Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika aya ya 21 ukurasa wa tisa na 10 ya hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, imeelezwa kwamba hali ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam imeimarika baada ya kukamilika kwa maboresho ya mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini. Hata hivyo, Wizara izingatie kuwa hali haijaimarika katika maeneo yanayohudumiwa na Ruvu Juu kwa upande wa Jimbo la Kibamba katika kata za Kwembe, Mbezi, Msigani, Saranga na Kibamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema kufanya ziara ya haraka ya kikazi yenye kumhusisha Waziri wa Maji, Mbunge, DAWASA na DAWASCO ili kukagua maeneo yote ya mabomba ya Mchina ambayo nilipowasilisha hoja binafsi tarehe 4 Februari, 2013 Bungeni Serikali iliahidi kwamba baada ya kukamilika kwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu na ujenzi wa bomba maji yangekuwa yanatoka. Aidha, kwa upande wa maeneo katika kata hizo za Kibamba, Kwembe, Mbezi, Msigani na Sarange ambayo hayana mtandao wa usambazaji wa maji, kasi ya kuwaunganishia wananchi ni ndogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba katika aya ya 135 ukurasa wa 72 na 73, Wizara imetaja maeneo ya Mbezi hadi Kiluvya na maeneo ya Kibamba, Msakuzi, Makabe, Malamba Mawili na Msigani. Upanuzi wa mfumo wa kusambaza maji katika maeneo hayo unasuasua, kadhalika yapo maeneo mengine katika kata hizo hayajatajwa katika orodha hiyo. Hivyo naomba Wizara inipatie orodha ya maeneo yote ambayo hayana mfumo wa kusambaza maji safi katika kata hizo tano na ratiba yenye kuonyesha ni lini maeneo hayo yatasambaziwa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Ruvu Chini ieleweke kwamba katika Jimbo la Kibamba kata pekee inayopata maji kutoka chanzo hiki ni kata ya Goba, katika aya ya 135 ukurasa wa 73 yanatajwa maeneo ya Kinzudi, Matosa na Mtaa wa Goba. Hata hivyo mtandao wa mabomba ya maji katika maeneo hayo haulingani kabisa na mahitaji. Aidha, ipo mitaa mingine katika kata ya Goba ambayo haipo katika orodha ya kusambaziwa maji katika mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba kupewa orodha ya maeneo yote ya kata ya Goba yasiyokuwa na mtandao wa mabomba ya maji yenye kuonyesha ratiba ya lini yatawekewa mabomba ya maji. Naomba Wizara inaposhughulikia miradi ya maji ya Ruvu Chini kwa upande wa DAWASA na DAWASCO itoe kipaumbele maalum kwa kata ya Goba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika aya ya 133 ukurasa 71, Serikali imeeleza kwamba inaendelea kutekeleza mradi wa Bwawa la Kidunda unaogharimu dola za Marekani milioni 215. Hata hivyo, kimsingi hakuna utekelezaji unaoendelea kwa kuwa pamoja na usanifu kukamilika muda mrefu, mpaka sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha. Mradi huu ni wa kutoka wakati wa Mwalimu Nyerere mwaka 1980 na sasa ni wa dharura kutokana na mabadiliko ya tabianchi.