Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunipa afya njema hadi leo ninapohitimisha majadiliano ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017. Ninakushukuru sana wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Mheshimiwa Spika ambaye kwa sasa hayupo Mezani na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia kwa umakini mkubwa majadiliano ya hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niwashuhukuru Waheshimiwa Mawaziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Possi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini, Makatibu Wakuu wote watatu, Wakurugenzi na Wakuu wa taasisi zote za Ofisi ya Waziri Mkuu. Nitumie nafasi hii pia kuwashukuru watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kunipa ushirikiano mkubwa wakati wote katika utumishi lakini pia katika kuandaa shughuli hii ambayo leo tunaihitimisha hapa mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kwa ujumla wenu, kwa namna ya pekee kwa michango yenu ya kina ambayo imefanikisha kwa kiasi kikubwa kuboresha mipango na kazi ambazo zimekusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka huu wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kutoa majibu, maelezo mbalimbali ya wachangiaji, nitumie nafasi hii kupitia Bunge lako Tukufu kutoa pole kwa wananchi wetu waliokumbwa na maafa makubwa kule Mkoani Morogoro, Wilaya ya Kilosa lakini pia Wilaya za Rombo na Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro. Taarifa si nzuri sana kwa sababu Wilayani Rombo tumeweza kupoteza kwa vifo Watanzania wenzetu wanne, Moshi Vijijini Watanzania watatu lakini pia kuna uharibufu mkubwa wa nyumba, mali, ikiwemo mashamba na vyakula. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwapa pole wote na wale ambao wametangulia mbele za haki tumwombe Mwenyezi Mungu aweke roho zao mahali pema peponi. Serikali itafanya jitihada za kuokoa wale ambao bado wamekwama na janga hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kuwapa taarifa Watanzania kwamba Taasisi yetu ya Hali ya Hewa imeendelea kutupa tahadhari kubwa kwamba kipindi kilichobaki kufikia mwanzo mwa Mei, mvua zitaendelea kunyesha kwa kasi kubwa.
Kwa hiyo basi, wale wote ambao wako maeneo hatarishi waanze kuondoka katika maeneo hayo waende maeneo salama ili kuepusha majanga yanayoweza kujitokeza tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa nimetoa salamu za shukrani pamoja na pole kwa waliopata maafa, sasa nijikite katika mjadala huu ambao ulichangiwa na jumla ya Wabunge 93; Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa maneno ni 80 na waliochangia kwa maandishi 13. Wote hawa wameweza kutoa mchango wao kwa kina kupitia bajeti yetu ambayo leo hii niko hapa kwa ajili ya kuhitimisha. Napenda niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa hoja zao nzuri. Hata hivyo, kutokana na muda, naomba nisiwataje kwa majina lakini naomba majina yao yaingizwe katika Hansard.
Serikali imejibu hoja hizo kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri lakini hoja zilizosalia zitajibiwa kwa maandishi. Aidha, na mimi nitatumia nafasi hii kutoa ufafanuzi wa hoja chache huku nikijua kwamba kwenye hotuba yangu nilizungumzia sekta mbalimbali za Wizara za Kisekta lakini pia nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba sekta zote ambazo zimechangiwa zitajibiwa vizuri na Wizara husika, mimi nitajikita kwenye maeneo ya kisera kupitia sekta hizo zote ambazo zimeweza kuzungumziwa.
Aidha, napenda nitumie nafasi hii ya awali kuwashukuru tena Wabunge wote kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, kwa utendaji wao na kasi nzuri waliyonayo katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru wote wale ambao wameonesha nia ya dhati ya kuunga mkono jitihada hizi za viongozi wetu wakuu katika kutekeleza kauli mbiu ya hapa kazi tu. Ni dhahiri kwamba wananchi wengi wamemuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais. Hivyo, ni wajibu wetu sisi kama viongozi na wawakilishi wao kuonyesha njia bora ya kutekeleza kauli mbiu hiyo na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mimi naamini kabisa kuwa mijadala yote iliyowasilishwa hapa itatusaidia sana kuwa makini zaidi katika kukidhi matarajio ya wananchi wetu katika Serikali ya Awamu ya Tano. Pongezi mlizozitoa Waheshimiwa Wabunge, zimetutia moyo sana na kutupa nguvu zaidi kama Serikali katika kuimarisha utendaji wetu katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa hoja ambazo zilitolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 99(13) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016, naomba sasa nichukue nafasi hii kujibu na kufafanua baadhi ya maeneo ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kama zilivyojitokeza. Katika ufafanuzi huu Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mawaziri walijikita kujibu hoja zilizochangiwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, sikusudii kurudia ila nataka tu niweke nyongeza ya majibu ya Mwanasheria Mkuu juu ya kipengele cha instrument. Eneo hili lina mchakato mrefu, pamoja na uwezo na mamlaka aliyonayo Mheshimiwa Rais ni kwamba Mheshimiwa Rais anaendelea kuiunda Serikali yake, alianza na Mawaziri na Makatibu Wakuu ambao ndiyo watendaji wa Serikali wameteuliwa mwanzoni mwa Januari.