Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Nianze kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa bajeti yenye matumaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mafia ni kisiwa na kutokana na jiografia yake hiyo hakuna mito yenye kutiririka mwaka mzima. Ukweli kuwa chanzo kikuu cha maji kisiwani Mafia ni uchimbaji wa visima virefu na vifupi. Kwa masikitiko makubwa miradi ya maji iliyoletwa Kisiwani Mafia ni michache sana hivyo kisiwa cha Mafia kina shida kubwa ya maji. Kupitia Bunge lako Tukufu kwa namna ya kipekee, tunaiomba Serikali ituongezee miradi ya maji kutokana na mazingira magumu ya upatikanaji wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa kuvusha maji kutoka Kisiwa Kikuu cha Mafia eneo la Kiegeani kwenda Kisiwa kidogo cha Jibondo takriban kilometa tisa umekuwa kwenye hatua mbalimbali za michakato kwa takribani miaka mitano sasa. Kupitia Bunge lako hili Tukufu tunaomba Serikali iharakishe mchakato huu kwani Kisiwa cha Jibondo kwa asili na ardhi yake ni mawe matupu na hakuna namna yoyote hivyo kulazimisha kuchimbwa kisima kilometa tisa nje ya Kisiwa Kikuu cha Mafia na kupitisha mabomba chini ya maji mpaka Kisiwa cha Jibondo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kwa kuwa mradi huo haupo wananchi wanalazimika kukodi mashua za uvuvi kuja Kisiwa Kikuu na madumu ya maji na kuchota maji na kuvuka nayo. Nyakati za pepo kali za kusi na kaskazi zoezi hili linakuwa gumu na wananchi wanatumia maji ya chumvi ambayo ni hatari kwa usalama wao. Hivyo, tunaiomba Serikali kuharakisha mradi huu ili kuondoa adha hii kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.