatizo, tunatatua tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napata shida sana kuwaelewa watu wa aina kama ya akina Mheshimiwa Mwita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna kichekesho cha mwaka kama kile ambapo mtu umeliona kosa, unalirekebisha halafu mtu anatokea anakuambia kwa nini ulikosea si uendawazimu huo? Yaani mimi napata shida kuelewa, kosa limetokea unalirekebisha, katika process ya kulitatua tatizo unasema eti kwa nini ulikosea, ni akili za chizi tu zenye uwezo wa kufanya mambo kama haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.