Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe shukrani za dhati kwa Bunge lako kujadili hoja hii kwa huo muda wa siku tatu. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote mliochangia Wizara hii. Wabunge wapatao 193, zaidi ya nusu ya Wabunge waliopo hapa wamechangia kwa kuandika na wengine wameongea hapa. Walioweza kuchangia kwa maandishi wako Wabunge 102 na walioweza kuongea hapa ni Wabunge 91. Nawashukuru sana. Ushauri wenu wote mlioutoa, Wizara yangu itauzingatia katika utekelezaji. Naomba niwahakikishie, haya maandishi na majibu tutayatoa kabla ya mwisho wa Bunge hili. Kwa hiyo, kila mmoja atakwenda Jimboni kwake akiwa na majibu ya hoja zake alizokuwa amezitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumza habari ya kugawana maji yaliyopo. Kama nilivyosema kwenye hotuba yangu, rasilimali za maji tulizonazo nchini ni kilometa za ujazo
96.27 ambapo tukigawana sisi kwa population ya nchi kila mmoja anaweza akatumia maji ya ujazo 1,800, lakini tumefanya utafiti na kufuatilia, maji haya tunategemea zaidi mvua. Hali ya tabianchi kama mnavyoona imekuwa inapungua mwaka hadi mwaka, kwa hiyo, hata rasilimali za maji zinapungua. Sasa sisi kama Serikali ni lazima tuwe na mikakati ya kuhakikisha tunaongeza rasilimali za maji nchini kulingana na mahitaji ili tuweze kuwagawia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tuchukue hatua mbalimbali. Pamoja na hatua hizo tunazozichukua, Serikali ina mpango maalum wa kutunza vyanzo vya maji; kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kuhakikisha vyanzo vinabainishwa, vinawekewa mipaka; tunatengeneza ramani pamoja na kuandaa taratibu za fidia kwa sababu baadhi ya watu tutawaondoa maeneo yale ambayo yana vyanzo vya maji na maeneo oevu. Hili naomba sana Waheshimiwa Wabunge tukubaliane kwamba lazima tuchukue hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kuwa na mipango hii, tunaomba tutoe wito kwa Watanzania wote, tusiendelee kulia kwamba maji hakuna na tuna miradi mingi ambayo imejengwa kwa fedha nyingi za Serikali, leo haifanyi kazi. Haifanyi kazi kwa sababu vyanzo vile vilivyoainishwa, leo havitoi maji. Kwa hiyo, sasa ni lazima sisi tuchukue hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetembelea Mkoa mmoja, naweza nikasema Mkoa wa Rukwa nikakuta kuna chanzo ambacho kilikuwa kinatoa maji kwa vijiji kama vinne, lakini chanzo kile kwa sababu watu wamekivamia, ndiyo eneo wameweka la ufugaji ng’ombe, kwa hiyo, maji hakuna. Leo hawapati maji! Inabidi tuanze kutafuta tena njia nyingine ambazo ni gharama zaidi kwa Taifa ili kuwapelekea wananchi wale maji wakati maji yalikuwepo. Kwa hiyo, ni lazima tuchukue hatua kwamba wananchi washiriki katika kutunza na kulinda vyanzo vya maji lakini pia tutoe elimu ya kutosha, wananchi waache kulima na kufuga katika maeneo ndani ya mita 60 ambayo tumeainisha ndiyo vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwahamasisha wananchi kutumia teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua, hiyo itaongeza rasilimali ya maji kama mlivyochangia Wabunge wengi. Tumekuwa tunapata mvua, lakini maji yote yanakwenda baharini. Sasa tunaanza kuchukua hatua kwa mtu mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia na kwenye Taasisi zetu, kwenye shule, zahanati; hakuna sababu ya kuwa huna maji ya kuwahudumia wagonjwa wakati tunaweza tukavuna maji ya mvua kwenye paa la zahanati. Tumetoa mwongozo kwa Halmashauri zetu zote nchini sasa tuanze kuchukua hatua. Ikibidi tutunge Sheria ndogo ndogo za kudhibiti watu ambao hawatataka kufanya suala hili la uvunaji wa maji ya mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua za muda mrefu Serikali imepanga kujenga mabwawa ya kimkakati, likiwepo Bwawa la Farkwa, Ndembela na Kidunda ili kuweza kuongeza rasilimali za maji. Pia tumetoa mwongozo kwa Halmashauri zetu kwamba tuwe na mkakati kwa kutumia mapato ya ndani tujiwekee ratiba wa kujenga bwawa moja kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki ni kitu kinachowezekana kwa mabwawa madogo madogo; tutaondoa tatizo la wafugaji wetu kuwa wanazunguka nchi nzima tatizo kubwa wanatafuta maji kwa ajili ya mifugo. Tukiwajengea mabwawa kwenye maeneo yao, migogoro ya wafugaji na wakulima itapungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wabunge wengi wamezungumza habari ya mifumo endelevu ya kuweza kuendesha miradi yetu ya maji katika maeneo ya vijijini. Wizara inaendelea na uandaaji wa mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji kwa kutumia ofisi zetu za mabonde kama ya Rufiji, Ziwa Rukwa, Ruvuma na Pwani ya Kusini; Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika na bonde la kati. Sasa hivi tunaandaa taratibu za manunuzi kwa ajili ya kuweza kuajiri wataalam watakaosaidia mabonde haya katika suala hili la mifumo endelevu ya kusimamia rasilimali za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto za uendelevu za huduma ya maji, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri inaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na upatikanaji wa takwimu. Sasa hivi tunazungumza habari ya wastani wa upatikanaji wa maji 72.15%, lakini Kambi ya Upinzani wao badala ya kusikiliza takwimu za Serikali wanakwenda TWAWEZA. Sasa unamwamini TWAWEZA kuliko Serikali!

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, Waheshimiwa Wabunge, takwimu za upatikanaji wa maji zinaendana na uwingi wa watu wanaopata maji, siyo kwa wingi wa vijiji. Maana mtu anasema nina vijiji 100; vinavyopata maji viko 30. Kwa hiyo, anasema wastani ni hivyo. Haiendani hivyo! Tunaangalia wingi wa watu wanaopata maji kulingana na Sera yetu ndani ya umbali wa mita 400.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila kituo cha kuchotea maji tumeweka wastani wa watu 250. Kwa hiyo, kwa namna hiyo ndiyo tumetengeza takwimu, lakini bado tunaweza tukaboresha zaidi suala hili la upatikanaji maji, lakini usitumie TWAWEZA, kwa sababu TWAWEZA anaweza akamwuliza mtu kwa kupiga simu. Huwezi kufanya utafiti kwa kupiga simu. Sisi tunazo data. Nakubali kweli kuna miradi mingi ambayo ilikuwa inafanya kazi, leo ina changamoto kwamba maji hayatoki, lakini ni jambo la kufanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye hotuba yangu, tumeshatoa mpango sasa wa kukarabati miradi yote ambayo haitoi maji. Payment by result, Serikali ya Uingereza imeweka fedha zaidi ya shilingi bilioni 200 na kitu kwa miaka mitatu kusaidia Halmashauri zetu kufufua miradi yote ambayo imekufa (ambayo haifanyi kazi). Kwa hiyo, mpango huu ni mzuri na nina hakika kwamba tukifufua miradi yote ya zamani tutakwenda vizuri na tutakwenda kweye data hizi ambazo tunazizungumza leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaahidi wananchi wetu kwamba ndani ya miaka mitano, ikifika mwaka 2020 Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha upatikanaji wa maji unafika asilimia 85 vijijiini na asilimia 95 mijini. Ndugu zangu huu ni mwaka wa kwanza wa Bajeti, ndiyo tumemaliza. Tunaandaa sasa mwaka wa pili. Kwa hiyo, hatuwezi kufikia asilimia 85 katika bajeti ya mwaka mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa kwanza tulipanga bajeti ya shilingi bilioni 915 kwenye maendeleo, lakini sasa kuna hatua mbili; kwanza unafanya manunuzi halafu unakwenda kwenye utekelezaji…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kumekuwa na hoja watu wanasema kwamba pesa zilizopangwa mwaka huu ni kidogo. Mimi nasema siyo suala la kusema kidogo, suala kubwa ni fedha kupatikana. Kwa hiyo, bajeti yetu ya mwaka huu ya shilingi bilioni 913, sisi kama Wizara tumeshafanya manunuzi. Fedha zilizotolewa zaidi ya shilingi bilioni 10 ambazo ni asilimia 19, ni zile ambazo tayari tumelipa certificates kwamba fedha hii
