Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002, nchi yetu ina eneo la hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mkoa wa Songwe una vyanzo vingi vya maji ambavyo vingeweza kutumika vizuri, vingeweza kusaidia huduma ya maji pamoja na kilimo cha umwagiliaji ambacho kinaweza kulisha nchi nzima. Ushauri wangu kwa Serikali, Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Kilimo vikae pamoja na kuona ni namna gani wanaweza kutumia vyanzo vya maji ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji kwa mkoa mpya wa Songwe

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango shirikishi wa maji shirikishi katika Mto Momba na Songwe unaweza kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na kutoa ajira kwa makundi ya vijana na akina mama ambao wengi wanategemea kilimo. Wizara ishirikiane na sekta binafsi kukamilisha miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uharibifu wa miundombinu ya maji na umwagiliaji; kumekuwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya maji hasa maeneo ya vijijini. Mfano, maeneo mengi ambayo yamewekwa mabomba ya maji ya kuchota kwa ujumla, wananchi wamekuwa wakiharibu mabomba hayo kwa kuwa hawana uchungu na miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri uwekwe utaratibu wa kuchangia miundombinu ya maji ili wananchi watambue thamani ya miundombinu ya maji na kuithamini. Hii itasaidia ukarabati wa miundombinu hiyo bila kutegemea ufadhili pindi miundombinu hiyo ikiharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo kubwa la upotevu wa maji hasa kwenye mashamba makubwa ya mpunga na mfano mzuri ni Bonde la Usangu - Mbarali. Miundombinu ya umwagiliaji ni ya zamani tangu kukiwa na mashamba machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua za haraka zisipochukuliwa kudhibiti kilimo holela cha umwagiliaji katika Bonde la Usangu kuna uwezekano mkubwa wa uzalishaji wa nishati ya umeme katika Bwawa la Mtera na Kidatu ukapotea kwa kiwango kikubwa kutokana na upotevu wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia haki za binadamu ziheshimiwe, mfano; haki ya kupata elimu, afya, maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa maji safi na salama vijijini bado ni changamoto kutokana na wananchi wengi kupata maji yasiyo salama. Uharibifu wa mazingira ni hatari sana kwa maisha ya binadamu kwa asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania wanatumia misitu kama malighafi kwa shughuli za uzalishaji na huduma pamoja na kuwa ni fursa ya ajira kwa watu wengi. Uharibifu wa mazingira ni chanzo cha mafuriko na ukame wa kutisha

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Wizara ya Mazingira na Wizara ya Kilimo kuhakikisha utoaji wa elimu juu ya utunzaji wa mazingira unapewa kipaumbele na ikiwezekana kuwepo na faini zinazotozwa kwa watumiaji wabaya wa maji na vyanzo vyake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa maji ni afya, uhai na maendeleo, ninashauri Wizara ya Maji kwa kushirikina na Wizara zote ihakikishe kuwa majengo yote ya taasisi mbalimbali yawe na michoro itakayoonesha utunzaji wa maji ya mvua ili kusaidia wakati ambao kuna upungufu wa maji. Mfano katika shule, hospitali, ofisi, hoteli na shughuli zote za kilimo cha umwagiliaji kuwekewa mifumo ya kutumia maji kidogo na kuzuia upotevu wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kushauri Wizara iendelee kutembelea na kutoa elimu kwenye maeneo yenye vyanzo vya maji hasa kusisitiza suala la mita 60 kutoka vyanzo vya maji. Kuendelea kutumia mila na desturi zinazosaidia utunzaji wa maeneo yenye vyanzo vya maji.