Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Peter Ambrose Lijualikali

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nataka nizungumzie ushuru wa mazao ambao Mheshimiwa Waziri ametoa kwa mazao ya kilimo. Alisema kwa hawa wakulima ambao wanasafirisha mizigo yao kwa maana ya mazao kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine, kama ni mzigo usiozidi tani moja wasitoe ushuru.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri sana mimi nina Halmashauri mbili, ya Ifakara na Kilombero. Wananchi wangu hasa wa Ifakara wengi wanalima Halmashauri ya Kilombero wanakuja Ifakara hapa katikati huwa kuna barrier ambapo huwa wanawekwa pale Askari Polisi wenye bunduki kwa ajili ya ushuru. Kama Halmashauri ya Kilombero tulisema mkulima kutoka Ifakara anayelima Kilombero, akirudi na magunia yasiyozidi 20 anapita bure.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa hili agizo kwamba tani moja ndiyo ipite, tani moja ni wastani wa magunia 10 maana yake ni kwamba tayari tumesha-confuse utaratibu wetu kule Ifakara. Maana yake tunawaambia wananchi wa Ifakara kama tulikuwa tunasema wapite na magunia 20 sasa wapite na magunia 10 tu kwa mujibu wa sheria hii, tayari ni confusion. Maana yake ni kwamba hapa sasa hatusadii.

Mheshimiwa Spika, mimi nasema tani na ningependa unisikilize mpaka mwisho kwa sababu katika hicho kizuizi wanapokaa askari hapo, mkulima hata kama ana gunia tano za mpunga, hawezi kuchukua fuso au usafiri mkubwa kwa ajili ya kubeba hizi gunia tano, maana yake lazima wakulima watachanga, watakodi usafiri mkubwa waweke kwenye hilo gari waweze kuja Ifakara. Haiwezekani mkulima atoke na mzigo Idoko akiwa na gunia 10 atembee nazo mpaka Ifakara, hawezi kukodi maana yake lazima wachange wawe wengi. Wakifika pale wanaambiwa huu mzigo ni wa mtu mmoja wakati wale ni wakulima wengi wamechanga gari.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hili Mheshimiwa Waziri aliangalie, aende kule Ifakara aweke sawa, haiwezekani mkulima mmoja akodi gari wakati ana magunia matano au sita maana yake lazima wakulima wengi wachange kwenye hili gari moja ili wawe na mzigo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niseme nina shida ya barabara pale, barabara yangu ya kutoka Kidatu mpaka Ifakara ni mbovu kwa miaka mingi. Sasa Mheshimiwa Waziri nimeambiwa imetengwa shilingi milioni 300 kwa ajili ya fidia, maana barabara hiyo sasa hivi ndiyo inataka kujengwa, hivi kutoka Kidatu mpaka Ifakara pale kuna nyumba ngapi, ni nyingi sana. Hii fidia ya shilingi milioni 300 ni takribani nyumba mbili tu hizi, hawa wengine fidia yao iko wapi? Kwa hiyo, naiomba Serikali kama ina ya dhati ya kujenga barabara hii, fidia iongezwe siyo hii hela ndogo ambayo imewekwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo lingine, hotuba ya Mheshimiwa Msigwa, hii hotuba ya akili ndogo nafikiri itaishi milele. Kwa sababu mambo yanayotokea leo katika nchi hii yameshasemwa miaka mingi sana na hata Msigwa alisema akili ndogo haiwezi kuongoza akili kubwa. Leo ambacho kinatokea hapa ni kwamba akili ndogo ile ambayo ilikuwa inapiga makofi wakati sheria mbovu zinatungwa hapa Bungeni, ile akili ndogo wakati akina Zitto wanasema hawa Mawaziri wanakwenda kusaini mikataba nje, Waziri anapewa ndege aende nje akaingie mkataba mlikuwa mnapiga kelele nyie mnasema kwamba huyu Zitto mwongo, hafai na ametumwa, Zitto akafukuzwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati haya yanatokea huyu Rais wetu alikuwa pale amekaa. Wakati Mnyika anaongea haya maneno kwamba nchi hii inaibiwa, nchi hii inafilisiwa, mlikuwa mnapiga makofi nyie, akili ndogo hiyo inapiga makofi. Akili kubwa akina Msigwa, Zitto na Mnyika wakati wanasema haya maneno walionekana wabaya.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu unakuja hivi, kwa kuwa tumeshasema na kama Taifa tumeona kwamba Acacia ni wezi na kwa kuwa na Rais amesema hawa watu wanatakiwa wafanyiwe kazi, kwanza lazima kinga ya Rais itolewe, tufanye amendment hapa, Marais wa nchi hii wasiwe na kinga ya kutokushtakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu hainiingii akilini wakati leo unamwambia Karamagi, unamwambia mzee wangu Chenge kwamba wahojiwe Marais waliopita wanaachwa. Haiwezekani Chenge alifanya makosa Rais asijue, haiwezekani Cabinet ilikuwa haijui. Tufanye amendment ya sheria Marais wote na hii vita siyo iwe ni one man army, isiwe vita ya jeshi la mtu mmoja ndiyo lipigane iwe vita ya Taifa zima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ni kuomba radhi, CCM lazima muombe radhi kwa hasara ambayo mmeleta kwenye Taifa hili. Leo hapa mnajifanya mnapiga makofi, mnashangilia wakati nyie mmeua watu, watu wamekosa madawa kwa sababu ya uamuzi wenu wa hovyo. Kwa hiyo, huo ndiyo ushauri wangu, amendment ije, Rais aombe radhi, Bunge liombe radhi na CCM muombe radhi kwa maamuzi mliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.