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia lazima kuwe na utaratibu wa kila Wizara baada ya kuwa Mheshimiwa Rais ameziunganisha Wizara mbalimbali ili sasa kupata uwezo mzuri wa kuweza kutengeneza hiyo instrument ambayo taratibu zake zimeendelea. Instrument hiyo baada ya kuwa imekamilika na hawa watendaji lazima itangazwe na Gazeti la Serikali. Taratibu zote zikiwa zimeshakamilika ni lazima sasa itangazwe kwenye Gazeti la Serikali lakini utangazaji wa Gazeti la Serikali hauwi kama ilivyo kwenye magazeti yetu ya kawaida ambayo yanatangazwa kila siku, ni baada ya kuwa tumeshapata hoja za kutosha zilizo kwenye Gazeti la Serikali ndiyo unaweza kulitangaza ili wananchi waweze kuona.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwape faraja kwamba instrument za Wizara zote zimeshakamilika na zimesainiwa tarehe 20/04/2016 sasa tunasubiri kutangaza, wakati wowote Mheshimiwa Rais atakapoamua kutangaza zitakuwa zimetoka. Kwa hiyo, Mawaziri walioko kazini sasa wanafanya kazi kwa mujibu wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais lakini pia na Ilani ya Chama kinachotawala ambacho kimeunda Serikali hii. Kwa hiyo, nataka niwape faraja kwamba instrument ipo na imeshasainiwa na watendaji wetu wanafanya kazi kwa mujibu wa instrument hiyo. (Makofi)
Naomba sasa nianze na maeneo ya jumla yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na kama muda ukiruhusu nitaelezea machache pia ya kisekta kama ambavyo nimeeleza. Nianze na hoja ambayo imezungumzwa sana ya kuitaka Serikali iilipe MSD deni la shilingi bilioni 1.13 ili iweze kuendesha shughuli za kusambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini. Nataka nieleze kwamba taarifa iliyotolewa ya MSD kwamba Serikali inadaiwa na jumla ya shilingi bilioni 134 na siyo ile shilingi bilioni 1.34 kama ilivyokuwa imechangiwa. Hata hivyo, nataka nilipe taarifa Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeshaanza kushughulikia deni hilo kwa kumwelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhakiki deni hilo. Mpaka sasa CAG ameshahakiki madeni jumla ya shilingi bilioni 67 na kazi ya uhakiki inaendelea na malipo yatakuwa yanatoka kadri ambavyo CAG atakavyokuwa anaweza kuhakiki ili tuone madai haya na uhalisia wake. Ndiyo mkakati tulionao katika kuhakikisha deni hili la MSD linamalizika.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ilikuwa ni ununuzi wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI lililochangiwa na Wabunge kadhaa pamoja na Kamati ya Bunge ya masuala ya UKIMWI. Kama nilivyoeleza katika hotuba yangu Serikali inao mpango wa kuendelea kununua dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kwa kutumia vyanzo vya ndani na kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache Barani Afrika zinazoweza kuwanunulia wananchi dawa hizo kwa kutumia fedha zake za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanikisha mpango huo, Serikali imeanzisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya kupunguza utegemezi wa wahisani katika ununuzi wa dawa za ARV na mfuko huo unachangiwa sana na Serikali na sekta binafsi. Hivyo naziomba sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia mfuko huo. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 imeshatenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya dawa za ARV.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni suala la vibali vya kuagiza mchele kutoka nje. Limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge, napenda pia kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa hali ya uzalishaji wa mazao ya nafaka hapa nchini imeendelea kuwa nzuri kila msimu. Takwimu za uzalishaji mpunga zinaonesha uwepo ongezeko katika kipindi cha miaka sita iliyopita na takwimu zinaonesha kwamba kiasi cha uzalishaji wa mpunga kimeongezeka kwa tani 1,669,825 kutoka mwaka 2009/2010 hadi kufikia tani 1,936,000 kwa mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 14.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ambayo tunaifanya sasa Serikali ni kuhakikisha kwamba kupitia Wizara ya Kilimo tunaweka mkakati wa uzalishaji wa nafaka zaidi ili tuweze kuzalisha kwa kiwango kikubwa. Ninayo matumani pia kwamba kwa sasa tunayo hifadhi ya kutosha ya chakula kwenye maghala yetu na mkakati huo unaendelea ili tuweze kuwa na akiba ya kutosha kwenye maeneo yetu. Kutokana na mwelekeo mzuri huu wa uzalishaji wa mchele hapa nchini, Serikali imesitisha kutoa vibali vya uagizaji wa mchele kutoka nje kwa lengo la kuleta unafuu lakini pia uthamani wa mchele ulioko ndani na kuimarisha masoko yaliyoko ndani kwa zao hili la mchele. Kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania kwamba hatutakuwa na vibali vya kuagiza mchele kutoka nje.
