Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Mawaziri wote wawili kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya pamoja na matatizo ya upungufu wa fedha. Bajeti ya mwaka 2016/2017, fungu la maendeleo walitengewa Sh.915,193,937,771 lakini walipata Sh.181,209,813.609, sawa na asilimia 19.8. Mwaka huu 2017/2018 wametengewa Sh.623,606,748,000, pana tofauti ya Sh.291,587,189. Upungufu huu ni mkubwa na ningeshauri kiwango kikubwa kiongezwe kabla ya Juni katika kipindi hiki.

Sioni mantiki ya kuongeza fedha kwa tarakimu badala ya kupeleka fedha ambazo zimepitishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji Muheza bado ni kubwa sana. Ndoo moja ya maji ni Sh.800 hadi Sh.1,000/= mjini, bado huko vijijini. Ukombozi wa maji Muheza Mjini ni maji kutoka Mto Zigi kilometa 22.7. Mradi huu ni kati ya miradi 17 ya mkopo wa India (ukurasa wa 173) lakini kila siku tunaambiwa financial agreement bado. Tunaomba ishughulikiwe ili fedha hizo, dola milioni 14.754 zitolewe ili kazi ianze.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji kutoka Pongwe mpaka Mjini Muheza tenda zilikwishafunguliwa lakini bado wakandarasi hawajateuliwa. Tunaomba mradi huu unaoshughulikiwa na Tanga UWASA tupate majibu haraka ni nini kinachoendelea. Nawashukuru Mawaziri wote kwa ubunifu wa mradi huu na Tanga UWASA.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa maji Muheza pia miundombinu ni mibovu. Hivyo, miradi yote miwili ikikamilika bila kurekebisha miundombinu hiyo miradi hiyo itakuwa haijakamilika kikamilifu. Hivyo, nashukuru kwa kuwekewa shilingi bilioni tano kwa ajili ya mifumo ya maji mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji vijijini, nashukuru kwa kutengewa shilingi milioni 931.373 ingawaje zimepungua kutoka zile za mwaka 2016/2017. Ningeshukuru kama zingerudishwa ambazo ni Sh.222,105,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji ambavyo vinazunguka vyanzo vya maji vya Mto Zigi inabidi visaidiwe kupata maji safi na salama kwa kuwekewa mabomba na dawa kwenye maji yote yanayotiririka kutoka milimani, hususan Tarafa za Amani, Mbomole, Zirai, Kwezitu, Mbarai, Kisiwani, Moshewa, Kwemidimu na kadhalika. Wakisaidiwa naamini wataendelea kuvitunza vyanzo hivyo na kuwafanya wasichafue vyanzo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashauri yafuatayo:-

(i) Suala la maji litolewe kabisa TAMISEMI na lishughulikiwe moja kwa moja na Wizara kama umeme;

(ii) Tozo inayotozwa ya Sh.50 kwa ajili ya Mfuko wa Maji iongezwe na kuwa Sh.100, hii itasaidia kupunguza tatizo la maji hapa nchini; na

(iii) Ni muhimu tuanzishe Wakala wa Maji Vijijini kama REA, huenda ikasaidia kupunguza tatizo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.