inakwenda kulipa kazi iliyofanyika. Fedha ambazo tayari tumeajiri Wakandarasi na tumeshasaini mikataba zaidi ya fedha hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi tunakwenda kwa utekelezaji wa hiyo shilingi bilioni 915 na Serikali kwa commitment hiyo ni kwamba mpaka ikifika Juni; kwa sababu hii status ilikuwa ni mwezi wa Tatu; kuna mwezi wa Nne, wa Tano na wa Sita. Kwa hiyo fedha itatolewa na Serikali kama ilivyokuwa imepanga. Kwa hiyo, hakuna haja ya kuwa na wasiwasi wa hii bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya hilo, kuna hizi dola milioni 500 za kutoka Serikali ya India. Katika utaratibu wa upangaji wa bajeti, wakati mnaandaa zile ceiling, mara nyingi huwezi ukaiweka kwenye vitabu vya Hazina fedha ambayo bado hujasaini ule mkataba wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ambayo naomba niitoe ambayo tayari Kamati ya Madeni na Mikopo imeshaidhinisha fedha hii, kwa hiyo, fedha hii itakuja kupatikana katika mwaka wa fedha huu wa 2017/2018. Kwa hiyo, fedha ya Bajeti ya Wizara ya Maji itaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kikubwa ambacho naomba na ambacho ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge nimeona, kwa kweli kila mmoja amekuwa analia na Jimbo lake. Naomba sana, tatizo kubwa tulilokuwa nalo ni utekelezaji ndani ya Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepeleka fedha za Mfuko wa Maji katika Halmashauri mbalimbali lakini mpaka leo kuna Halmashauri fedha zipo lakini hakuna walichokifanya. Sasa ndiyo maana tunafikiria kwamba ili tuweze kujenga miradi hii ya maji, lazima tuanzishe Mfumo wa Wakala wa Maji Vijijini ili tuwe na standard inayofanana katika utekelezaji. Kwa sababu mpaka leo yuko Mkurugenzi hajafanya manunuzi, anasubiri apelekewe fedha na tumetoa mwongozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, tumewapa nakala za mwongozo kwamba hatutapeleka fedha, bajeti yetu ni cash budget. Tunapeleka fedha mahali ambapo kuna utekelezaji na ndiyo maana kumekuwa na hata uwiano wa mgao. Tumepeleka fedha, unaweza ukakuta mahali pengine zimekwenda fedha nyingi kwa sababu wana mradi, lakini sehemu nyingine utapeleka fedha nyingi mradi hawana, hawataki kubadilika wanataka kufanya kazi kimazoea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Waheshimiwa Wabunge, tusaidiane katika kusimamia Halmashauri zetu ili tuendane na kasi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Ningeweza kusema maji hoyee, lakini ndiyo hali halisi kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kabisa kuondoa tatizo hili la maji kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Mkutano wa Kimataifa ambayo tunasema lengo la sita la maendeleo endelevu wanataka kwamba tukifika mwaka 2030 tuhakikishe wananchi wetu wanaoishi vijijini na wanaokaa mijini wanapata maji kwa asilimia 100. Nataka niwahakikishie Bunge hili kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano itahakikisha tunafikisha lengo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imetolewa hoja ya kuboresha Mfuko wa Maji na hoja