Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Lathifah Hassan Chande

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabla ya yote napenda kutoa pole zangu kwa familia zote zilizokumbwa na msiba huu mkubwa, kwa kweli ni janga kubwa katika Taifa letu. Vilevile ningependa kutoa pole kwa Mbunge wa Mkoa wa Arusha Mheshimmwa Godbless Lema. Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi, Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia katika Wizara hii hususan juu ya Sera ya Serikali ya 2002 iliyoelekeza kwamba wananchi waweze kupata huduma ya maji ndani ya umbali usiozidi mita 400, lakini ni dhahiri kwamba imeonesha hadi sasa hii sera imeshindikana kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba maji ni uhai. Mwanadamu akose kila kitu lakini si kukosa maji. Sasa pale ambapo Serikali inaweka mipango ya maendeleo, hata kama ikaweza kufanyia kazi mipango yote isipokuwa hili suala la maji basi nisawa sawa na bure. Kwa sababu mwananchi analazimia kutumia muda mwingi katika kutafuta maji kuliko katika kufanya shughuli za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inavyosema kwamba uchumi unakua kwa asilimia saba ni bure kama mwananchi analazimika kutembea umbali wa hadi kilometa tano hata kumi kwa ajili ya kutafuta maji. Hii sera imeshindikana si kwa vijijini tu, mfano mkubwa ni mkoa wetu wa Lindi ambako maji ni janga kubwa mno kiasi cha kusababisha maji kuwa yenye thamani kama dhahabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Hospitali ya Sokoine hakuna maji, kweli hospitali inakosa maji au kwa kuwa Mawaziri mnapata maji hadi majumbani mwenu? Akina mama wanaenda kujifungua hospitali huku hakuna huduma ya maji wagonjwa wanaenda hospitali wanaolazwa pale wanakosa huduma ya maji, jambo ambalo linasababisha kuwa prone katika kupata magonjwa ya mlipuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wauguzi wanakosa huduma ya maji, madaktari wanakosa huduma ya maji kweli Serikali inaliona hili tatizo na kukaa kimya bila kukuchua hatua yoyote? Kusema ukweli hili ni suala la kusikitisha mno kwa sababu hadi vyoo navyo vinakosa maji pale hospitalini, naomba mliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hapo tu unapoingia vijijini vile vile hali ni mbaya zaidi katika mkoa wetu wa Lindi. Hatuna maji katika Wilaya za Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Mchinga, Mtama pamoja na Kilwa. Ni sawa sawa na kwamba sisi hatustahili kuwa na haya maji, kitu ambacho ni muhimu kuliko vitu vyote ambavyo binadamu anahitaji. Ukienda Liwale si vijijini tu, ukienda Ruangwa siyo vijijini tu bali hata mjini tunakosa maji, naomba mliangalie hili. Wananchi wanalazimika kutembea umbali wa kilometa tatu hadi kilometa kumi kwa ajili tu ya kutafuta maji, na mwisho wa siku hawapati maji safi na salama kwa sababu wanaishia kufuata na kutumia maji ya madimbwi na maji ya mabwawa ambayo pia wanyama wanatumia maji hayo hayo.