Hata hivyo, napenda pia kuagiza vyombo vya dola kuendelea kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu yote hasa katika mwambao wa Bahari ya Hindi ili kuzuia uingizwaji holela wa mchele wa magendo kutoka nje ya nchi kwa lengo la kulinda wafanyabiashara na mchele ambao tunao ndani uweze kuingia kwenye masoko tunayoyakusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hili, naomba kuzungumzia suala la upungufu wa sukari nchini. Ni kweli kwamba uzalishaji wa sukari nchini upo chini ya kiwango cha mahitaji. Mahitaji ya sukari nchini ni tani 420,000 na kiwango cha uzalishaji nchini ni tani 320,000 na kweli tuna upungufu wa tani 100,000 na sasa hivi tumeanza kuona upungufu wa sukari.
Nataka niwaambie sukari iliyokuwepo kwenye maghala yetu na viwanda vyetu imepungua lakini tumeshaiagiza na baada ya muda mfupi kutoka sasa sukari itakuwa imeingia nchini. Sukari ambayo tumeiagiza ni ile tu iliyopungua kwa lengo la kuzuia kuingiza sukari nyingi ikadhoofisha viwanda vyetu tulivyonavyo nchini huku tukiwa tumeshaweka malengo ya uzalishaji wa ndani ya nchi ili kuweza kufikia mahitaji ya Kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kuwaeleza wananchi kwamba sukari itaingia baada ya muda mfupi. Nawasihi wafanyabiashara wote wenye sukari, wenye maduka, waitoe sukari waliyonayo kwa sababu takwimu tuliyonayo sasa hivi nchini tuna tani zisizopungua 37,000 ambazo tunaamini zinaendelea kuuzwa na hii itakapoingia itaweza kukamilisha na kuzuia upungufu wa sukari tulionao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kauli hii, natoa agizo kwa Maafisa Biashara kwenye Halmashauri za Wilaya, wafanye ufuatiliaji kwenye maduka yetu kuona kwamba sukari haifichwi kwa lengo la kuuza kwa bei ya juu ili sukari iuzwe kwa bei elekezi ambayo imetolewa na Serikali ili wananchi waweze kupata sukari wakati wote wanaohitaji. Kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba Watanzania na wafanyabiashara wote, sukari hii ambayo tunajua tunayo nchini itatolewa nje ili wananchi waweze kununua kwenye maduka yetu tena kwa bei ileile elekezi kwa sababu upungufu huo unaotamkwa hauko kwa kiwango hicho lakini hata hivyo ule upungufu ambao tunao tayari taratibu za uagizaji wa sukari umeshakamilika na wakati wowote itaingia kwenye soko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni ile hoja ya mfumo wa stakabadhi za ghala, ambao umechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi na Serikali. Mfumo huu ulianzishwa kwa zao la korosho kwanza, kwa nia ya kuwawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa utaratibu wa ushindani baada ya kuyakusanya katika maghala ya Vyama vya Ushirika vilivyo kwenye maeneo yao. Hii ilikuwa inalenga kuwawezesha wakulima kupata kipato zaidi ikilinganishwa na mifumo mingi iliyokuwepo huko nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nakiri kwamba mfumo huu umeleta changamoto nyingi na malalamiko mengi. Nataka niwahakikishie Watanzania na wakulima wa zao la korosho nchini, kwamba mfumo huu ni mzuri, lakini changamoto zake ni zile ambazo zimesababishwa na Watendaji wetu, nami nikiri kwamba tunao usimamizi mbovu wa Vyama vya Ushirika (AMCOS), lakini ia usimamizi mbovu wa Vyama vyetu Vikuu pamoja na Bodi yenyewe. Vilevile uwepo wa makato holela ya hovyo, pia kunakuwa na riba za juu za mabenki yetu ambapo yote haya kwa pamoja yanapelekea mkulima kuwa na pato dogo ambalo pia wakulima wamekuwa wakilalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ambao sasa tunafanya mapitio ya mazao yetu yote makuu nchini ya kuondoa matatizo yaliyojikita kwenye maeneo haya ikiwemo kuyaondoa makato ya hovyo hovyo yaliyopo kwenye mazao haya. Kwa mfumo huu wa Stakabadhi Ghalani ambao umeanza kwenye zao la Korosho, tumebaini pamoja na upungufu niliousema ya usimamizi mbovu, lakini tuna makato tisa ambayo mkulima huwa anakatwa na yote haya yanamsababisha mkulima kupata pato dogo na hatimaye wakulima kulalamika. Mpaka sasa tumeshafanya vikao vya pamoja, Wizara pamoja na Bodi, tumekubaliana na Serikali imeondoa makato sita kati ya tisa ili kuweza kumfanya mkulima aweze kupata tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, makato tuliyoyaondoa ni gharama ya usafirishaji ya zao la mkulima kutoka nyumbani kwake mpaka kwenye maghala na kazi hiyo tumewaachia Vyama vya AMCOS vyenyewe na viko Vyama vya AMCOS vimenunua magari yao, watanunua matrekta yao, watasafirisha wenyewe kwa gharama zao wenyewe badala ya kuwakata kutoka chama kikuu cha ushirika kwa thamani ya shilingi 