hii imetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Maji na Mifugo. Ni hoja nzuri na ilishatolewa hata kipindi kilichotangulia, lakini kulingana na Kanuni zetu, hatuwezi tukaamua humu ndani. Tutaipeleka kwenye Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kile kipindi cha siku saba, tutafanya mashauriano na kuona namna gani pendekezo la Wabunge la Kamati ya Bunge pamoja na Wabunge wengi wameunga mkono. Tutaona namna gani jambo hili linaweza kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la mchango wa Mheshimiwa Kitwanga. Amechangia hapa kwa hisia kubwa kuonesha kama Serikali ya Chama cha Mapinduzi haijafanya chochote kwa Wilaya ya Misungwi. Sasa nataka nimwulize Mheshimiwa Kitwanga kama yupo, labda yale maneno anasema ni ya kwake au ya wananchi; kwa sababu wananchi nitawaambia nini kimefanyika Misungwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tumesaini mikataba, Mkurugenzi wake na Mwenyekiti wa Halmashauri alikuwepo, tunasaini mikataba hadharani ya kupeleka maji ya Ziwa Victoria Wilaya ya Misungwi, kwa fedha nyingi, zaidi ya shilingi bilioni 38.5, zinakwenda Misungwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Mbunge anaposema anakwenda kuhamasisha wananchi wakabomoe huo mtambo wa Ihelele, maana yake analeta uasi au anataka asithamini kazi iliyofanywa na chama chake? Basi ajitoe kwenye chama! Eeh!

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Serikali imepeleka fedha, sasa leo maendeleo ambayo yameshafanyika ni lazima tuwahamasishe wananchi wetu. Kitu cha kwanza tuwahamasishe wananchi wetu kutunza miundombinu ambayo tayari tumeshafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani ukasema miundombinu ambayo tumefanikiwa tukabomoe. Ukichukulia umeme kwa mfano, unatoka kijiji kimoja unaruka vitatu unakwenda cha nne, sijasikia mahali wanang’oa nguzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimwambie Serikali inaendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwepo Misungwi na Usagara. Kwa upande wa Usagara, watapata maji yatakayosukumwa kutoka eneo la Nyashishi hadi kilima cha Usagara ambapo watazalisha maji kiasi cha lita milioni tatu. Hadi sasa usanifu wa awali unaojumuisha Buswelu umefanyika. Kwa hiyo, kazi hii itafanywa kwenye mwaka huu wa fedha, tumeshaweka fedha. Sasa akisema haungi mkono maana yake hii fedha shilingi bilioni 4.46 tupeleke Wilaya nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mji wa Misungwi, Wizara yangu kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza tayari imesaini mkataba na mkandarasi wenye thamani hiyo ya shilingi bilioni 38 kwa ajili ya kupeleka maji katika Mji wake wa Misungwi. Tumepata ufadhili kutoka Benki ya Maendeleo ya Ulaya pamoja na Shirika la Maendeleo Ufaransa. Sasa leo ukisikia mtu wa Misungwi anasema kwamba kwa kweli haithamini kazi ya Serikali ni kitu kinachosikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Halmashauri ya Misungwi, awamu ya kwanza ya mradi Serikali itajenga miundombinu ya maji kutoka Kijiji cha Mbarika kwenda Misasi kupitia Vijiji vya Lutaletale, Bugisha, Naya, Ikula, Sumbungu, Makale, Kasororo, Misha na Nabwawa. Kwa hiyo, miundombinu hii tayari imekamilika kwa fedha ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Vilevile zaidi ya shilingi bilioni
