Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Niseme moja kwa moja kwamba naiunga mkono hoja iliyotolewa kwa 200%. Kwa kuwa hoja ni nyingi, tunaahidi kuleta majibu ya hoja zote kwa maandishi lakini nizungumzie chache.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kulikuwa na maswali hapa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji zimetengwa wapi. Katika mwaka wa fedha ujao kiasi cha shilingi bilioni 59.5 kimetengwa kwenye Fungu 21 - Hazina, sub-vote 2001, mradi namba 4,903, uwezeshaji wa vijiji. Hiyo imefanywa kwa makusudi kuruhusu taasisi zote zinazohusika ziweze kuandaa utaratibu mzuri wa matumizi ya hizi fedha na fedha hizi zitaratibiwa na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo napenda kulisema ni hoja ya Mheshimiwa Mchungaji Msigwa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imeikuta Hazina tupu. Kama ilivyo kwa Serikali zote duniani, Serikali ya Awamu ya Tano imerithi mambo mengi mazuri kutoka Serikali ya Awamu ya Nne. Macroeconomic stability ni dhahiri, umeme vijijini uko wazi, Serikali ya Awamu ya Nne imejenga barabara nyingi na madaraja na Serikali ya Awamu ya Nne imepeleka maji vijijini. Vilevile tunakiri kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imerithi pia changamoto na hili ni kawaida kuna changamoto za kibajeti kama ukusanyaji hafifu wa mapato na kadhalika lakini si kweli hata kidogo kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ilikuta Hazina iko tupu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo inadhihirishwa na yafuatayo, Serikali imeendelea kugharamia kazi za msingi za ulinzi na usalama wa nchi yetu. Hakuna hata wakati mmoja kuanzia tulipochukua madaraka tumelegalega. Siyo hivyo tu, Serikali imegharamia shughuli za mihimili mingine yote ya dola ikiwemo Bunge. Pia Serikali imeendelea kulipa madai mbalimbali ya wakandarasi, watoa huduma na kadhalika. Si hivi tu chini ya mpango wa Policy Support Instrument na IMF ambao wanakuwa wanafanya tathmini huru ya utekekelezaji wa bajeti ya Serikali na mwenendo wa uchumi kwa ujumla, mara ya mwisho walikuwa nchini Disemba, hakuna mahali popote katika taarifa yao wanaonesha kwamba Hazina ya Tanzania ilikuwa tupu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia vigezo vya kimataifa viko bayana. Deni la Taifa ni himilivu nchi yetu inakopesheka. Tumeendelea kulipa mishahara ya watumishi bila kutetereka. Kwa hiyo, kwa kweli namshangaa sana Mheshimiwa Msigwa kwa madai yake hayo ambayo kwa kweli siyo sahihi. Kama ana ushahidi kinyume cha hayo niliyoyasema au hivyo vigezo nilivyoeleza alete uthibitisho Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya walimu waliyosimamia mitihani kidato cha nne mwezi Oktoba. Mwaka 2015/2016 tulitenga shilingi bilioni 17.7 kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa mitihani ya kidato cha nne. Hii inahusisha usimamizi, usafirishaji wa mitihani na ulinzi. Oktoba mwaka jana tulitoa fedha zote shilingi 17,762,472,220 kwa ajili ya kugharamia hiyo mitihani na hizi zote zilipelekwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi wa pili TAMISEMI ikaleta madai ya nyongeza ya shilingi 6,846,552,000. Hizi bado tunazifanyia mchanganuo kwa maana ya gharama ya malipo haya yaliyopungua na kuangalia matumizi ya fedha ambazo tulitoa awali. Uchambuzi huu utakapokamilika Serikali italipa fedha kwa wanaostahili haraka inavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya wastaafu ambao hawalipwi pensheni zao Hazina ambao hawalipwi kwa kiwango cha shilingi laki moja. Serikali imesikia kilio cha wastaafu hao kupitia kwa wawakilishi wao na tutalifanyia kazi haraka na tutalijulisha Bunge lako hatua ambazo zitachukuliwa. Kwa nafasi hii, wenzangu wa Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali wako hapa, ninawaagiza walifanyie kazi suala hili mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, madeni ya walimu. Kuna hoja kwamba Serikali hailipi madeni ya walimu, Serikali ilipe stahili za walimu. Serikali imekuwa inalipa madeni na stahili za walimu miaka yote. Nitatoa tu mfano, mwaka 2014/2015 tulipokea madai ya shilingi 19,631,843,225. Tulipofanya uhakiki tulilipa shilingi 5,665,772,117.93 ambazo tulilipa mwezi Julai, 2015. Mwaka huu wa fedha wa 2015/2016 tulipokea madai ya shilingi 29,800,000,000 na baada ya kuhakiki Oktoba, 2015 tumelipa shilingi 20,125,578,770.05.