50. Tumesema kuanzia sasa, minada yote itafanywa kwenye maeneo ya wakulima ili wakulima wenyewe washuhudie minada yao. Badala ya kuipeleka minada eneo la mbali, linamfanya mkulima anashindwa kujua mnada uliofanywa ni wa kiasi gani na una uhalali wa kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna hii itaweza kumdhihirishia mkulima kuona wanunuzi na kusikia kila mnunuzi ananunua kwa kiasi gani na watafanya maamuzi ya kuwaachia korosho au lah ili waweze kupata tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kato la pili ni ushuru wa maghala unaotozwa kule ambapo korosho zinatunzwa. Tumeondoa ushuru huu kwa sababu kila Chama cha Ushirika kimejenga ghala lake. Wakulima walishachangia ujenzi wa ghala lao na korosho zao zitatunzwa kwenye ghala lao na mnada utakaofanywa kwenye eneo lao, hautamlazimisha mkulima kukatwa shilingi 50/= ya kulipa kwenye maghala. Kwa hiyo, makato hayo tumeyaondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, makato mengine ni ya mkulima kulipa Chama Kikuu. Mkulima hana mahusiano na Chama Kikuu zaidi ya kwamba chenyewe ndiyo kinaratibu. Chama Kikuu kimeundwa na AMCOS na kwa hiyo, Chama Kikuu kitatoza mchango kwa AMCOS na kwa hiyo, Chama Kikuu hakiwezi kumtoza mkulima. Tumefuta mchango huo na badala yake fedha ile itarudi kwa mkulima ili iweze kuongeza tija yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na malipo yanalipwa Sekretarieti ya Mkoa, asilimia moja. Fedha hizi ni nyingi kwenda Mkoani, watu wa Mkoa watafanya kazi zao kwa mujibu wa ajira yao ya kufuatilia mwenendo wa zao la Korosho na wala hakuna sababu ya mkulima kuichangia Ofisi ya Mkoa shilingi moja, hiyo ilikuwa ni kupunguza mapato ya mkulima. Tumeiondoa na sasa hivi mapato haya hayatakuwepo tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na makato ya unyaufu wa zao la korosho. Sheria ya Unyaufu inatekelezwa tu pale ambapo korosho itakaa zaidi ya miezi sita na siyo mwezi mmoja. Kwa hiyo, zao hili lilikuwa linakatwa asilimia 0.5 ya unyaufu ambayo tunasema sasa tumeiondoa na fedha hiyo itarudi kwa mkulima mwenyewe, tukiamini kutoka siku mkulima anapeleka ghalani mpaka siku ya mnada haiwezi kuchukua muda wa miezi sita. Kwa hiyo, makato hayo tumeyaondoa na mkulima atapata hela yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kato lingine ambalo tunaanza kuliangalia sasa ni riba ya benki ambapo AMCOS huwa zinakopa benki. Mfumo wa Stakabadhi Ghalani haulazimishi AMCOS kwenda kukopa benki. Unapokwenda kukopa benki inashawishi viongozi wa AMCOS kugawana kwanza na hawalipi na badala yake malipo hayo hulipwa na mkulima. Kwa hiyo, tunaanza kuangalia uwezekano wa AMCOS kukopa benki au mkulima apeleke mazao, asubiri siku ya mnada ili aweze kuuza apate fedha yake yote, badala ya utaratibu wa sasa wa kulipa kidogo kidogo. Wanalipa malipo ya kwanza, malipo ya pili, hiyo haitakuwepo tena kama AMCOS itapeleka mazao hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati huu unaacha malipo yafuatayo tu; mchango wa Halmashauri wa mazao wa 3% mpaka 5%; Mfuko wa Wakfu ambao tumeupa kazi ya kununua magunia na mbolea na kuhakikisha kwamba mkulima anapata pembejeo; na mkulima kuichangia AMCOS yake iliyopo kwenye eneo lake na siyo Chama Kikuu. Kwa hiyo, makato hayo ndiyo pekee ambayo mkulima sasa atakuwa anachangia na kwahiyo, tumeondoa zaidi ya shilingi 360 ambazo alikuwa anakatwa mkulima bila sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na zoezi hili la kufanya mapitio ya kila zao maarufu ikiwemo la pamba, kahawa, chai pamoja na tumbaku ili kuhakikisha kwamba wakulima wa mazao haya, wanapata unafuu. Na mimi nitalisimamia mwenyewe kwa kupita kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kutoa huduma kwa wananchi na Mikoa, lakini pia kulikuwa na changamoto ambazo Waheshimiwa Wabunge walizionyesha kwamba Benki ya Kilimo ina mtaji mdogo ikilinganishwa na mahitaji na kwahiyo, Serikali iliombwa iweke utaratibu mzuri kwa ajili ya kuhakikisha kwamba benki hii inapata unafuu wa kuweza kuhudumia wakulima nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika hotuba yangu, Serikali ilizindua Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili kuwawezesha wakulima kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuendeleza na kukuza shughuli za kilimo nchini. Kitaalam kilimo ni pamoja na shughuli za kilimo cha mazao, uvuvi, mifugo na maliasili, hivyo naamini kuwa hata wavuvi na wafugaji waliopo katika Jiji la Dar es Salaam, wanastahili kutumia huduma za mikopo kutoka benki hii.