3.5 imepangwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mingine katika Wilaya ya Misungwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kwa hisia sana kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo yao. Naomba Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla wao waunge mkono juhudi za Serikali katika kutatua changamoto za upatikanaji wa maji nchini. Katika maeneo mengi nchini, miradi ya maji na umwagiliaji imeendelea kutekelezwa na ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji kama ilivyoelezwa katika hotuba yangu. Miundombinu iliyokamilika kujengwa ni mojawapo ya mafanikio ya Serikali na inabidi tushirikiane kuhakikisha inatunzwa ili wananchi waendelee kupata huduma inayokusudiwa na kwa ubora unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema sikutarajia sana kauli hii itoke kwa Mheshimiwa Kitwanga, mtu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya mgawanyo wa fedha usiokuwa na uwiano sawa kwenye Halmashauri. Kama nilivyoeleza hapo mwanzo, ni kweli hatujagawa sawasawa kwa sababu ya kasi ya utekelezaji kutofautiana. Kwa hiyo, suala hili tunalifanyia kazi lakini tumetembelea kila Halmashauri na kuwaelekeza mahali ambapo kuna matatizo ya wataalam tunatumia Mamlaka za Mikoa au Kanda kusaidia kuwaelekeza namna ya kufanya manunuzi na kuweza kusimamia miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo kuhusu fedha za USD milioni 503. Kama nilivyosema, wakati tunafanya ceiling fedha hii tunaitarajia kwamba itasainiwa kabla ya mwisho wa mwaka huu. Kwa hiyo, bajeti yetu ya maji itaruka toka shilingi bilioni 600 na itakwenda zaidi ya shilingi trilioni 1. Kwa sababu hii fedha ya USD milioni 503 tayari imeshaidhinishwa na Kamati ya Madeni na Mikopo. Tunatarajia mkataba utasainiwa kabla ya Juni kwa sababu Kamati ya Mikopo imeshaidhinisha na itakuja kuonekana kwenye bajeti ya 2017/2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, nielezee hoja moja ya Kambi ya Upinzani kuhusu tenda ya miradi ya Ziwa Victoria kwenda Tabora na Nzega. Mwasilishaji wa hoja hii ya Kambi ya Upinzani anasema kulikuwa na harufu ya rushwa. Nataka kwanza nimhakikishie harufu ya rushwa labda iko upande wake kwa sababu katika taratibu za manunuzi za tenda wakati mkiwa kwenye mchakato kuna stage fulani mkifika mnataka sasa kupata aliyeshinda huwa kunatolewa muda wa kutosha kwamba kuna mtu mwenye malalamiko anatakiwa apelekwe kwenye mamlaka za PPRA na PPA. Waziri wa Maji hawezi kuingilia kwenye mchakato ya tenda, hii hairuhusiwi na pia hairuhusiwi kwenda kwenye magazeti. Mchakato huu uliandikwa hata kwenye magazeti mtu analalamika anakwenda kwenye magazeti, sasa leo wanawatumia Wabunge kulalamika, hiki kitu hakikubaliki. Ni lazima twende kwenye kanuni na taratibu za manunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, manunuzi yamekwenda vizuri na tumepata wakandarasi wazuri na kila hatua tulioifanya tunawasiliana na mwenye fedha Exim Bank. Kama kuna kampuni imeonekana imetumia rushwa kule India haruhusiwi kupata kazi ile, kwa hiyo sisi tunapeleka kwake. Kama kungekuwa kuna jambo ambalo halikubaliki na Serikali ya India wangesema, Serikali ya India wametoa No Objection kwamba endeleeni. Sasa ndugu yangu wa Kambi ya Upinzani yeye hili analitoa wapi? Sasa mkandarasi ameshapatikana, tayari tumeshasaini mkataba na anakwenda kuanza kufanya kazi. Namshauri aunge mkono fedha zile zifanye kazi ili kuleta maendeleo kwa wananchi waliokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nielezee kidogo kuhusu masuala ya azma ya Serikali kuboresha huduma ya maji safi kwa Jiji la Dar es Salaam. Kama tulivyosema tumeshaongeza uzalishaji kutoka lita milioni 300 kwa siku sasa tumefikia lita milioni 504 kwa siku. Mheshimiwa Mnyika maeneo mengi aliyosema ya mabomba ya Mchina leo yana maji. Ninayo taarifa ya leo kwamba maji yanatoka. Tatizo lililopo mabomba ya Mchina yamekaa muda