Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Mheshimiwa Mwijage ni kaka yangu na mara nyingi tumekuwa tukiwasiliana na leo nataka nimkumbushe tu mambo machache ambayo tungependa Mheshimiwa Rais lakini pamoja na Taifa liyafahamu. Kwanza kabisa nimfahamishe kwamba mwaka wa jana wakati fulani Mheshimiwa Waitara alichangia akimtaka CAG kwenda kufanya ukaguzi maalum Chuo cha Elimu ya Biashara, Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, CAG amekwenda kukagua amekiri lakini bahati mbaya sana ukaguzi huu umefanyika Chuo cha Dodoma pamoja na Chuo cha Mwanza, Dar es Salaam ambako ndiko kwenye upotevu wa zaidi wa Sh.400,000,000 ukaguzi haujafanyika. Taarifa za CAG ni hizi hapa, naomba apatiwe copy.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri mambo machache. Tunatamani sana kuwa na viwanda Tanzania, lakini Sera yetu bado haijabadilika. Ukiangalia kimtazamo, wawekezaji wengi wanashindwa kuja Tanzania kwa sababu ya kodi. Kodi nyingi zinatozwa kabla mtu hajawekeza hata kitu kimoja; atakutana na watu wa ardhi, watataka pesa kutoka kwake, atakutana na watu wa NEMC, atataka pesa kutoka kwake. Sasa tunawavutiaje wawekezaji kama vyanzo au vivutio vya uwekezaji ni vichache au vilivyokuwa na misongo misongo? Kwa hiyo, tuangalie namna bora ya kufanya, NEMC pamoja na watu wa ardhi waone namna ya kutoza kodi ikiwezekana baada ya mtu kuwekeza katika mazingira fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nataka nimkumbushe lakini pia tumsaidie Mheshimiwa Waziri kumkumbusha Mheshimiwa Rais; alipokuja Mtwara wakati anaomba kura, alisema atahakikisha viwanda vya korosho vinafanya kazi. Sasa hivi tuna mwaka mmoja takriban na nusu viwanda vile havijaanza kufanya kazi na hatujaona juhudi zozote zinafanyika angalau kuwatafuta wale watu ambao walipewa viwanda na Serikali ili waviendeleze. Vile viwanda sasa vimegeuka kuwa maghala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tafiti mbalimbali zimefanyika ambazo zinaonesha kabisa kwa kutumia tu korosho iliyoko Mtwara sisi tunaweza tusiwe watu tunaohitaji viwanda vingine vyovyote. Korosho yetu ina uwezo wa kututoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina hii paper hapa mbele yangu inasema; justification for cashew value addition in Tanzania. Hii karatasi nitaileta kwako lakini ina mambo mengi sana humu ndani ikiwa ni pamoja na kuonesha faida mbalimbali zinazoweza kupatikana baada ya kuwa na kiwanda cha korosho; kwa sababu unapozalisha korosho zile cashewnut kernels, zile korosho za ndani ni asilimia 25 ndiyo ambayo inatumika na inasafirishwa kwenda nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule inakokwenda wanapata maganda ya korosho ambayo ni asilimia 50 – 60 na saa zingine inafikia 70 – 80 ya maganda ya korosho. Sasa faida za maganda ya korosho. Sasa, faida ya kwanza kabisa maganda yanaweza yakatumika kutengeneza break lining kwa ajili ya magari. Maganda ya korosho yanaweza yakatumika kutengeneza vilainishi vinavyotumika kwenye nchi zenye joto kali, maganda ya korosho yanaweza yakatumika kutengeneza vipodozi (cosmetics). Nadhani ukiangalia watu wa Mtwara wengi utaona wamejichora alama fulani za korosho, maana yake kwamba inaweza kubadilisha ngozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tukiangalia maganda haya haya ya korosho (sina hakika sana) lakini ilikuwa inasadikika Mheshimiwa Rais alifanya