Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii ili nami nichangie hotuba hii muhimu ya bajeti.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mwaka jana wakati nachangia hotuba hii ya bajeti nilisema hawa Madaktari wawili wa Uchumi, Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mheshimiwa Dkt. Ashatu, kama tutawapa support watatufikisha mbali

sana, wengi hawakunielewa, lakini kutokana na uwasilishaji huu wa hii bajeti ambayo wengi wanaiita bajeti ya karne nadhani yale niliyoyasema mwaka jana yamethibitika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana wakati Mtemi Chenge anaahirisha Bunge, alitoa maangalizo mazuri sana, kwamba jamani hii bajeti haya ni mapendekezo, sisi tunatakiwa tutie nyama, tutoe maoni yetu. Sasa mimi nina machache ya kujazia kwenye bajeti hii nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Mpango.

Mheshimiwa Spika, vyanzo vya mapato, mimi natokea Mafia, kule Mafia tunavyo vyanzo vya mapato na ukusanyaji wa mapato ambao kwa mitazamo yetu tuliopo Mafia kule tunaona kwamba Serikali inapoteza mapato mengi sana. Tuna taasisi kule, inaitwa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari hawa kazi yao kubwa ni uhifadhi wa bahari, lakini wamejiingiza katika masuala ya ukusanyaji wa tozo.

Mheshimiwa Spika, tungeomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango na kupitia Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wakichukue hiki chanzo, wawaagize TRA Mafia waanze kukusanya ile entry fees ya watalii wanaoingia katika maeneo ya hifadhi, tunawabebesha mzigo watu wa hifadhi ya bahari ambao si wao, kwa sababu wao wanatakiwa washughulike na hifadhi. Haya mambo ya kukusanya mapato yana wataalam na wataalam wa TRA wapo pale, Ofisi ya TRA ipo pale Mafia.

Mheshimiwa Spika, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri achukue haya maoni na amwagize Kamishina wa TRA amwaagize Meneja wa TRA pale Mafia, waanze kukusanya mapato yale kutokana na watalii. Hawa watu yale mapato wanashindwa hawana capacity, hawana uzoefu, hawana wataalam, matokeo yake pale tunakadiria kupata karibuni bilioni mbili kwa mwaka lakini wao wanakuja kutuambia kwamba tumepata milioni 700 milioni 600.

Mheshimiwa Spika, kinachoshangaza sana wanayatumia vibaya, wanarundika mle gharama za uendeshaji nyingi sana, likizo yao yamo humo, safari zao zimo humo, makongamano yamo humo na mambo chungu nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kibaya zaidi haya mapato mwisho wa siku Halmashauri ya Mafia inatakiwa ipate asilimia 10. Sasa wenzetu wanavyorundika haya matumizi wanasema kwamba asilimia 10 hiyo baada ya kutoa gharama zote. Sasa gharama wanarundika mambo chungu mzima. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie aagize Mamlaka ya Mapato waanze kufanya kazi hiyo ya kukusanya mapato katika entry fees ya watalii kule Mafia.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linaweza likatusaidia sana kwa mapato limesemwa hapa asubuhi na Mheshimiwa Zaynab Vulu umefika wakati sasa tufungue hii Southern Circuit ya utalii kwani kuna fursa kubwa sana za utalii. Kama nilivyotangulia kusema mimi natokea Mafia, Mafia kuna fursa kubwa sana za kiutalii ikiwemo yule samaki anayeitwa potwe ambaye ni samaki maarufu sana duniani na anapatikana Mafia na Australia tu, lakini kwa bahati mbaya sana hatujaanza kumtangaza vizuri na watalii wengi wanakuja pale. Naomba sana Serikali ituangalie, tutangaze vivutio hivi, lakini sio tu kutangaza vilevile kuna tatizo la accessibility ya kuingia Mafia. Hiyo ndiyo hoja yangu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, usafiri wa kuingia Mafia ni mgumu, sasa hawa watalii watapita wapi, hatuwezi kila mtalii apande ndege afike Mafia, lazima wapite njia ya bahari, lakini njia ya bahari kwa bahati mbaya sana kuna matatizo, hakuna boti za kisasa, kuna magogo yale. Kwa hiyo tungeomba sana Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Waziri wa Ujenzi watusaidie sana pale Mafia kutupatia boti ya kisasa ambayo watalii wanaweza kuja, bahati nzuri Naibu Waziri wa Ujenzi Mzee Ngonyani nimemwona hapa, watupatie boti ya kisasa ili tuweze kufungua ile fursa ili watalii waje kwa wingi na wasafiri vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hilo kwa kuwa Mheshimiwa Ngonyani nimemwona suala la Gati la Nyamisati, Gati ya Nyamisati mwaka jana zilitengwa pesa hapa na nilitoa angalizo jamani hizi pesa ziende zikafanye hiyo kazi, tumebakiwa na wiki hazizidi mbili mwaka wa fedha unakwisha pesa zilitengwa, gati halijaanza kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana ndugu zetu wa Wizara ya Ujenzi...

TAARIFA ....

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, kuna tofauti kati ya Potwe whale-sharks na dolphins, kama yeye anazungumzia dolphins wanapatikana maeneo hayo aliyoyasema. Mimi namzungumzia whale-shark - potwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Mheshimiwa watufungulie njia ya usafiri kwa upande wa Mafia, gati lile pesa zilitengwa, lakini mwaka unakwisha ujenzi haujaanza, tunaingia mwaka mwingine. Naomba sana Mheshimiwa

Waziri zile pesa zisiwe kama tena zimepotea, tutakapoingia mwaka mwingine wa fedha ule mchakato wa kujenga lile Gati la Nyamisati na kufungua fursa za utalii pale, ziweze kufikiriwa.

Mheshimiwa Spika, lingine suala la utalii kwa upande wa Mafia tulikuwa na Hoteli pale na ndugu yangu Mheshimiwa Maghembe anaifahamu. Hoteli ile ya Chole Mjini, ilifungwa kutokana na matatizo ya uendeshaji wa yule mmiliki pale. Kwa kiasi kikubwa sana yale matatizo yameshakwisha, pale ni chanzo kikubwa sana cha mapato. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Utalii na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI wakishirikiana kwa pamoja watufanyie utaratibu hoteli ile ifunguliwe ili Serikali isiendelee kukosa mapato.

Mheshimiwa Spika, tunahitaji watalii na utalii wa Mafia zaidi ni wa scuba diving, sport fishing na vitu kama hivyo. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho hapa, aligusie hilo na kwa kushirikiana na Wizara hizi nilizozitaja ili tuweze kufungua fursa za utalii pale Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utalii pia unakwenda sambamba na miundombinu iliyo bora, barabara ya kutoka Kilindoni kwenda Rasi Mkumbi kilometa 55 na Mheshimiwa Waziri alizungumza kwa uchungu sana tunakwenda kubana matumizi, bajeti hii ni ya kubana matumizi. Nilizungumza wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mbarawa kwamba kule Mafia kuna tatizo, kile ni kisiwa kuna udongo ambao unakwisha...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana.