Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Mendard Lutengano Kigola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Rais wetu.
Kwanza kabisa, naunga mkono hotuba hii ambayo ni hotuba nzuri kabisa ametoa kwa Watanzania wote na wamemuelewa vizuri sana.
Mheshimiwa Hotuba hii inatoa mvuto sana siyo kwa Watanzania tu ni watu wote ulimwenguni. Kuna Marais wengi sana wanatoa hotuba, lakini hotuba hii imekuwa ya mvuto kwa sababu amesema kile kitu ambacho wananchi wanakihitaji. Hotuba yake imetokana na jinsi alivyotembelea wakati wa kujinadi, amepita Wilaya zote za Tanzania na majimbo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kero za wananchi zinaeleweka na Rais ameweza kuelezea vizuri sana kwenye hotuba yake. Kwa mfano, ameelezea vizuri sana masuala ya maji, barabara, umeme na afya. Wabunge wote tunaungana na hotuba hii ambayo imekuwa kama mwongozo kwa shughuli zote ambazo Wabunge tunazifanya kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais ameongelea sana Tanzania iweje na ameliongelea kwa mapana yake. Kitu ambacho kimenifurahisha, ahadi zake ambazo alizitoa wakati wa kampeni, ndani ya miezi mitatu sasa hivi tukianzia mwezi Novemba, Disemba na sasa ni Januari tayari ameanza kutekeleza zile ahadi ambazo aliahidi. Ahadi ya kwanza ambayo sisi Watanzania tunahakikisha kwamba ameanza kuitekeleza, alisema kwamba elimu bure kwa watoto wetu na hili limeanza kutekelezwa. Hakuna mtu ambaye hasikii wala haoni, tumeshaona. Kufanya utekelezaji ndani ya miezi tatu duniani haijawahitokea kwa Rais yeyote, huyu ni namba moja. Kuna watu wengine wameanza kusema anatekeleza kidogo kidogo, wewe hata nyumbani kwako umetekeleza mangapi, hicho kidogo kidogo umeweza? Nataka niwaambie Rais tusimkatishe tamaa, Rais wetu ameshaanza kufanya kazi na inaonekana kwa Watanzania na lazima tumuunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili alisema atapunguza matumizi makubwa kwa Serikali, Rais ameanza kupunguza na vitu vinaonekana. Jambo la kwanza alisema atapunguza Baraza la Mawaziri na amepunguza kutoka Mawaziri 60 kuwa 34 ni hatua kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu alisema atapambana na mafisadi na tumeona TRA kilichotokea ndani ya mwezi mmoja ilikuwa ni balaa, ilikuwa ni mtafutano, hiyo yote ni ahadi alisema ataifanyia kazi. Pia alisema atapeleka watu mahakamani na tumeona ameanza kufanya kazi hiyo. Sasa nataka niseme, kwa mwenendo huu Tanzania ambayo tunaihitaji ndiyo inakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ameongelea sana masuala ya viwanda kwamba Tanzania itakuwa nchi ya viwanda. Uchumi wa nchi yoyote ukitaka upande lazima uhakikishe viwanda ndani ya nchi yako vinafanya kazi ya uzalishaji vizuri, mimi nakubaliana naye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kwamba Tanzania hatuna viwanda lakini havifanyi kazi kwa ile standard ya viwanda vilivyoko duniani. Kwa mfano, mimi natoka kwenye Jimbo la Mufindi Kusini, Wilaya ya Mufindi tuna viwanda vingi sana tukianza na Kiwanda cha Chai ambacho ni kikubwa katika Afrika; Kiwanda cha Karatasi pale MPL ni kikubwa sana katika East Africa na Kiwanda cha Pareto ni kikubwa katika dunia siyo Afrika. Tatizo kubwa ambalo tunalipata ili ku-improve uzalishaji ni miundombinu mibovu. Hivi sasa navyoongea kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini ambako kuna Kiwanda cha Chai na wakulima wa chai wako pale kuna magari mengi sana yanakwama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze Rais kipindi alipokuwa Waziri wa Ujenzi barabara ile alishaanza kuifanyia kazi. Nina maana kwamba upembuzi yakinifu alishamaliza tayari na kwenye ripoti ya RCC waliyotoa walisema kwamba upembuzi yakinifu uliisha Mei, 2015. Kwa hiyo, nataka nitoe taarifa kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi kwamba barabara ya kutoka Nyololo – Mtwango - Mgololo na kutoka Mafinga - Mgololo ambayo ina kilometa 84 na kutoka Nyololo - Mtwango ni kilometa 40 upembuzi yakinifu ulishaisha na Serikali iliahidi kwamba itaitengeneza kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, mategemeo yangu ni kwamba bajeti tunayokwenda kupitisha sasa hivi siyo ya upembuzi yakinifu tena ni ya kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami ile barabara ambayo aliahidi Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli na kwenye kampeni alisema ataijenga. Ninavyomfahamu tukimaliza bajeti hii ataanza kujenga kule kwa sababu amesema anataka kuimarisha viwanda na hizi barabara zote zimekuwa connected kwenye viwanda