Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, mwingi wa Utukufu ambaye ameniwezesha kusimama hapa siku hii ya leo nikiwa na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nianze na barabara ya kilometa 130 ambayo inatoka Kitai kwenda Mbambabay. Barabara hii ni ndefu, lakini kulingana na changamoto ambayo iko katika barabara hiyo ya kipande cha kilometa 40 inayotaka Kitai kwenda mpaka pale Rwanda kwenye uchimbaji wa makaa ya mawe, mimi naomba Serikali ichukue kipande hiki cha kilometa 40 kwa maana ya changamoto yake, ili iweze kurahisisha uchimbaji wa makaa ya mawe na usafirishaji wake. Kilometa 40 hizi zitasaidia sana kurahisisha utekelezaji huu wa uchimbaji wa makaa ya mawe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niende kwenye suala la maji, wanawake wenzangu wa Mkoa wa Ruvuma wanapata shida sana kwenye eneo hili la maji. Maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma bado yana shida kubwa ya maji. Inawezekana kabisa asilimia chache sana za upatikanaji wa maji, naomba suala hili Serikali ilichukue na kuhakikisha kwamba maeneo yote ya Mkoa wa Ruvuma wanawake wenzangu wanapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika niseme kuna Benki ya Kilimo. Benki ya Kilimo hata mwaka jana nilisimama hapa. Benki ya Kilimo imekwenda kuwekwa kwenye maeneo ambayo mengine hayana walengwa sahihi wa masuala ya kilimo.

Ninaomba benki hii ya kilimo, nilisimama mwaka jana Mheshimiwa Mpango, nikakamata na shilingi yako ukaniahidi kwamba mimi hii ni bajeti yangu ya kwanza, naomba uniachie ili mimi nitahakikisha kwamba mwaka huu wa fedha Benki ya Kilimo inakwenda Ruvuma. Mpaka leo ng’oo hakuna Benki ya Kilimo, sasa sijui nikueleweje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba utakapokuwa unakuja ku wind up hapa unieleze benki hii inaanza lini? Kama shida ni majengo basi mimi nitawapa jengo langu ili wakae pale wafanye kazi hiyo. Tafadhali naomba ili wanawake waweze kukopa mikopo na wananchi wengine wote waweze kukopa mikopo waweze kufanya kilimo chenye tija ambacho kitawasababisha wapate mitaji mizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kodi ya nyumba. Kodi ya nyumba ni nzuri, hata mimi mwaka jana nilisimama hapa nikapongeza Serikali kuchukua uamuzi wa kuipa TRA iweze kukusanya pesa hiyo kwa maana ya kodi ya majengo. Lakini sasa naona kwamba yaani napata picha namna gani ambavyo utakwenda kwa mwananchi ukasimama pale akamwambia akupe shilingi 10,000 ya pamoja ni maumivu, na inawezekana kabisa utekelezaji wake utakuwka na rabsha mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mawazo yangu ni kwamba, kwenye ile tozo ya shilingi 40 tuliyoiweka tungeongeza tozo ya shilingi 50 ili iingie huko na watu waweze kulipa kodi hii bila maumivu ya moja kwa moja wanayoyaona. Na ninaamini kabisa hili litatekelezeka bila kelele zozote. Lakini pia tutenganishe nyumba, nyumba ziko za biashara na nyumba za makazi. Kwa hiyo, wale wa biashara basi wachukuliwe kibishara na hizi za makazi iongezeke tozo ya shilingi 50 ili waweze kulipa kwa mtindo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye afya. Niombe sana, kuna maeneo ambayo wakati wa Wizara ya TAMISEMI nilichangia hapa. Nikaainisha maeneo ya Namtumbo kule, kwenye Kituo cha Afya cha Rusewa, tunahitaji gari la afya, ambulance kwa ajili ya kurahisiha wanawake ambao wanakwenda kujifungua kutoka pale Rusewa kwenda kule katika Wilaya ya Tunduru. Kuna eneo ambalo lazima watembee kwa kilometa 150 ambalo wanakwenda kubebwa kwenye matenga. (Makofi)