research yake kwa kutumia maganda ya korosho akisema kwamba maganda ya korosho ni dawa nzuri sana ya kuua vidudu kuliko hizi dawa mnazoziingiza kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia maganda ya korosho yanaweza kutengeneza ceiling board. Sasa niombe Wizara wafufue viwanda vilivyoko Mtwara; hii sehemu waliyoitaja ndiyo inayoingiza pesa nyingi kwenye korosho kuliko hizi korosho chache wanazozitegemea ambazo ni asilimia 20 – 25. Kwa hiyo, waone namna watakavyofanya kuhakikisha viwanda vile vya korosho Mtwara vinafufuliwa kwa ajili ya kuongezea pesa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa yako tu mwaka huu Tanzania au korosho ya Tanzania ndiyo limekuwa zao la kwanza lililoingizia mapato makubwa Taifa hili. Sasa tuone hicho tunachokipata ni asilimia 25 tu ya hali halisi. Tulete viwanda, tuwatafute wawekezaji waje kuwekeza ili waweze kuzalisha tupate hivi vitu vingine. Hizo break lining zinazotoka India, China nyingine zinatengenezwa kwa kutumia maganda ya korosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Tanzania miaka ya 60 na 70 tulikuwa na viwanda vya kutosha tu maeneo ya Mtwara, Lindi, Ruvuma pamoja na Pwani, bahati mbaya vile viwanda viliuzwa na watu wanavifanya maghala. Sasa tunaamua kuondoa korosho zetu tunaziuza tunapeleka nchi za nje. Kule wenzetu wanakwenda kutengeneza hivi vitu ambavyo wanarudisha kwetu kuviuza. Faida ya korosho si kwenye ubanguaji ni mazao yanayotokana na ile korosho baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwongezee Mheshimiwa Waziri kitu kingine ambacho Watanzania wengi hawakifahamu na Mheshimiwa Waziri naomba achukue hili very serious. Kuna pombe inazalishwa kutokana na mazao ya korosho (bibo), ile pombe jina lake halisi inaitwa nipa. Watanzania walio wengi wanatumia hii pombe, inafahamika kwa majina mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Sheria hii inaitwa Intoxication Liquors Act 1968, ilitambua pombe mbalimbali za kienyeji katika maeneo yao. Sasa sisi kule kwetu tunatengneneza pombe inaitwa nipa kama nilivyoeleza, lakini inatambulika kama pombe ya Moshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tafsiri yake inasema hivi – Moshi means the distilled liquor commonly known as Moshi, Kitaifa, lakini pia watu wa Mtwara pamoja na Lindi tunaita nipa or piwa – watu wa Moshi. Sasa nimwombe; hii haijawahi kuharamishwa hata siku moja na hakuna Sheria yoyote iliyobadilishwa na kuharamisha hii pombe ya nipa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naongea hivyo kwa sababu kuna faida kubwa inayopatikana kwenye mabibo. Kwa mfano tu mwaka huu mabibo zaidi ya tani milioni moja na laki tatu yamezalishwa, lakini yametumika kiasi kidogo sana, watu wanakula wanatupa. Sasa tukiamua kuchukua hatua tukaenda mbele, tunaweza kupata wine, tunaweza kupata pale ndani hizo whisky na vitu vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, hii nipa ikiwa distilled, kwa sababu jukumu la Mheshimiwa Waziri kadri ya Sheria iliyoko hapa mbele ni wewe unatakiwa kutoa leseni kwa wapika nipa, si wapika gongo, wanaopika nipa inayotokana na mazao ya shambani; kama ambavyo iko kwa watu wanaopika nipa hiyo hiyo jina lingine tuseme Moshi wanaita piwa wanawauzia kiwanda cha K-Vant wanatoa pale ndani spirit. Ile spirit inatumika hospitalini kwa shughuli mbalimbali. Kwa hiyo inakuwa distilled vizuri, inakwenda kutumika vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kule kwetu tunatambua, watu wengi wanafahamu, sisi tunauza ile nipa kwa chupa moja ya fanta Sh.500, ile chupa ya bia Sh.1,000. Wakiamua sasa kuigeuza ikawa zao la biashara wananchi wakapewa leseni, wataipika vizuri si mafichoni kule ambako inatoka ikiwa chafu kwa sababu hawatumii vifaa vizuri. Itakapokuja hapa mbele itapata bei nzuri, hawatakunywa wale watu, hawataweza kununua, lakini itakwenda kutumika kuongeza na kukuza kipato cha wakulima. Pia wakati huo huo itasaidia kwenye hospitali zetu, sisi tunafanya importation ya spirit kutoka maeneo mbalimbali, spirit hii inapatikana kwenye nipa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria hizi hapa. Mara ya kwanza kabisa lilijadiliwa jambo hilo la ilisainiwa hii hapa na marehemu Mheshimiwa Mzee Kawawa. Mara ya pili imejadiliwa tena hii Imesaini na wakati huo Katibu wa hili Bunge ambaye alikuwa Mzee Msekwa. Baadaye Mheshimiwa hayati Nyerere Baba wa Taifa naye alisaini, hawakuharamisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilipoanza kuharamishwa hii ni pale ambapo mlianza kuiita, kuna jina waliita wataalam, unajua wanasema ukitaka kumpiga mbwa, mpe jina baya. Wakaanza kuita inaitwa illegal illicit alcohol, hii sasa ndiyo gongo. Hata hivyo, sisi kwetu hatutengenezi gongo, tunatengeneza nipa pure, inatokana na mazao ya shambani. Tuwaruhusu wale watu wajiongezee kipato, kwa sababu ni kweli inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwijage akija kule nyumbani hata mimi nitamtafutia kichupa kidogo cha nipa aonje ladha yake ambayo inafanana na whisky, hizi tunazo import kutoka nchi mbalimbali, tunazileta Tanzania tunazitoza kodi wakati tunapoteza mapato kule kwa wakulima, lakini pia pamoja na kuwaongezea kipato wakulima wetu. Kwa hiyo, kuna hii research nimeweka hapa kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo hilo bibo ni zuri zaidi kuliko ilivyokuwa pamoja na hizi citrus fruits, ina vitamin c mara tano zaidi. Sasa kwa nini tusiache wale wananchi wakajipatia kipato kutokana na hivi vitu? Sheria iko wazi, ikiwezekana Mheshimiwa akija hapa awaombe radhi Watanzania waliofungwa kwa kutumia mazao yao ya shambani kutengeneza pombe ambayo inaitwa haramu wakati pombe hiyo haijawahi kuharamishwa, ni sehemu ya kuongezea kipato wakulima. Kwa hiyo, naona unamwonesha Mheshimiwa Mwigulu hapo awataarifu polisi wake, lakini na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda ana jukumu la kutoa leseni kwa watengenezaji wadogo wadogo ili waweze kufanya vizuri, wakauzie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti umekamilika Chuo cha Kilimo Naliendele, wanasubiri tu sasa kununua hivi vitu kutoka kwa wakulima wa korosho. Bei ya korosho inaweza ikashuka muda wowote na faida ya korosho inapatikana kwenye mazao mbadala. Mwaka huu tumefanikiwa kuuza mpaka Sh.4,000 lakini niseme tukiamua sasa kuwaachia wakulima wakawa huru wakafanya jambo hili kwa Mheshimiwa Waziri kuwapa leseni, kilo moja ya korosho na mazao yake wanaweza kupata mpaka Sh.6,000 au 7,000 na haitashuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nia yangu hasa ni kuonesha economic importance of cashewnuts na chain nzima ya korosho. Naomba Mheshimiwa Waziri alichukulie hili very serious na nitakwenda ofisini tuweze kulijadili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga hoja ya Upinzani.