siyo kwamba zimejengwa tu, unapojenga barabara lazima uangalie inaenda wapi. Hizi barabara zimejengwa kwenye viwanda ambapo tumesema Tanzania inakuwa ya viwanda tu, viwanda hivyo vipo lakini miundombinu ni mibovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine la muhimu sana kwenye viwanda hivi ni lazima tuhakikishe tuna-improve masuala ya umeme. Bahati nzuri juhudi za Serikali ni nzuri maana tunazungumzia masuala ya gesi, kila mtu anasikia na juhudi tumeziona na tumeona REA wanavyofanya kazi, wanapeleka umeme kwa kila kijiji. Nashukuru sana Mungu Waziri wetu Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo amerudishwa tena kwenye Wizara hiyo kwa sababu alifanya kazi vizuri sana, vijiji vingi sana vilipata umeme. Kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini kuna vijiji vingine hata ndoto tu kuota kwamba vitapewa umeme ilikuwa haipo sasa vilishapata umeme. Vijiji hivyo ni Kata ya Malangali, Ihoanza, Mbalamaziwa huo umeme unaelekea kwa jirani yangu wa Makambako. Ingawa juhudi ni nzuri lakini kuna vijijji kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini bado havijapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe ushauri kuhusiana na usambazaji huu wa umeme, tunataka umeme uende kwenye vitongoji kwa sababu utakuta umeme unafuata line kubwa tu. Sasa kuna kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata umeme kwenye vitongoji. Nadhani hili tutasaidiana kusimamia ili tuhakikishe vitongoji vyote vinapewa umeme. Kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini kuna vitongoji vingi, nina vitongoji 365, vijiji 88, tutataka tuhakikishe vijiji vyote vinapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, huu umeme unaotoka Mbalamaziwa ambao unaelekea mpaka kule Kinegembasi, kuna vijiji vya Mtambule mpaka kule Kilolo, Hiyawaga, Kiyowela mpaka kule Itika na Iholo mpaka kule Idete havina umeme. Kwa mpango huu, naiomba Serikali, siwezi kutaja vijiji vyote lakini tuhakikishe kwamba kwa mwaka huu tunaosema kwamba tunataka nchi yetu iwe ya viwanda tushughulikie suala hili la umeme. Tunaposema viwanda kuna viwanda vikubwa, vya kati na viwanda vidogo vidogo. Hivi viwanda vidogo vidogo viko kwenye kata na ili wananchi wawe na viwanda hivyo lazima tuhakikishe miundombinu ya umeme imekaa vizuri.
Suala lingine ambalo ni la mwisho ni maji. Kila Mbunge akisimama hapa anauliza masuala ya maji. Bahati nzuri Serikali ilijitahidi sana kujenga matenki ya maji katika kila kijiji. Kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini, kuna matenki 11 hayafanyi kazi mpaka mimi Mbunge niliamua kuanza kuchimba visima tu lakini huwezi kuanza kuchimba visima kwenye maeneo ambayo mikondo ya maji ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Maji atambue kwamba hii siyo miradi mipya ni ukarabati wa miundombinu ya maji. Pale Igowole pameshakuwa mji kuna tenki la maji kubwa sana lakini halina maji, lina miaka zaidi ya 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda pale Nyololo kuna tenki la maji la muda mrefu, wananchi hawapati maji ya gravity system, mimi Mbunge nimechimba visima pale. Sasa namwomba Waziri haya matenki ambayo yapo ni miundombinu chakavu basi muweze kuitengeneza.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri kwenye swali la msingi lililokuwa limeulizwa hapa, anasema kwamba kuna shilingi trilioni moja imetengwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji. Namuomba Waziri asisahau Jimbo la Mufindi Kusini. Nimeshaanza kutaja pale Igohole, Nyololo, Nyigo, Idunda, Itandula mpaka Iramba kuna matenki ya maji tayari, ni kutengeneza miundombinu na kuwawezesha wananchi maji yaingie kwenye tenki na ku-supply kwa wananchi basi. Hizo shilingi trilioni moja siwezi kuzimaliza, mimi hata ukinipa shilingi milioni 800 za kuanzia siyo mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Maji kwenye mgao huu unaokuja asinisahau kwa sababu hayo matenki yapo tayari. Wakati tutakapokuwa tuna-discuss bajeti inayokuja mwezi Mei au Juni, nikiona bajeti ya vijiji vyangu haipo hiyo bajeti haitapita, nafuu nianze kusema mapema na nitakuwa namkumbusha kila wakati, haya ni masuala ya msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni masuala ya ardhi. Masuala ya ardhi imekuwa kero sana. Bahati nzuri Waziri ameanza mpango mzuri sana, ametugawia barua tuwasilishe matatizo. Kuna mgongano kati ya Maliasili na Ardhi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kigola muda wako umekwisha.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)