mrefu hayakuwa na maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna watu sehemu zingine waliamua kutoboa na tatizo tulilonalo sasa ni umwagikaji ovyo wa maji katika mabomba haya lakini kazi hiyo ndiyo tunayoishughulikia ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu katika maeneo yale ambayo hayakuwa na mtandao. Kuna mkandarasi ameshaanza kufanya kazi Changanyikeni kwenda mpaka Bagamoyo kuongeza mtandao. Pia tumepata fedha kutoka Benki ya Dunia nao watajenga mtandao maeneo mengine. Kwa hiyo, tunaendelea kutafuta fedha na kwenye bajeti hii tumeweka fedha za kujenga mitandao katika maeneo yale ambayo hayana mtandao. Kwa hiyo, maji yapo mengi na ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika maji yanayotokana na visima vya Kimbiji na Mpera tunategemea kupata lita milioni 260. Katika mwaka huu wa fedha tunategemea tujenge sasa mtandao wa bomba la kuleta maji maeneo ya Kigamboni na maeneo mengine yote ambayo hayana maji kwa upande ule. Kwa hiyo, Serikali inafanyia kazi suala hili na hayo matatizo madogo madogo ya kuvuja na kadhalika ndiyo kazi inabidi tuifanye. Ndiyo maana sasa hivi tunataka tuimarishe sana Shirika la DAWASCO kwa ajili ya kupeleka maji kwa wananchi. Kwa sababu DAWASCO kwa utaratibu uliokuwepo anakwenda kushughulikia kuwasha mitambo sisi hatutaki afanye kazi hiyo. Tunataka tufanye maboresho, yeye ashughulike na wateja moja kwa moja, aende kwa Mheshimiwa Mnyika ili tupeleke maji haya kwa wateja wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa, wananchi waliounganishiwa maji kwa Dar es Salaam hawazidi 300,000 tunataka sasa wafike 1,000,000 ili waweze kuchangia gharama za uendeshaji. Nimeshawaambia hiyo ndiyo kazi ya kufanya tupate wananchi wengi waliounganishwa na maji safi. Pia tuna miradi ya majitaka, mfumo wa majitaka kwa Dar es Salaam kwa muda mrefu ulishakuwa hakuna na wananchi chini ya asilimia 20 ndiyo ambao wameunganishwa na maji taka. Tumepata fedha toka Korea Kusini pamoja na Benki ya Dunia tunakwenda kujenga mitambo ya kisasa ya kusafisha maji taka kwa ajili ya Jiji letu la Dar es Salaam. Kwa hiyo, ndugu zangu tumeahidi na tunatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimwambie Mheshimiwa Mnyika na Wabunge wengine wa Dar es Salaam maeneo ambayo sasa maji yanapatika. Ukichukulia kwa mfano Temeke, maeneo ya Kurasini Beach, Baraza la Maaskofu, Mtoni, Sabasaba, Mtoni kwa Kabuma, Temeke Wiles, Temeke Quarter, Temeke Sokota, Temeke Veterinary, Temeke Sandali, Temeke Mwembe Yanga, St. Mary’s Mbagala, VETA na Rangi Tatu. Haya maeneo yalikuwa hayana maji lakini sasa yana maji. Ukija kwa Kimara, Stop Over kwa Koleza, Kimara Bakery, Kimara Polisi, Michungwani, Mbezi Igubilo, Kimara, TANESCO, Kimara B Bonyokwa, leo maeneo haya yanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija sehemu za Ilala, maeneo ya Buguruni Mnyamani, Buguruni Sokoni, Buguruni Rosana, Buguruni Y2K, Sharifu Shamba Bondeni, Kipata Kariakoo, Uhuru kuanzia round about to Lumumba, Illala Bungoni, Mtaa wa Mafuriko, Amani Kariakoo leo wanapata maji maeneo yote yalikuwa hayana maji. Ni kazi kubwa inafanyika ndugu yangu Mheshimiwa Mnyika. Eneo la Tabata Mbuyuni, Ogongombelwa, Kilumi Chang’ombe, Banebane, Vigunguti Darajani, Segerea, Tutundu, Makaburi Mwasaka, Vigunguti, Kwamnyamani, Maji Chumvi Kasukuru, Msamvu Street, Kibangu Ubungo, Segerea kwa Bibi, Kisukuru Chumba Kimoja na Kibangu Unovo leo wanapata maji. Kwa hiyo, kazi kubwa tumeshafanya kwa kuboresha huduma ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam. Ni lazima tuthamini kazi ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa