Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili nami nipate fursa ya kuchangia katika Wizara hii nyeti sana ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama wenzangu walivyolalamika na kuonesha kwamba bado tuna tatizo kubwa la maji, nami Dar es Salaam tatizo lipo; na ukingalia takwimu za Mheshimiwa Waziri, zinaonesha kwamba katika maji tumetoka asilimia 72 tumekwenda asilimia 75, lakini kwa masikitiko makubwa, sisi watu wa Dar es Salaam hatuna mbadala wa maji. Unapotupa maji asilimia 75 maana yake hii asilimia 25 nyingine tunaitoa wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna mito kusema kwamba tutakwenda kuteka maji kwenye mito, hatuna maziwa, hatuna visima. Kwa hiyo, maana yake kutoa maji asilimia 75 Dar es Salaam ni kuwaambia wananchi wa Dar es Salaam asilimia 25 watumie maji machafu; na hata hivyo visima ukichimba havichimbiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Dar es Salaam kuna maeneo mengi hakuna maji. Mengi sana, Majimbo yote, Dar es Salaam yote; ukienda kwa kaka yangu Mheshimiwa Mnyika utakuta kuna maeneo mengi hakuna maji, ukienda kule Kigamboni hakuna maji, ukienda huku Kawe hakuna maji. Sasa sisi tuna tatizo hilo kubwa sana la maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna tatizo lingine ambalo hatuwezi kulalamika sana ambalo ni tatizo la fedha na Waheshimiwa Wabunge wenzangu hapa wamechangia kwamba tuongeze tozo ya sh.50/=. Mimi bahati nzuri nipo kwenye Kamati ya Nishati na Madini na kama kuna jambo ambalo lina tozo kubwa, basi mafuta yana tozo kubwa sana. Sipingi kuongezwa sh.50/= lakini nataka nitoe njia mbadala.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna hii Mamlaka yetu ya EWURA ambayo inasimamia tozo hizi za kwenye mafuta; na kuna vinasaba ambavyo tunavigharamia, lakini katika tozo la vinasaba kwa Tanzania tunafika mpaka shilingi sita na senti kidogo, lakini ukienda wenzetu wa Kenya na Uganda wana shilingi moja na shilingi mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua teknolojia yawezekana ni ya juu sana kwa sababu sisi tunatumia chemicals, wenzetu wanatumia marking kwa maana wakati mwingine ni kubadilisha tu rangi ya mafuta, inajulikana kwamba haya yamechakachuliwa, haya hayajachakachuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali sasa wanapokwenda kukaa, watazame; wakati umefika sasa, ni bora kutumia teknolojia ambayo tunadhani itakuwa na gharama nafuu hata kama ubora wake utakuwa siyo sawa na ubora wa sasa ili isiwe tu kila tunapopata tatizo tunaongeza tozo la mafuta ambayo athari yake kimsingi ni lazima itarudi kwa mwananchi. Huyo mwananchi tunataka kumkomboa ili apate maji, lakini huyo huyo tunamwongezea mzigo. Kwa sababu huduma zote mwananchi anazopata kijijini lazima atatumia mafuta. Hakiendi chochote lazima mafuta itatumika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, badala ya kutumia shilingi sita, tutumie zile shilingi mbili au shilingi moja ili sasa upungufu iwe ndiyo pesa ambayo tunaweza tukaitumia tukaingiza kwenye maji ili mwananchi asipate mzigo wa moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tuna tatizo la ukosefu wa maji na takwimu hapa ninazo. Ukiangalia vitabu vya Mheshimiwa Waziri, ameeleza hapa. Mwaka 2016 maji ilikuwa kila mwananchi anaweza kupata mita ya ujazo 1,952, lakini katika kitabu chake cha 2017 ameonesha kwamba inapungua mpaka 1,800. Ukiangalia 2025 inakadiriwa maji yatapungua mpaka millimeter 1,500.