Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Rev. Dr. Getrude Pangalile Rwakatare

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

HE. DKT. GETRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu. Namshukuru Jehova Mungu wa Mbinguni, Elishadai, mwenye uwezo wa kunirudisha tena Bungeni. Namshukuru kwa afya na uzima, wote tumeweza kufika salama na kulinda familia zetu, Mungu wetu ni mwema. Bwana asifiwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda nimshukuru Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniona, kunikumbuka na kuniteua kuwa Mbunge wa Viti Maalum katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mungu ambariki sana, sana, sana na Mungu amlinde. Namwahidi nitamwombea, Mungu ampe afya njema, Mungu aweze kumpa uongozi bora na kuwe na amani na utulivu kabisa siku zote za uongozi wake. Mungu ampe maisha marefu, aishi akiona vijukuu hadi vitukuu kwa utukufu wa Bwana. Kwa kweli ni mwema, ni mwaminifu; kwa kweli ni mchapakazi, ni jembe; ni komandoo na anaweza. Ahadi yangu kwake sitamwangusha, nitaendelea kumwombea siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena niwashukuru wanawake wote wa UWT Tanzania nzima kwa maombi, kwa simu zao za kunitia moyo na kunipongeza. Naahidi pia kwamba nitafanya kazi na UWT kwa uwezo wangu wote. Wanawake, kaeni mkao wa kula, nakuja tufanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kushukuru Kanisa langu la Mlima wa Moto, Mikocheni ‘B’, Assemblies of God kwa maombi yao; nikianza na Wachungaji, Wazee wa Kanisa na Washirika wote. Ahsanteni kwa maombi yenu. Nashukuru. (Makofi)

Mungu wetu ni mwema.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuishukuru familia yangu. Mama yangu mzazi, familia yangu, kaka zangu, dada zangu na watoto wangu wote. Ahsante kwa kunivumilia na kunitia moyo. Mungu awabariki. (Makofi)

Pia naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu na pia Watanzania wote, kwa msiba mkubwa tulioupata kwa kupotelewa na watoto wetu kwa ajili ya basi huko Karatu. Mungu aziweke roho zao mahali pema, peponi.

Nawaombea wazazi wao faraja, nawaombea Mungu awape amani, wakubali yote kwa sababu kazi ya Mungu haina makosa. Bwana alitupa na Bwana ameatwaa, jina la Bwana libarikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii niweze kuchangia katika hotuba hii nzuri ya Wizara ya Viwanda Biashara…

WABUNGE FULANI: Waliongea bila kutumia vipaza sauti.

MHE. DKT. GETRUDE P. LWAKATARE: Eeh, jamani, mimi Mchungaji, msinitanie! (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii niweze kuchangia katika hotuba hii nzuri ya Wizara ya Viwanda Biashara nikianza kumpongeza kwanza kabisa Waziri, Mheshimiwa Mwijage, shemeji yangu. Anafanya kazi nzuri kwa kweli. Kazi imepata mtu! Siyo mtu amepata cheo, lakini ukweli cheo kimepata mtu sahihi. Anafanya kazi nzuri, tunafurahi na timu yake yote. Yaani kama uhamasishaji, ameufanya, tumeona wawekezaji wakiingia na kutoka Tanzania; tumeona kwamba viwanda vingi vimefunguliwa na hata hivyo tunaona pia juhudi yake, bado anajitahidi. Hata kama watu wakitupa madongo, nasema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Jamani, mtoto wa Kihaya anafanya kazi nzuri, tumshukuru. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumtia moyo Mtumishi wa Mungu Mheshimiwa Mwijage pamoja na timu yake ya kwamba aendelee mbele, azibe pamba masikio; mema ayachukue, lakini yale ambayo ni ya kukatisha tamaa ayaache. Abantu baabi! Wahaya wanasema: “watu wote siyo wema, wengine wabaya.” Kwa hiyo, jipe moyo, songa mbele.”

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa asilia inajulikana kwamba watu wengi humshukuru na kumsifu mtu akifa. Siku ya tanzia ndiyo wanasema ooh, alikuwa hivi, alikuwa hivi. Kwa hiyo, usijali, songa mbele. Rome was not built in a day, you have tried. Umejaribu ulivyoweza. Lazima tuanze kidogo, polepole tutapanda, huwezi kuamini, pengine baada ya miaka mitano Tanzania ndiyo itaongoza kwa viwanda vingi kuliko kote East Africa nzima. Kwa dira hii tunayoiona tumeridhika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe ushauri kwa sababu kwa kweli kazi ni nzuri sana na mwanga tunauona. Ushauri wangu wa kwanza, ni punguzo la kodi. Jamani kodi Mheshimiwa Waziri ungekaa na Waziri wa Fedha mkaangalia ni jinsi gani mnaweza kutoa incentive ya kutosha kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na hata wa nje. Yaani kodi ni kikwazo, kwa sababu kwa kweli ukihesabu, kodi ni nyingi mno. Zinakatisha tamaa, hata mwisho ukijaribu kujumlisha unakuta kwamba faida ni ndogo sana. Inakatisha tamaa wawekezaji na wengine wanafunga kabisa viwanda au wanafunga kabisa biashara zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya Viwanda inawezekana, lakini pia tuangalie hao wanaowekeza; wanakopa, wana madeni na wana mambo mbalimbali. Kwa hiyo, lazima tuangalie na sisi kama Serikali tuone tunawasaidiaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ushauri wangu mwingine, nasema pia ili kuwa na Tanzania ya viwanda, ni lazima kuwe na umeme wa uhakika. Umeme wetu kwa kweli siyo wa uhakika. Kama mnavyoona, mara nyingi unakatika na pia tozo inakuwa kubwa mno. Hasa ukiwa na kiwanda, ndiyo kabisa, yaani jiandae kulipa mamilioni. Hata kama unatumia diesel, vile vile hata diesel ni bei. (Makofi)

Kwa hiyo, unakuta kwamba mwenye kiwanda anakata tamaa, maana yake faida ni ndogo mno. Kama kweli tungekuwa nao bega kwa bega kwa kuwasaidia pamoja na kuhamasisha kuja kuwekeza Tanzania, pia tuwasaidie na wao waweze kupata faida ili walipe madeni yale ambayo wamekopa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.