Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kuhusu miradi ya maji mikubwa miwili; mradi wa Rukoma na mradi wa Kandaga. Miradi hii ilianza bajeti ya 2012/2013 hadi bajeti hii ya 2017/2018 haina mwelekeo wowote wa kukamilishwa. Tatizo la miradi hii ni mgawanyo wa Halmashauri ya Wilaya mbili yaani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Vijijini na kuzaliwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na miradi hii ikabaki Halmashauri mama ya Wilaya ya Kigoma Vijijini na miradi mingine mikubwa kama Uvinza, Nguruka, Ilagala na Kalya ilihamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na inaendelea vizuri.

Mhshimiwa Naibu Spika, niombe Wizara isiache kutupia macho miradi ya Kandaga na Rukoma ili Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Vijijini watumalizie na kutukabidhi kwenye Halmashauri ya Uvinza.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii minne inayotekelezwa na Halmashauri ya Uvinza kwa maana ya Mradi wa Nguruka, kiasi kilichobaki ni Sh.1,865,024,153; Mradi wa Ilagala kiasi kilichobaki ni Sh.491,628,240; Mradi wa Uvinza thamani ya pesa zilizobaki ili mradi ukamilike ni Sh.1,040,943,442 na Mradi wa Kalya kiasi kilichobaki ni Sh.185,170,935. Jumla tunahitaji Sh.3,582,766,770 ili tukamilishe miradi hii minne.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kitabu cha bajeti cha Mheshimiwa Waziri, bajeti ya miundombinu ya maji kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni Sh.1,723,135,000. Utaona ni kwa namna gani miradi hii iliyoanza tangu bajeti ya 2012/ 2013 haitakamilika na kusababisha wananchi wa maeneo husika kukosa maji safi na salama na ikizingatiwa kati ya vijiji 61 ni vijiji vitano tu ndivyo vinavyopata maji safi na salama tena ya visima vifupi. Tuombe Wizara ione namna ya kutuongezea fedha pale ambapo wakandarasi watakapokuwa wamelipwa hizi 1.7 bilioni na wakawa wameleta certificate zao kwa ajili ya malipo ili basi miradi hii iweze kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pia masikitiko yangu kwa Wizara ya Fedha na Mipango kupunguza bajeti ya maendeleo ya miradi ya maji kutoka shilingi bilioni 900 kwenye bajeti ya 2016/2017 hadi shilingi bilioni 600 kwa bajeti ya mwaka huu wa bajeti 2017/2018 unaoanza tarehe 1/07/ 2017. Inasikitisha sana tena sana na kwa mpango huu wa upunguzaji wa bajeti ya maendeleo ya miradi ya maji inaonesha jinsi gani Serikali haina dhamira ya dhati ya kumaliza miradi ya maji inayoendelea kwenye majimbo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza tunavyo visima virefu na vifupi kama cha Mganza, kisima cha Shule ya Msingi Mliyabibi, kisima cha Sanuka na maeneo mengine havijafanyiwa marekebisho kwa miaka mingi sana na kusababisha visima hivi kutotoa maji na badala yake wananchi wa maeneo haya wanabaki kuona visima ambavyo hawana faida navyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua bajeti ya mwaka 2017/2018 ni finyu ila tuombe Wizara iliangalie Jimbo la Kigoma Kusini kwa jicho la huruma kwani hali ya upatikanaji wa maji safi na salama ni mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kuzungumzia suala la umwagiliaji. Mheshimiwa Waziri anatambua fika Jimbo langu ndiko Mto Malagarasi ulipo na mto huu unapita takribani vijiji 22 na mradi wa maji safi na salama wa Mto Malagarasi unahusisha Miji ya Urambo, Kaliua na Nguruka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na uchambuzi yakinifu unaoendelea kwenye mradi huu mkubwa lakini pia tunalo Bonde la Mto Malagarasi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji hasa kilimo cha mpunga. Tumwombe Mheshimiwa Waziri pale panapokuwa na fursa ya kusaidia wakazi wa Tarafa hii ya Nguruka ili waweze kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na ukizingatia Tarafa hii inalima sana mpunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.