Kwa mara nyingine tena niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa ujumla kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo ili kuongezea benki hii mtaji wake; lakini bado Serikali pia imeongeza benki nyingine inaitwa TIB Maendeleo na TIB Ushirika (TID Development na TIB Corporate). Zote hizi nazo tumeziongeza kwenye mifumo ya mikopo kwa ajili ya kilimo. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wakulima wote nchini, tunayo fursa kubwa sasa kukopa kwenye Benki ya Kilimo, lakini pia na TID Development na TIB Corporate ili kuweza kuongeza mtaji wa shughuli za kilimo.
Kulikuwa na suala la hifadhi ya jamii nalo pia ni jambo ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi walichangia. Kwenye eneo hili Wabunge waliomba Sera ya Uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na kupunguza idadi ya mifuko hiyo iweze kuangaliwa tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetoa miongozo ya uwekezaji iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi ya Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, kaguzi za mara kwa mara zinafanyika kuhusu uwekezaji wa mifuko hii ya jamii. Sambamba na hatua hizo, Serikali imekwishatoa maelekezo kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuona namna itakavyoshiriki katika sekta ya viwanda ili kuchangia katika uchumi wa viwanda, kuongeza fursa za ajira na hatimaye kujipatia wanachama wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kupunguza idadi ya mifuko ya hifadhi ya jamii, ushauri uliotolewa umepokewa na ni mzuri na tayari Serikali inakamilisha utafiti wa kina kuhusu hali ya mifuko na namna ya kupunguza idadi ya mifuko iliyopo. Kwa sasa hatua inayoendelea ni kupokea maoni ya wadau ili kuwezesha mabadiliko husika kufanyika kwa wakati muafaka. Napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba mawazo yenu tutaendelea kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ilikuwa ni mchakato wa kura za maoni na Katiba Iliyopendekezwa. Ilitakiwa Serikali itoe tamko kuhusu maandalizi ya utekelezaji wa mchakato wa kura za maoni katika Katiba Iliyopendekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013 mchakato wa kura za maoni kuhusu Katiba Iliyopendekezwa unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa Tanzania Bara na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa upande wa Tanzania Zanzibar. Zoezi hilo lilipangwa kufanyika tarehe 30 Aprili, 2015 lakini likaahirishwa kwa sababu zifuatazo:-
Moja, kutokamilika kwa zoezi la kuandikisha wapigakura wakati muda wa kura ya maoni ukiwa umekaribia.
Pili, mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa ni sawasawa na mchakato wa uchaguzi, kwahiyo, Tume zisingeweza kuendesha kura ya maoni pamoja na Uchaguzi Mkuu kwa pamoja. Hivyo njia pekee ilikuwa ni kuahirisha kura ya maoni ili ikuendesha uchaguzi wa mwaka 2015 kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia haya, kwa kuwa Tume hizi mbili ndizo zilizoahirisha mchakato huo kwa sababu zilizoelezwa na pia ndizo zenye dhamana ya kuendesha zoezi hilo, napenda kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kuwa taarifa na ratiba mpya ya kura za maoni zitatolewa na Tume hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya ratiba ya uchaguzi iliyotakiwa Serikali iweke utaratibu mpya wa ratiba ya upigaji kura ili kuwezesha chaguzi zote za Rais, Wabunge, Madiwani na Serikali za Mitaa zifanyike kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nieleze tu kwamba uendeshaji wa usimamizi wa Uchaguzi Mkuu ambapo Rais, Wabunge na Madiwani ndio unawahusu na uchaguzi wa Serikali za Mitaa unasimamiwa na kuratibiwa na kuendeshwa kwa sheria na mamlaka mbili tofauti kama ifuatavyo:-
Moja, uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unasimamiwa na sheria mbili ambazo ni Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292 na uchaguzi huo husimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unasimamiwa na sheria mbili ambazo ni Sheria ya Mitaa, Mamlaka ya Wilaya Sura Namba 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka za Miji Sura Namba 288. Uchaguzi huu usimamiwe na Wizara yenye dhamana na masuala ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huo uliwekwa ili kutowachanganya wananchi katika upigaji kura, kwani kwa kufanya chaguzi hizo zote kuwa pamoja, zingeweza kusababisha karatasi za kura kuwa na picha rundo au nyingi kiasi kwamba mpigakura angeshindwa kuweza kutambua kwa haraka. Pamoja na maelezo haya, Serikali imepokea mapendekezo na nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaendelea kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na suala la uhakiki wa majina ya wapigakura ya kwamba Serikali iongeze muda wa uhakiki wa majina kabla ya kupiga kura ili kuwawezesha wananchi wengi waweze kupiga kura.