Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie changamoto zilizopo katika Mkoa wetu wa Iringa kama ifuatavyo:-

(i) Ukosefu wa fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa kwa baadhi ya miradi kama Tanangozi, Kidabaga, Malangali na Mbalamaziwa;

(ii) Ukosefu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mipya vijijini kama Mkonge – Igoda, Ukelemi na Uyela – Nyololo, Njiapanda na Makungu;

(iii) Uwezo mdogo wa wakandarasi na wataalam washauri kifedha na kitaalam katika kujenga na kusimamia mradi wa maji;

(iv) Ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya uchangiaji wa huduma ya maji na uendeshaji wa miradi ya maji vijijini; na

(v) Upungufu wa wataalam wenye sifa katika Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya LAAC
ilipotembelea katika Mkoa wetu wa Iringa ilibaini yafuatayo:-

(i) Miradi mingi ilikosewa wakati wa usanifu, hivyo, visima vingi kwa sasa havina maji na kama yapo basi sio ya kutosha;

(ii) Miradi mingine chanzo cha maji kimehama na hivyo kukosa maji katika chanzo;

(iii) Baadhi ya wakandarasi hawana uwezo wa kifedha na kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati; na

(iv) Ucheleweshwaji wa wakandarasi kupatiwa malipo wanapowasilisha certificates mpaka kupelekwa mahakamani kwa baadhi ya miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua tatizo linalosababisha Serikali kutotumia mito mingi tuliyonayo katika mkoa wetu kama Mto Ruaha, Mto Lukosi, Mto Mtitu katika kutatua tatizo kubwa la maji badala ya miradi ya visima inayotumia pesa nyingi na hakuna maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya umwagiliaji. Katika Mkoa wetu wa Iringa na hasa Jimbo la Iringa, ipo miradi miwili ya umwagiliaji ya Ruaha Irrigation Scheme, huu upo Kata ya Ruaha na Mkoga Irrigation Scheme, huu upo katika Kata ya Isakalilo. Miradi hii ni ya siku nyingi sana, Serikali haijaweza kuitengea pesa ili iweze kukamilika na kutoa ajira kwa wananchi. Nataka kujua vigezo vinavyotumika kupeleka hizi pesa za miradi ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, uvunaji wa maji. Ni lini Serikali itatoa elimu katika suala hili ili Halmashauri zetu ziweke utaratibu wa kuhakikisha maji yanavunwa wakati wa mvua nyingi ili kuwa na akiba ya maji wakati wa kiangazi? Hayo maji yangeweza kusaidia katika shughuli za kibinadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bustani za mboga (vinyungu). Mkoa wetu wa Iringa ni mkoa ambao wananchi wake wanafanya shughuli za kibiashara hasa za mbogamboga kutumia maeneo hayo nyevunyevu kujipatia kipato lakini Serikali imepiga marufuku. Sasa nini mpango
wa kuwasaidia hawa wananchi waliokuwa wanategemea kilimo hicho?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.