msukumo mkubwa anaoutoa kuondoa kero hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema maeneo yale mengine ya pembezoni haya sasa tunaendelea na utaratibu wa kuongeza mtandao. Naamini tutafanikisha kwa sababu maji yapo. Tuna tatizo la upotevu wa maji na ndiyo maana tunasema DAWASCO sasa tunataka a-concentrate na distribution pamoja na kudhibiti upotevu wa maji, tuachane naye na kwenda kuwasha mitambo kila siku kule Ruvu Chini, Ruvu Juu kazi hiyo itafanywa na watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna muda basi nafikiri naweza nikaongezea baadhi ya hoja, kuna Mradi wa maji Kishapu. Hii ilikuwa hoja ya Kamati ya Bunge, kazi ya usanifu wa miundombinu ya kusambaza maji katika Mji wa Kishapu imekamilika na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, yamezungumziwa mambo mengi lakini kama nilivyosema tutajibu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, habari ya umwagiliaji Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea kwa kirefu sana. Miradi hii ilikuwa inashughulikiwa katika Programu ya Maendeleo ya Kilimo. Sasa sisi Wizara ya Maji kazi yetu kubwa ni kushughulika na ujenzi wa miundombinu na miundombinu mingi iliyokuwa imejengwa ni kweli tumekuta ipo hovyo. Awamu hii inabidi tuanze pale walipoanzia wenzetu tuweze kurekebisha na tumeanza kuainisha maeneo ambayo yanatakiwa yarekebishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimepitia miradi mingi na Naibu Waziri amepitia miradi mingi. Kazi yetu mwaka huu wa fedha wa bajeti tulisema tuirekebishe miradi ile ambayo iko tayari inafanya kazi kabla ya kujenga miradi mipya lakini pia kufanya usanifu wa miradi mipya ambayo inaendana na ujenzi wa mabwawa. Hii ni kazi ambayo tutaendelea nayo katika bajeti hii na tumeweka maeneo mengi kwenye bajeti ukisoma hotuba utaona maeneo mengi tumeelezea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa ufupi ni kwamba hapa kwenye umwagiliaji tunahitaji uwekezaji zaidi kama Taifa. Mwaka wa kwanza hatukuweza kuweka uwekezaji wa kutosha, mwaka wa pili hatujaweza kuweka pia uwekezaji wa kutosha lakini nina imani mwaka utakaofuata tutaweka uwekezaji wa kutosha wa kujenga miundombinu ili tujiondoe kwenye tabu hii ya kuwa na njaa kila mwaka. Najua katika hizi hekta milioni 29 ambazo zinafaa kwa umwagiliaji tukiziendeleza hatutakuwa na tatizo la chakula. Pia tutaelekeza na aina ya mazao ya kulima ili kusudi kwa sababu wengi wanafikiri kuondoa njaa ni kulima mahindi tu na mpunga.
Lakini tunaweza kulima mahindi tukamwagilia. Kwa hiyo, nadhani sasa kama Taifa tuweke rasilimali na wanaoweza kuweka rasilimali ni Wabunge mnaoidhinisha bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza kwa kirefu sana masuala ya umwagiliaji. Nami nakubaliana naye kabisa na namuunga mkono amesema vizuri sisi Wabunge ndiyo tunaopanga bajeti sasa tuwekeze zaidi kwenye umwagiliaji kwa ajili ya kujiondoa katika tatizo la chakula maana ndiyo kitu cha msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nihitimishe kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa maoni yenu na mapendekezo mliyotoa. Niwahakikishie msiwe na wasiwasi, Wizara ya Maji ina bajeti ya kutosha ya kutekeleza miradi tuliyopanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, naomba sasa nitoe hoja kwamba Bunge lako liingie kwenye Kamati ya Matumizi na kuweza kuidhinisha bajeti hii ili twende kutekeleza tuliyojipangia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Watanzania wetu wanapata maji safi na salama na pia wanaendeleza kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.