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekamilisha zoezi la tathmini baada ya uchaguzi (post-election evaluation) na inakamilisha uchambuzi wa tathmini hiyo na matokeo ya tathimini hiyo yatawezesha kuboresha maeneo mbalimbali likiwemo suala la uwekaji wazi daftari la kudumu la wapiga kura.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na utafiti wa wananchi ambao hawakupiga kura nalo pia lilijitokeza na Waheshimiwa Wabunge walichangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria za Uchaguzi; kujiandikisha na kupiga kura ni haki na hiyari ya mwananchi. Hata hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi imefanya tathmini za uchaguzi, pamoja na mambo mengine na kubaini sababu za baadhi ya maeneo wananchi kujitokeza wachache kupiga kura. Uchambuzi wa taarifa hiyo utakapokamilika, Tume itabainisha sababu ya baadhi ya wananchi kutokujitokeza kupiga kura pamoja na mapendekezo ya hatua za kuchukua ili wananchi wengi waweze kujitokeza kwenye chaguzi zijazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na mchango wa Waheshimiwa Wabunge juu ya vigezo vya kugawanya Majimbo ya Uchaguzi. Eneo hili ni kwamba vigezo vinavyotumika kugawa majimbo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ni pamoja na wastani wa idadi ya watu, hali ya kiuchumi, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, hali ya kijiografia, upatikanaji wa mawasiliano, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, lakini mazingira ya muungano wenyewe, uwezo wa ukumbi wa Bunge na idadi ya Viti Maalum vya Wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2015 Tume ilipokea maombi 77 ya kuanzishwa au kagawa majimbo ambapo Halmashauri 37 ziliwasilisha maombi ya kugawa majimbo ya uchaguzi na maombi 40 yalitoka katika Majimbo yakiomba kugawanywa. Kati ya maombi yaliyowasilishwa, maombi 35 yalikidhi vigezo na yalistahili kugawanywa.
Hata hivyo, kutokana na ongezeko la Halmashauri mpya ambazo kisheria ni majimbo ya uchaguzi, ongezeko la idadi ya Wabunge wanawake na Viti Maalum na uwezo wa ukumbi wa Bunge, Tume iliamua kutumia vigezo vitatu ili kupata idadi ya majimbo yanayoweza kugawanywa. Vigezo hivyo ni hivi hapa wastani wa idadi ya watu, mipaka ya kiutawala na uwezo wa ukumbi wetu wa Bunge kwa kutumia vigezo hivyo vitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ilianzisha Majimbo 25 kwa mchanganuo ufuatao; majimbo 19 yalitokana na ongezeko la Halmashauri mpya na majimbo sita yalitokana na kigezo cha wastani wa idadi ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia pia maombi ya kugawa majimbo katika Wilaya ya Chemba na Sumbawanga, natarajia kwamba kwa kuzingatia vigezo vilivyotajwa hapo juu, Tume itaangalia uwezekano wa kugawa majimbo hayo iwapo yanakidhi vigezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa sasa hatutaweza kutamka maeneo mapya ya utawala, hii ikiwemo na maombi ya Wilaya, Halmashauri hata Mikoa. Hii ni kutokana na mamlaka zile mpya ambazo tumezipa maeneo mapya bado hatujakamilisha kuzijenga na kuzipa uwezo wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwenye maeneo mapya. Baada ya kuridhika kwamba tumeshakamilisha hayo, tutawapa taarifa na jambo hili tutaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na jambo la miradi ya REA kutaka miradi ya usambazaji umeme vijijini ikamilishwe na leo nimefurahi nimemsikia Naibu Waziri hapa akitoa ufafanuzi. Kwa ufafanuzi ule, niwahakikishie tu kwamba vile vijiji vyote ambavyo vilishaingia kwenye Mpango wa REA, kazi hizo zinaendelea, lakini Awamu ya Tatu Itakapoanza vijiji vyote vilivyobaki tunatarajia vitaingia kwenye mpango ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakamilisha. Malengo yetu vijiji vyetu nchini vipate umeme na wananchi wetu wote wapate umeme wa kutosha kwenye maeneo yao. Uwezo huo tunao na tunawaahidi kwamba Serikali itakamilisha jambo hili kwenye maeneo yetu kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la uwezeshaji wananchi vijijini ambapo pia ilitakiwa Serikali iweke utaratibu wa vigezo vitakavyozingatiwa kwa wananchi kabla ya kutoa Shilingi milioni 50 zile ambazo zinaenda vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili, niseme tu kwamba mradi unalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutenga shilingi milioni 50 kwa kila kijiji kama Mfuko wa uwezeshaji kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia Ushirika wa Kuweka na Kukopa katika vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi bilioni 59 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo. Ili kuwapatia mikopo wakopaji, masharti yafuatayo yatatumika katika kutekeleza mpango huu. (Makofi)
Moja, ni kikundi cha kifedha kiwe kimesajiliwa na Halmashauri na Tume ya Ushirika; pili, kikundi kiwe na Katiba, uongozi uliochaguliwa kidemokrasia na kupata mafunzo ya mikopo; tatu, kikundi kiwe chini ya asasi ya kiraia inayotambulika na yenye uzoefu wa shughuli za mikopo; nne kikundi kionyeshe uzoefu wa kukopeshana kwa muda wa mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa historia ya urejeshaji wa mikopo hiyo kwa asilimia kuanzia 95.
