Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nianze kwa kusema kwamba katika hotuba ya Kambi ya Upinzani niliweka utafiti kadhaa uliofanywa na TWAWEZA na sisi tunawaamini TWAWEZA kwamba ni Taasisi iliyosajiliwa na inachokifanya nadhani Serikali wanajua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina wasiwasi kwamba tumeendelea kurudia kosa ambalo mwaka 2016 tulilifanya la kuendelea kutenga fedha nyingi za nje tukitegemea kwamba tuzipeleke kwenye miradi ya maji vijijini, fedha ambazo hazitoki. Ukisoma randama, inaonyesha kwamba katika hizi shilingi bilioni 623 za maendeleo zilizotengwa mwaka huu, shilingi bilioni 214 zinategemewa kuwa ni fedha za wahisani. Kwa bahati mbaya, kati ya hizo 214 shilingi bilioni 130 zinakwenda kwenye miradi ya maji vijijini. Wasiwasi wangu ni kwamba, tutaendelea kufanya kosa lile lile, Waheshimiwa Wabunge watakuja hapa mwakani kulalamika kwa sababu fedha hizi hazitatoka na miradi ya maji vijijini itakwama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wazungumzaji waliopita wamesema, kwamba kulikuwa na haja leo Mheshimiwa Waziri wa Fedha awepo, namwona Naibu Waziri wa Fedha yupo. Atakapokuja kuchangia aseme, kwa nini fedha za mwaka 2016 za Wahisani hazikutoka? Unakuta mradi ambao Wahisani waliahidi shilingi bilioni 41 wametoa shilingi bilioni moja; ni kana kwamba wanatutania, huu ni mzaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili lazima tuliweke wazi, kwamba hizi fedha shilingi bilioni 214 za Wahisani ambazo mnazitegemea, ni fedha ambazo mimi naziona kama kiini macho, sizitegemei kupatikana. Lazima Serikali ije na maelezo, kwa nini fedha za Wahisani hazitoki? Isiwe tunaishia tu kwamba tunapanga tunazitumaini shilingi bilioni 200 zitakuja, halafu hazitoki na Serikali haiji na maelezo kwamba kwa nini hatukupata fedha kutoka kwa Wahisani?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwamba sh.50/= iongezeke ili fedha za Mfuko wa Maji uweze kuongezeka. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maji, tumetembelea miradi mingi. Hizi fedha asilimia 19.8 zinazosemwa, kati ya hizo, zaidi ya 8% mpaka 9% ni fedha za Mfuko wa Maji. Kwa hiyo, kama siyo Mfuko wa Maji kuwa na fedha, leo tungekuwa tunazungumza chini ya asilimia 10 ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara hii. Kwa hiyo, tunahitaji fedha iongezeke ili angalau mwakani bajeti iwe imetekelezwa kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie miradi ya skimu za umwagiliaji. Mheshimiwa Waziri aje atueleze, kuna skimu nyingi nchi hii, karibu kila Halmashari. Zilianzishwa mwaka 2014/2015, 2015/2016 na 2016/2017, fedha zimeliwa. Mfano mzuri ni Skimu ya Umwagiliaji Narunyu pale Kiwalala kwenye Halmashauri yetu, shilingi milioni 600 imeliwa, halafu Mkandarasi anasema kwamba Designer alikosea. Kwa hiyo, hizi shilingi milioni 600 zimeliwa, nani ana-compensate?

Mheshimiwa Naibu Spika, kilio hiki hakipo Lindi Vijijini tu, kipo karibu nchi nzima. Aje na maelezo, kuna miradi mingi na kwenye hotuba ya kambi tumeorodhosha. Aje atujibu kwa nini miradi ya umwagiliaji imetafuna fedha za Watanzania halafu imeishia katikati na hakuna maelezo? Atueleze, hao waliohusika na wizi huu wamewajibikaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie suala la Bonde la Rufiji. Nasikitika sana, leo nchi hii tunalia na njaa. Bonde la Rufiji lina maji the whole season. Ukipita pale unakutana na maji, yapo. Bonde liko zuri, kwa hiyo, katika kilimo cha mwagiliaji kwa nini hatulitumii? Leo tunalalamika kwamba tuna njaa, wenzetu, jirani zetu hapo South Sudani wana vita, wenzetu Wakenya wanahitaji chakula, Ethiopia wanataka chakula; tunashindwa kutumia chanzo ambacho tungeweza kukitumia kama pato letu la Taifa? Lingeongeza pato; lakini pia leo tusingekuwa na malalamiko kwamba chakula hakuna nchi hii. Tungekuwa na chakula ambacho tungeweza kusaidia hata Mataifa mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba maelezo ya kina. Kwa nini bonde la Rufiji halitumiki? Sisi tunaopita pale kila siku kwenda Lindi na kurudi, tunajisikia aibu. Mwaka 2016 nilisema hapa, wale RUBADA; kitu kinachoitwa RUBADA, kama kuna watu wanaofilisi nchi hii, wale wanaongoza, kwa sababu hakuna wanachokifanya. Wako pale, sasa hivi wamekuwa kama madalali wa kuuza ardhi, madalali wa kuingiza mifugo; ng’ombe kuingia pale, hakuna zaidi ya hilo. Kwa hiyo, naomba maelezo ya kina juu ya suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.