Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii kuweza kuchangia na kwa niaba ya wapiga kura wangu wa Geita Mjini, naomba nitumie nafasi hii pia kuwataarifu kwamba lile tatizo lao la watu wa TFS kuweka alama kwenye nyumba ambazo zipo katikati ya Mji wa Geita wakidai ni hifadhi, nilishamjulisha Waziri wa Maliasili na kwamba tunachosubiri ni maombi ya RCC ili waweze kufikia maamuzi ya kuliachia eneo hilo. Maamuzi hayo yanachelewa sana na wananchi wanaendelea kusumbuliwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wananchi wa Geita wanaomba kuona unachukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mbunge, Mheshimiwa Doto Biteko, nimesomeshwa na pamba, lakini pia nimesomeshwa na uvuvi. Nimesomeshwa na uvuvi, natoka kilometa mbili kutoka Ziwani ndiko nilipozaliwa; na eneo letu tulilokuwa sisi tulikuwa na mashamba makubwa sana ya Nyanza wakati ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na pongezi nyingi sana ambazo nampatia Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwenye Wizara hii, hasa kwa kuondoa kero nyingi kwenye zao la pamba. Pia ninaomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba Nyanza Cooperative Union, mali zake ambazo zilihujumiwa kinyemela, zinarudi na hatimaye Nyanza iweze kusimama imara. (Mkofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha mkataba inaoneka sasa hivi ni suala geni lakini sisi wakati tunakua wakati ule, pamba ndiyo lilikuwa zao la kujivunia kwenye Kanda ya Ziwa na umaskini wa wananchi wa Mkoa wa Geita na Mikoa ya Kanda ya Ziwa inaonekana kudorora kwa zao la pamba. Wakati huo mashamba yote ya pamba makubwa na mazuri uliyokuwa unayaona, wananchi walikuwa wanalima yalikuwa aidha ni ya Nyanza au ni ya watu walikuwa wanakopa pembejeo. Mfumo wa kukopa pembejeo ulikuwepo tangu zamani wala siyo mgeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi walikuwa wanapewa mbegu bora, walikuwa wanapewa madawa na baadaye vyama vya ushirika kwa sababu vilikuwa vina nguvu, vilikuwa vinaweza kununua yale mazao kwa wakati na kuwalipa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri kuona namna ya kuimarisha vyama vya ushirika kwa sababu ndiyo reliable vinaweza kuwakopesha wakulima. Kama hilo haliwezekani, ni kuona namna ya kuwafanya hawa private buyers ambao mnawapa usajili waweze kuwa engaged namna ya kuwasaidia wakulima. Bila kutatua tatizo la kuwapatia pembejeo na mbegu bora wakulima, hatuwezi kulifanya zao la pamba likarudi kwenye nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna ambayo naiona hapa, kwanza wakulima sasa hivi wamekata tamaa kwa sababu ukiacha wastani wa heka moja kuzalisha tani mbili na kilo 200 wengi wanazalisha kilo 100 au kilo 200. Sasa kilo 200 hata kama ungempa kilo moja Sh.2,000/= bado hawezi kulipa gharama za kilimo, productivity imeshuka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu mkulima kama ataweza kuzalisha tani moja kwenye heka, hata ukimpa kilo Sh.1,000/= utakuwa umemsaidia. Tatizo kubwa liko wapi? Tunao Maafisa Ugani wengi sana kwenye Halmashauri za Wilaya, lakini nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri hawa watu hawapewi target. Ameajiriwa, amepewa ofisi, amepewa Kata, hakuna mtu anayemsimamia. Nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, hebu aweke utaratibu wa kuhakikisha kwamba hawa watu wanakaguliwa, wanapimwa kwa kitu fulani ambacho wamekifanya kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu wanaamka asubuhi, anakwenda anasaini, anarudi, analala, hata katika kijiji ambacho anakaa wakulima hawafahamu. Hata katika kijiji ambacho wanakaa hajawahi kutoa utaalam wa aina yoyote. Kwa hiyo, matokeo yake wakulima wameligeuza zao la pamba kuwa zao la pili na wengi wamehama. Wengi wanakwenda kwenye mazao mengine kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Geita watu wengi wanalima mpunga; na mpunga kwa sababu pia hata utaalam wa watu wengi wanalima kutokana na ulimaji wa asili, wamehamia huko kwa sababu ni zao la chakula na zao la biashara. Kwa hiyo, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri Maafisa Kilimo, hata angeajiri wengi namna gani, kama waliopo hawasimamiwi, bado zao la pamba litaendelea kuwa chini kwa sababu hakuna uzalishaji ambao unaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba nilisomeshwa na samaki. Naomba hapa Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri. Ipo sheria ambayo ilitungwa mwaka 2003 na kanuni yake ya mwaka 2009. Sheria ambayo inasema “it is illegal to manufacture, possess, store, sell and use or cause another person to use for a fishing gear of more than 26 mesh deep in the Lake Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lugha ya kawaida wanasema ni makosa kuzalisha au kukutwa una nyavu ambayo ina macho 26. Sasa macho 26 nikifanya mikono yangu miwili hapa, tayari ni macho 26 ya mtego.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anatoka kisiwani, tumevua wote samaki. Naomba nimkumbushe, ukitoka Mwanza South pale ukaenda Nautical Mile 15, chini ni mita 70, hebu aende na hiyo nyavu ya macho 26 akavue samaki kama atapata kilo tano. Kinachofanyika sasa, imetungwa sheria, hiyo sheria imeipitishwa lakini inahamasisha watu waende kuvua samaki kwenye breeding areas. Wanakwenda kwenye zile breeding areas ambazo tungetarajia ziwe hifadhi, samaki wazaliane kwa sababu nyavu wanayopendekeza ambayo wanaiita illegal, ni nyavu fupi. Ni mikono yangu miwili hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Gozba ni mita 100 chini. Nataka nimpe challenge Mheshimiwa Waziri, nimefanya kazi ya samaki miaka 25. Kama ana wataalam wake wa uvuvi awaambie waweke nyavu 100 twende Gozba, wakirudi na kilo kumi naacha Ubunge. Naacha Ubunge kwa sababu wanachokifanya ni kuwaonea kabisa wavuvi. Wanaenda wanachukua zile nyavu, wanaita illegal wanazichoma moto.

Mheshimiwa Naibu Spika, mvuvi gani anatengeneza nyavu? Nyavu zimepita bandarini, zimelipiwa ushuru, mvuvi amekopa pesa benki, amekwenda kuweka kwenye mtumbwi, size ya nyavu anayotaka ni ile ile nchi tano au sita ambazo wameruhusu; lakini wanasema ikishazidi macho 26 ni illegal. Sasa wakati inapita bandarini watu wake walikuwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu. Yeye kama ni mvuvi na anafahamu mambo ya uvuvi twende ziwani. Wavuvi wetu wengi ni local, wanafanya traditional fishing, hakuna mwenye fish finder; hakuna mwenye chochote. Kwa hiyo, hakuna anayeona samaki chini. Tuchukue hizo nyavu tuende nautical mile 50 tukatege, halafu turudi kesho tukavue; tukipata samaki kilo 50, mimi naacha Ubunge. Kwa sababu nimefanya kazi hii kwa miaka 20 na nimekimbia huko kwa sababu ya masharti mengi yasiyo na maana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachomaliza samaki Ziwa Victoria ni matumizi ya monofilament na matumizi ya makokoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nashukuru sana.