Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wa Maji na Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha Watanzania wanapata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai; bila maji hakuna maisha ya binadamu wala viumbe hai vingine. Tatizo la uhaba wa maji nchini na duniani linazidi kuongezeka. Hii kama wataalam wanavyosema, inaashiria, vita kubwa duniani itakayotokea itakuwa ni vita ya kuvigombea (scramble for) maji. Hivyo ni muhimu kwa nchi yetu, Serikali yetu kupanga vizuri juu ya mipango mizuri ya usambazaji maji kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe bado tuna vijiji vingi havina maji safi na salama. Mfano vijiji vya Matiganyora, Nyombo, Lole, Igongolo, Tage, Mende, Kichiwi, Ilengititu, Ibiki, Kidegembye, Havanga, Iyembele, Isoliwaya, Kanikelele, Iwafi, Lima, Welele, Ikang’asi na Igombola havina maji. Tunaomba vijiji hivi navyo viwekwe kwenye mpango wa kupewa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maji imekuwa ikitekelezwa kwa kuchelewa sana na wakati mwingine imekuwa haikamiliki vizuri. Hii ni kutokana na kucheleweshwa na taratibu za manunuzi na zabuni. Mara nyingi wanaochelewesha zabuni hizi na taratibu za manunuzi ni watendaji wetu waliopo kwenye Halmashauri zetu. Hivyo nadhani umefika wakati Serikali iwapime Watendaji wetu waliopo kwenye Halmashauri kwa idadi ya miradi ya maji iliyokamilika ndani ya muda ndani ya Halmashauri zao. Mfano, Mhandisi wa Maji wa Halmashauri atabaki kwenye nafasi yake kwa kupimwa kwa speed yake ya kusimamia miradi ya maji, ubora wa kazi ilivyofanyika, utoaji wa elimu bora kwa watumiaji wa maji kupitia Kamati za Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado fedha inayotengwa kwenye Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Maji haitoshelezi mahitaji ya maji safi na salama nchini. Hivyo, nami naungana na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba iongezwe sh.50/= kutoka kwenye kila lita ya mafuta. Tatizo la maji mijini na vijijini linawaingizia gharama kubwa wananchi, kutokana na gharama ya kununua maji kwa wale wanaouza maji; gharama ya muda ambao akinamama wanatumia kwenda kutafuta maji; gharama kubwa wananchi wanazotumia kutibu magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa maji nchini ni muhimu tuongeze sh.50/= kwenye bei ya mafuta ili fedha hizi ziende kwenye mfuko huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu tumejaliwa kuwa na vipindi vya mvua ya kutosha kila mwaka. Maji yanayotokana na mvua hayatumiki vizuri, yamekuwa yakipotea tu. Ni muhimu Serikali ipitishe sheria ndogo ya uvunaji wa maji toka kwenye majengo yetu, pia maeneo ambayo yana mvua nyingi. Ni vizuri tukaanzisha utaratibu wa kujenga mabwawa ya maji ili yatumike wakati wa kiangazi kwa shughuli mbalimbali, pia uvunaji wa maji maeneo ya mvua nyingi itasaidia kupunguza mafuriko maeneo ambayo maji haya huelekea, yaani maeneo ya uwanda wa chini (low land).

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naunga mkono hoja.