Pia dhamana ya Serikali itakuwa kwenye kiasi cha msingi cha mkopo na siyo kwenye kiasi ambacho kimechanganywa na riba. Sita, kikundi kitaweka amana akiba ya fedha benki katika akaunti maalum; asilimia 10 ya mkopo ndani ya kikundi, hautazidisha riba zaidi ya asilimia 11, lakini mkopo wa SACCOS itafuata Kanuni ya Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013. Kwa hiyo, ni vyema sasa Waheshimiwa Wabunge tukaendelea kuhamasisha kwenye maeneo yetu ili vikundi mbalimbali vianze kusajiliwa na viweze kuingia kwenye utaratibu huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ilikuwa ni suala la CDA kutokuwa na Sheria ya Makau Makuu, hili limejibiwa vizuri na Waziri, Mheshimiwa Jenista Mhagama kwamba sheria imekamilika, bado taratibu zinaendelea ili kuweza kuifanya CDA sasa kuwa kwenye sheria iliyo kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo lilichangiwa ni suala la uchakavu wa meli ya MV Serengeti ya Ziwa Victoria; Waheshimiwa Wabunge hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Nataka niwahakikishie, hata nilipokuwa Mkoani Kagera niliwahakikishia wananchi kwenye mkutano wa hadhara kwamba ahadi hii ya kupata meli mpya itatekelezwa, itakayoweza kufanya safati zake kwenye Ziwa Victoria. Kwa hiyo, wananchi waendelee kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho tunaendela kuomba bajeti hapa. Na mimi nawaomba Waheshimiwa Wabunge tupitishe hii bajeti ili tuendelee kufanya kazi za Serikali ikiwemo na ahadi ambazo Mheshimiwa Rais ameahidi katika maeneo mbalimbali nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo lilikuwa limehitaji mchango lakini na majibu, ni uwepo wa Makau Makuu wa Wilaya ya Nyang‟hwale, ambapo sasa kumetokea na mkanganyiko kule. Nataka niwahakikishie Wana-Nyang‟hwale wote kwamba bado Serikali inatambua kuwa Makao Makuu ya Wilaya ni Karumwa, ambayo ilipendekezwa na ninyi wenyewe na sisi wajibu wetu sasa ni kuanda certificate au cheti kwa ajili ya kuthibitisha uwepo wa Makao Makuu hayo.
