Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuungana na wachangiaji waliopita katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ahadi zake za kuondoa tozo mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, nampongeza sana. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Makatibu wao kwa taarifa yao nzuri. Tunajua ameingia hivi karibuni, lakini taarifa hii inaonesha mtu huyu ana uwezo wa kuibeba hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Kamati ya Kilimo, imechanganua vizuri sana. Naipongeza kwa kweli Kamati mmefanya kazi yenu vizuri sana, hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ni uhai, kilimo ni viwanda, kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa letu. Nchi ikikosa chakula, haina utengamano wa kisiasa, kiusalama na hakuna atakayekusikiliza kwa jambo lolote lile. Ndiyo maana Waswahili wanasema adui mwombee njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, bajeti ya kilimo kama wenzangu walivyotangulia kusema, ni ndogo sana. Hata tuseme maneno namna gani, tutamlaumu Mheshimiwa Waziri bure, bajeti ni ndogo. Sisi wote tuungane kusukuma jambo hili kwamba bajeti haitoshi. Kama kweli kilimo ni uti wa mgongo, ni wazi kwamba tukubaliane bajeti hii haitoshi. Tusiposhikamana, basi tusilaumiane, turidhike na kilichopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kuwapongeza wananchi wa Mkoa wa Rukwa kwa jitihada walizonazo za kilimo. Wananchi wa Mkoa wa Rukwa hawahimizwi kulima, hapana. Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanaweza kudhoofishwa na kilimo kwa kukosa soko, kwa kucheleweshewa pembejeo, mbegu na kupewa madawa feki. Ukiwatimizia mambo hayo wananchi hawa ni hodari kwa kilimo. Hata mwaka huu wamelima vizuri sana, wafanyabiashara njooni mnunue mahindi mkoa wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni kilimo cha umwagiliaji. Lazima tukubali kwamba ili twende mbele bila mashaka, ni lazima tukubaliane kwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji. Nchi yetu ina hekta za kilimo milioni 29.4 ambazo zina sifa ya umwagiliaji, lakini mpaka sasa tunatumia hekta 463,000 tu. Kwa hiyo, hatujafikia hata 2% ya eneo tulilonalo la umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya nini ili hizi fursa ambazo tumepewa na Mwenyezi Mungu tuzitumie kikamilifu? Kilimo cha umwagiliaji ndiyo kinaweza kulivusha Taifa hili na kuliweka mahali pazuri. Kwa hiyo, tunaomba Wizara na Serikali itambue jambo hili kwamba ni la muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hifadhi ya chakula ni muhimu sana kwa sababu hatuwezi kumpangia Mwenyezi Mungu kwamba mvua hii itanyesha mwaka huu, mwaka kesho; lazima tuweke chakula cha kutosha hata cha miaka mitano. Unapowapa NFRA shilingi bilioni tisa, maana yake unategemea kununua tani karibu 180,000 ambazo ni Mkoa wa Rukwa peke yake unaweza ukatosheleza. Lazima tutenge pesa za kutosha kwa ajili ya kununua chakula cha kuhifadhi kama akiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye ujenzi wa maghala. Wananchi wetu wakati mwingine wanaharibu chakula kwa hofu ya kwamba mazao yao watayaweka wapi? Yanaweza yakanyeshewa na mvua, lakini tungekuwa na maghala ya kutosha, wananchi wangeweza kuhifadhi mazao yao pale anapokuwa na shida ya kuuza anakwenda anauza. Analazimika kuuza kwa lazima kwa sababu hawana mahali pa kuhifadhi; na uwezo wa kujenga maghala hawana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nizungumzie migogoro ya wakulima na hifadhi za akiba. Jambo hili limezungumzwa mara kadhaa; lipo tatizo kubwa sana la mgogoro wa Hifadhi ya Uwanda Game Reserve na wananchi. Hili eneo ni dogo. Bahati nzuri nimemwambia Mheshimiwa Waziri mara kadhaa, rafiki yangu, Mheshimiwa Maghembe, ikiwezekana basi aende akaone suluhisho la kufanya juu ya mgogoro ule. Ataacha watu wauane! Aende ikiwezekana akarekebishe mipaka. Namwomba sana angalau uende, wananchi wakuone inaweza kusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni shamba la Malonje. Shamba hili nimelizungumzia miaka sita. Sijui kuna mwarobaini gani katika jambo hili? Kwa mara ya mwisho amekuja Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Lukuvi akasema mimi ndio nitakuwa wa mwisho kuzungumzia mgogoro wa shamba hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nasema Mheshimiwa Lukuvi ni hodari, anafanya kazi vizuri sana na Naibu wake. Amefanya kazi katika maeneo mengi, tunamsifu, lakini kuna mfupa gani umemshinda katika shamba hili? Kuna tatizo gani? Shamba tumelizungumzia miaka sita na yeye alisema atakuwa mtu wa mwisho kuzungumzia mgogoro huu, kuna tatizo gani katika jambo hili? Huu mfupa hata fisi anang’ang’ania mpaka anaupasua, hata kama ni mkubwa kiasi gani!

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba akamalize mgogoro huu, wananchi wamenipigia simu Jumanne wamechangishana pesa wanakwenda ofisini kwake kupata mwarobaini wa jambo hili. Limechukua muda mrefu mno, wananchi hawana mahali pa kulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, jambo hili walishike vizuri walimalize kwa usalama. Kwanza wanamtia hofu hata mwekezaji mwenyewe, wanamfanya asifanye kazi kwa uhuru kwa sababu ana mashaka na hata wananchi. Pande zote mbili zinahitaji suluhu ili jambo hili liishe na usalama uweze kuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na nasisitiza sana, Mheshimiwa Waziri mgogoro huu waweze kwenda kuumaliza ili wananchi waweze kupata mahali pa kulima. Ila namjulisha kwamba wananchi wamechangishana pesa wanakwenda ofisini kwake, vijiji vyote vinavyozunguka shamba lile, Jumanne wanakwenda. Shamba hili limechukua muda mrefu mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kwa leo naishia hapo. Naunga mkono hoja.