Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri ambayo naiunga mkono, naomba kuchangia maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Mbozi kuna Mamlaka ya Maji ya Mji wa Vwawa na Mamlaka ya Maji ya Mji Mdogo wa Mlowo. Wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, aliahidi kuunganisha mamlaka hizi mbili na kuunda mamlaka kubwa itakayoshughulikia kutafuta, kusambaza na kusimamia maji katika miji hiyo ambayo ni sehemu ya Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe. Ni lini Wizara itaanza kutekeleza ahadi hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa maji safi na salama katika Mji wa Vwawa. Hivi sasa hakuna maji kabisa Mji wa Vwawa na yaliyopo ni machafu sana kwa sababu hayachujwi kabisa, yanasambazwa kama yalivyo. Bajeti iliyotengwa ni ndogo sana. Naomba Serikali ifanye kila linalowezekana kutuongezea bajeti ya kurekebisha miundombinu ya maji pale Vwawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi ulioandaliwa miaka mingi iliyopita uliotegemewa kusambaza maji katika Vijiji vya Iyula, Idiwili, Ipyana, Idunda, Igale, Luanda, Senjere na Lumbila. Serikali ina mpango gani wa kutekeleza mradi huu?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Lukuhe – Mlangali ambao ungesambazwa vijiji 14 katika Wilaya, baadhi ya fedha ziliwahi kutolewa na zikatumika vibaya. Naomba kupata maelezo ya kina juu ya hatma ya mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Vijiji vya Ihanda na Ipunga pamoja na kata zake, Serikali ilitoa zaidi ya Sh.320,000,000/=, mradi uliokuwa unafadhiliwa na Benki ya Dunia. Fedha hizo hazijulikani zilipo na mpaka leo hakuna maji katika Kata za Ihanda na Ipunga. Naomba tamko la Serikali juu ya mradi huu na hatua zilizochukuliwa dhidi ya fedha hizi. Naomba kupata majibu ili wananchi wa Jimbo la Vwawa na Mkoa wa Songwe waweze kuwa na imani na Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.