Mheshimiwa Rais uliko huko naomba unisikie na mimi naomba ambulance moja ili iende kule Namtumbo ikasaidie wanawake wa Namtumbo katika Mkoa wa Ruvuma. Nakuomba sana baba yangu, pamoja na jitihada zote na kazi zote unazoendelea kuzifanya basi na hilo naomba wanawake wa Ruvuma kule, walikutwangia kura nyingi sana za kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nizungumzie wazabuni wa ndani. Wazabuni wa ndani kama wa mawakala wa pembejeo wamekuwa wakinyanyasika mpaka sasa hivi hawajalipwa pesa zao, naomba Serikali ione umuhimu. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wewe ni Rais wa wanyonge, unagusa kabisa matatizo ya wanyonge. Waone hawa wazabuni ambao wamekuwa wakihangaika mpaka sasa hivi hawajui hatma yao, wasaidie ili waweze kupata haki yao. Wale ambao hawajafanya vizuri wawekwe pembeni, waliofanya vizuri kwa uaminifu walipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika wazabuni wa ndani, kwa mfano wako waliohudumia mashule, vyuo, lakini pia wapo waliohudumia kwenye vikosi vya jeshi, nao pia waweze kulipwa hizo pesa ili waweze kuendeleza mitaji yao. Tunahitaji uchumi wa viwanda wakati watu wetu wa ndani tunawaumiza na kuwaangamiza na kuua mitaji yao, tuwalipe waendeleze shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anatekeleza majukumu yake na kubainisha matatizo moja baada ya lingine na kuyaondoa kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza hapa masuala ya makinikia. Makinikia yamezungumzwa na Wabunge wengi, lakini juzi mmemsikia Mbunge alizungumza hapa, Mbunge huyu anaitwa Mheshimiwa Heche, alizungumza akawa anahamasisha wananchi wake waende kuvamia migodi, kwa hiyo kazi aliyoifanya na leo anajikosha kwa kuomba mwongozo hapa. Mimi niseme tu hicho ndicho alichokitaka na amesha-organize wameenda kuvamia migodi, Rais hajasema kwamba watu wakavamie migodi, kwa hiyo, huo ni uvunjaji wa sheria, hao watu washughulikiwe kama wahalifu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo mwongozo wako umeelekeza kwamba aende kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, mimi naomba aunganishwe na yeye kama mhalifu namba moja, kwa sababu yeye ndio aliyekuwa anahamasisha hapa ndani tumemsikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie pia suala la Mheshimiwa Tundu Lissu, Mheshimiwa Tundu Lissu anapinga ripoti hii iliyotolewa ya vyombo vya utafiti uliofanyika. Mimi nataka niseme hivi, hawa wajumbe walioingizwa kwenye ile Kamati sio kwamba wanajipangia wao wenyewe, vipo vyombo mahsusi vinavyochuja na kubainisha sifa za watu ili waweze kuingizwa kwenye vyombo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchunguzi uliofanyika ni sahihi na ripoti ambayo imeletwa kwa Mheshimiwa Rais ni sahihi na ninaomba ikumbukwe kwamba uchunguzi unapofanyika na ripoti inapopelekwa maana yake mwenye haki wa hiyo ripoti ni yule ambaye aliagiza ripoti ifanyike ambaye ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, kifo cha nyani kila mti huwa unateleza, imefika mahali hawa wenzetu sasa hata wanayoyasema kwamba Rais anatekeleza waliyoyasema wao, leo hii wanayakataa tuwaeleweje? Lakini pia amesimama Mbunge hapa, ametumia dakika 10 Mbunge wa Arumemeru Magharibi ametumia dakika 10 kulalamikia shamba la maua la Mheshimiwa Mbowe, hivi ni akili ni matope. Wananchi wake hawana shughuli zingine, hawana changamoto ni mambo ya aibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia alisimama Mbunge hapa akasema sisi Wapinzani ni kioo cha Chama cha Mapinduzi, mimi sikatai, inawezekana kuwa ni kioo, lakini kioo cha sasa hivi cha huo upinzani tayari kina crack hivi mtu utajionaje? Kioo kina ukungu utajionaje, ninyi wenyewe mnaenda mbele, mnarudi nyuma hamjitambui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba lakini pia niseme, kwa maana hiyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.