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya sababu ya kukataa baadhi ya madai, kuna madai ambayo yaliwasilishwa zaidi ya mara moja na yako madai ambayo yaliwasilishwa kwa kiwango cha juu kuliko uhalisia. Mtu anawasilisha madai ya shilingi 600,000,000; badala ya shilingi 600,000 na yako madai ambayo yalishalipwa yakawasilishwa tena na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachosema, ni lazima Serikali ipate nafasi ya kufanya uthamini kabla ya kuweza kulipa madai haya. Tuna thamini sana mchango wa walimu, tunajua sisi wote tusingekuwa hapa bila mchango wa walimu. Kwa hiyo, tutaendelea kulipa madai halali ya walimu na watumishi wengine wa umma kadiri yanavyowasilishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie jambo moja la fedha za vijana na wanawake ziko wapi kwenye bajeti? Bajeti inavyoainishwa kimataifa (International Budget Classification) huwa haiendi kwenye makundi ya jinsia, wazee, vijana na kadhalika. Ni wazi vilevile bajeti ya maji inagusa moja kwa moja akina mama, bajeti ya umeme vijijini kadhalika na barabara za vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuelekeza bajeti ya Serikali kwenye maeneo hayo ambayo yanagusa akina mama moja kwa moja, bajeti imetoa kipaumbele kwenye sekta na maeneo ambayo yanagusa wanawake moja kwa moja. Kwa mfano, kwa mwaka ujao wa fedha asilimia tano ya mapato ya ndani ya kila Halmashauri yametengwa kwa ajili ya vijana. Asilimia tano ya mapato ya ndani ya kila Halmashauri yametengwa kwa ajili ya wanawake. Shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya vijana kwenye Fungu 65, Ofisi ya Waziri Mkuu, shilingi bilioni 15 zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza ujuzi kwa vijana ambao hawana ajira na hizi nazo ziko kwenye Fungu 65. shilingi 1,955,000,000 zimetengwa kwa ajili ya kuwezesha wanawake kiuchumi na ziko Fungu 55.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Serikali inatambua umuhimu wa wanawake katika maendeleo ya Taifa letu na kamwe hatutasita kuchukua hatua za kibajeti ambazo zinawawezesha wanawake kutekeleza majukumu yao katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna suala la mizigo kupungua katika Bandari za Dar es Salaam kutokana na wafanyabiashara kulalamikia VAT pamoja na Single Customs Territory kwa mizigo ya Congo. Ni kweli katika siku za karibuni tumeangalia mizigo inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam kati ya mwezi Disemba mwaka jana na mpaka Machi mwaka huu kuna upungufu ukilinganisha na kipindi kama hicho katika mwaka uliopita. Kwa mfano, makontena ya kwenda Congo yamepungua kutoka 5,529 mpaka 4,092 ambapo ni upungufu wa 26%. Pia yale yanayokwenda Malawi nayo yamepungua kutoka 337 mpaka 265 na yale yanayokwenda Zambia nayo yalipungua kutoka 6,859 hadi 4,448. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ushuru wa forodha kwa miezi hiyo hiyo, ukusanyaji umeendelea kuwa juu ya malengo. Ukiangalia takwimu hizi tunazosema ni kwamba idadi ya makontena katika kipindi hichohicho imepungua hata kwa nchi ambazo hazimo kwenye mfumo wa Single Customs Territory. Kwa hiyo, nachosema ni kwamba hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya upungufu wa mizigo inayokwenda nchi jirani ikiwemo Kongo na huu mfumo wa Single Customs Territory. Nasema hivi kwa sababu, kwanza kwa upande wa kodi ya VAT hatutozi kodi kwenye transit cargo pamoja na kuwa Sheria ya VAT inatozwa kwa huduma ndogondogo peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili bado Serikali inalifanyia kazi kwa sababu taarifa za kiuchumi za hivi karibuni…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, sekunde tano, muda umeisha.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ikiwa ni pamoja na World Economic Outlook ya 2016, ukuaji wa uchumi wa China umeporomoka kwa miaka ya karibuni na umegusa biashara katika nchi nyingi ulimwenguni ikiwemo Tanzania. Kwa hiyo, sasa hivi tumeshawaagiza TPA na TRA kufanya uchambuzi wa kina kuona mwenendo huu wa mizigo katika bandari ya nchi jirani ikiwemo pia Dar es Salaam ili tuweze kuona ni nini kinaendelea. Taarifa ya jana…
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa.
WAZIRI WA FEDHA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.