Kwa hiyo, sasa nawasihi wananchi kupitia pia Mheshimiwa Mbunge ambaye ataonana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kupata hicho cheti muweze kuendelea na shughuli za maendeleo kwenye Wilaya yenu ya Nyang‟hwale ikiwa chini ya Makao Makuu pale Karumwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ambazo zilikuwa mezani kwangu siyo nyingi na hivyo naomba nihitimishe hoja hizi kwa hayo yafuatayo kwamba, kama nilivyosema hapo awali kwamba muda hautoshi kujibu hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, hata hivyo nirudie kusema kuwa Serikali yetu inayoongozwa na chama cha Mapinduzi, imejipanga vizuri sana katika kila sekta hasa za kiuchumi na kijamii, kuhakikisha kwamba wananchi wake wanajiletea maendeleo yao na Serikali hii itasimamia maendeleo hayo na maeneo ambayo yamekosa fursa, tutahakikisha kwamba tunapeleka fursa hizo ili wananchi waweze kwenda sambamba na hizo fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona juhudi kubwa za Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha tunakuwa na mapato ya kutosha kutuwezesha kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi na hususan katika sekta ya kilimo, miundombinu, elimu, afya, nishati na madini. Wito wangu bado unabaki pale pale kwa watendaji wa Serikali walioko kwenye maeneo haya kutoa huduma kwa wananchi ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanatarajia Serikali hii kuwa itawapokea, itawasikiliza na kuwahudumia na jukumu hili Serikali imewapa watumishi wa Serikali ili waweze kutenda hayo kwa wananchi, wananchi waone kabisa wapo kwenye nchi yao na kwamba inawajali na inaweza kuwaletea mafanikio. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kupitia maombi yangu ya leo kwenu Waheshimiwa Wabunge ya fedha za maendeleo ambazo tunatarajia tuzipeleke kwenye maeneo yetu, tulikuwa na tatizo la upitishaji wa mikataba ya thamani ya mikataba yenyewe kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitumie nafasi hii sasa kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa kwa sasa Serikali imefanya mapitio na hasa kupitia Gazeti la Serikali Toleo Namba 121 la tarehe 24/4/2016 imepandisha kiwango cha thamani za mikataba inayopaswa kupitiwa au kuhakikiwa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutoka shilingi milioni 50 ya awali hadi shilingi bilioni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapitio ya mikataba hii ya shilingi milioni 50 imekuwa ikileta matatizo makubwa kwenye Halmashauri. Mradi mdogo wa shilingi milioni 50, mkataba uende kwa Mwanasheria Mkuu. Tumegundua kuna mrundikano mkubwa wa mikataba hii pale kwa Mwanasheria Mkuu. Sasa Serikali imefanya marekebisho, mikataba ya kwenye Halmashauri itakayotakiwa kwenda kwa Mwanasheria Mkuu ni kuanzia shilingi bilioni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo basi, mikataba yote yenye thamani ya chini ya shilingi bilioni moja itahakikiwa na mamlaka yenyewe ya Halmashauri au taasisi husika kwa ajili ya manunuzi. Hatua hii itaharakisha kasi ya manunuzi na hivyo kasi ya maendeleo pia katika Halmashauri inaweza kufikiwa kwa haraka. Hata hivyo, Mamlaka za Ununuzi hazizuiliwi kuomba ushauri kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mikataba ya kiwango cha chini ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujiridhisha tu kwamba walichofanya ndicho chenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watakaokuwa wanahakiki mikataba hiyo katika Mamlaka za Ununuzi (procure re-entities) watapaswa kuzingatia Sheria ya Ununuzi na sheria nyinginezo zinazohusu mikataba hiyo na maadili ya Wanasheria lazima yazingatiwe katika utumishi wa umma ili kulinda maadili sahihi ya namna ya upitishaji wa mikataba hii. Kinyume cha hapo, kama maadili hayataweza kutekelezwa, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wale watendaji wetu kwenye Halmashauri zote, pale ambapo mikataba hiyo itapitiwa na pia itaweza kupindishwa kwa mujibu wa taratibu hizi za Serikali zinavyotaka hatua kali itachukuliwa na hatutasita kuchukua hatua kwa wale wote ambao hawawezi kufanya hivyo. (Makofi)
Mwisho, narudia tena kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, kwamba tumeshirikiana katika siku hizi zote hapa tukiwa tunachangia hoja mbalimbali kutoa maoni ya utendaji bora wa mwaka wa fedha ujao kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na mimi pamoja na Mawaziri wangu, Makatibu Wakuu wangu, Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi pamoja na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Kwa kuwa pia niliomba na nilieleza pia utendaji wa Serikali kwenye Wizara nyingine zote, nataka niwahakikishie, bajeti hizi zinazoletwa kwenu ambazo naamini mtaziridhia kuzipitisha ili tuanze kazi tarehe 1 Julai, tutasimamia maadili, tutasimamia uaminifu, tutasimamia uwezo mzuri wa kitaalamu katika utendaji wa kazi za kila siku ili Watanzania waweze kupata tija ndani ya nchi yao. Na ninyi kama Wabunge mtatusaidia sana kuona mwenendo wa utendaji wa Serikali kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu kwamba tutaendelea kushirikiana kwa pamoja, tutafanya hivyo bila kujali vyama vyetu, tutafanya hivyo kwa kujali maslahi ya Watanzania wote na tuendelee kushirikiana kwa pamoja, na mimi kama Msimamizi Mkuu wa Shughuli za Serikali nitashirikiana nanyi kuhakikisha kwamba miradi yetu inafikiwa kwa kiwango kinachostahili. (Makofi)
Sasa basi nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa ujumla, tushirikiane kuivusha nchi yetu katika hatua tuliyonayo kiuchumi, tunahitaji kusonga mbele, kwani wananchi wetu wanahitaji maendeleo, na sisi ndio wenye jukumu la kuwaongoza wananchi wetu kufikia malengo tuliyoyatarajia. Naomba sana, nitakapokuja kuwaomba fedha mridhie ili tuanze kazi ile mnayotarajia tuifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ndio ilikuwa kauli yangu ya msingi ya mwisho kwa Wabunge wenzangu ili tuweze kuungana kwa pamoja na sasa naomba kutoa hoja.