Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Mwanne Ismail Mchemba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, amefanya kazi kubwa ya mfano. Nijenge hoja ya kumpongeza, maana yake wengine watasema kwa nini wanapongezana; mimi nampongeza Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana kwa mwaka huu kwa Mkoa wa Tabora; amefanya mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ameamua kupeleka maji katika Mkoa wa Tabora kutoka lake Victoria, hiyo pongezi ya kwanza. La pili, ametengeneza barabara ambazo ziko kwenye mpango na ambazo zimekamilika tangu akiwa Waziri. Kubwa zaidi, amefanya kazi kubwa mno ya kuleta usafiri wa ndege katika Mkoa wa Tabora, hayo yote lazima nimpongeze. Si hilo tu, ameleta tena standard gauge ambayo itapita Tabora, mimi bado nitaendelea kumpongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutangaza viwanda na biashara kwa ajili ya kuondokana na umaskini kwenda kwenye lengo la uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba sasa niende kwenye hoja. Hoja yangu nzito kabisa nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri wa Viwanda kwamba mimi nilikuwa Mbunge mwaka 2000 mpaka 2010, hilo kwanza alielewe, kwa hiyo ninapochangia hapa kuzungumza haya ninayoyasema ayazingatie ayafuatilie.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, Kiwanda cha Manonga cha Usindikaji wa Mbegu za Pamba, kiwanda hiki kina historia yake, hawa wawekezaji wanambabaisha wanamtapeli, aende kwa kina, Rajan alikuwa mbabaishaji. Tumeanza kuzungumza kuhusu kukifufua kiwanda hiki ajenda ni ubabaishaji tu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, nakuheshimu; wakati anajibu swali la Dkt. Kafumu alisema yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, alisema hivi huyu mwekezaji inaonekana hana nia ya kuja kuwekeza au kukifufua kile kiwanda, sasa kigugumizi cha nini? Kwa nini asiamue akawapa Igembensabo ambao wapo na wanaweza kufanya kazi hiyo? Haya nayo yanachangia kuwafanya wananchi wa Tabora, vijana pamoja wakulima kurudi nyuma. Kwa hiyo, naomba hilo Mheshimiwa Waziri, mimi nitamfuata mpaka Ofisini kwake ili ajue uchungu wa wananchi wa Tabora. Maana alilijibu kama vile suala hili kama lipo lipo tu, lakini nimwombe alifuatilie kwa kina, lina uchungu sana na wananchi wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora kimepoteza ajira za vijana wa Mkoa wa Tabora wote na mikoa jirani kwa uzembe. Hivi hawa wawekezaji kwa nini mnawaogopa? Mpelekeeni Mheshimiwa Rais, atayatumbua haya ili angalau na sisi tuonekane katika nia ya Serikali ni kupeleka viwanda. Kiwanda cha Nyuzi cha Mkoa wa Tabora ambacho kiko Manispaa kina historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, alikuwepo Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Misigalo alishika shilingi katika jengo hili miaka ile. Kwa hiyo, alipolipeleka hilo wananchi wakaona anafaa bora aendelee akakaa vipindi viwili. Kwa matokeo hayo mpaka leo hakuna Mbunge anayekaa vipindi viwili kwa Mkoa wa Tabora kwa sababu hakuna wanachokiona tunachofanya. Sasa na mimi ili niweze kurudi tena lazima tupambane mimi na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mkoa wa Tabora kutokuleta wawekezaji ni makosa, tunazo fursa zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, Tabora inaongoza katika nchi hii kwa ulinaji wa asali, hilo nalo alizingatie na lazima niseme fursa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kwamba kuna nta ya kutosha, tumbaku ya kutosha, pamba ya kutosha, maembe ya kutosha pamoja na karanga za kutosha; na maeneo ya kuwaweka hao wawekezaji yapo na alishakiri mwenyewe, alikuwa anatuletea wawekezaji, lakini juzi wakati anajibu swali alisema hivi, aah wale wawekezaji tena hawapo. Hivi akisema hawapo kwa mtu wa chini kabisa kule inaonekana Serikali haitendi haki, kwingine wanapeleka wawekezaji, kwingine hawapeleki wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kiwanda cha nyama, mifugo ipo, zamani pale tulikuwa Kiwanda cha Maziwa, kwa hiyo ukileta Kiwanda cha Nyama kitahudumia Singida, Shinyanga, Mbeya na Kigoma, lazima watapita pale. Hata hivyo si hilo tu, Tabora iko kati; kwa nini nasema iko kati, ukiwatangazia wawekezaji ukasema Tabora kuna fursa zifuatazo, watauliza kuna nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema Tabora iko kati; ukiichukua Mbeya kuleta kutoka Zambia wapo pale watafika Tabora, ukitoka DRC lazima apite Tabora, ukitaka kwenda Burundi lazima apite Tabora, anapokwenda Rwanda lazima apite Tabora, anakwenda Uganda lazima apite Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, akiwekeza pale atakuwa na mfumuko wa kupata soko mpaka Afrika Kusini, kwa sababu hii ni center ambayo inafungua; kama anavyofanya Mheshimiwa Rais wetu anafungua barabara. Kwa hiyo hayo ndiyo nimesema nimfafanulie Mheshimiwa Waziri ili angalau aone uchungu tunaopata sisi Wanatabora na yeye aupate.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Tumbaku nilifikiri atakitaja leo humu, hakuna chochote alichokitaja ambacho nilimwomba mwaka 2016/2017, hakuna alichoweka humu. Leo ningepata majibu wala nisingechangia, sana sana ningefanya kumpongeza, anafanya kazi nzuri sana lakini si maeneo ya Tabora na Kigoma, majirani zangu wananiambia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine, hili ni la jumla, tuna tatizo sasa hivi la wawekezaji wa viwanda kuhusu sukari. Tuna tatizo la sukari tusijibu tu bla bla hapa; sukari sasa hivi ni tatizo kwa nchi nzima na kuna wenye viwanda ambao si waadilifu na si wazalendo. Sukari imekamatwa Kagera ambako anatoka Mheshimiwa Waziri, hivi imekamatwaje na imeuzwa na nani, ambayo ilikuwa inavuka wanaipaki kupeleka Kenya. Sasa hebu aniambie Tanzania tukoje?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, suala la sukari ajiulize kwa nini wanafanya vitu vya namna hii hususan unapoanza mwezi wa ramadhani? Maana ni keshokutwa tu, wanamchafua Rais wangu, hiyo ni hujuma ili wamsaliti lakini hawezi kusalitika, tunamuunga mkono hata yawe mapambano lakini sukari kwa nchi hii itapatikana na Mheshimiwa Waziri Mkuu alishasema. Kwa hiyo nimwombe afuatilie suala hili, nendeni kwenye ma- godown hawa watu mnawaogopa nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nimwombe, mikataba ya ubinafsishaji wale waliobinafsishiwa, waliopewa wale wa Kiwanda cha Nyuzi cha Manonga anipe majibu. Kwa nchi nzima viwanda vyote vile vije hapa, kwani kuna tatizo gani kuwanyang’anya? Mheshimiwa Lukuvi hapa ananyang’anya hati na kadhalika kwa nini Wizara ya Viwanda isifanye hivyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe, nimesema kwa hisia na uchungu kwamba nchi hii tusipopambana, nchi hii tusipoielekeza watamlaumu Waziri wa viwanda lakini utekelezaji wake utakuwa haupo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hawa watu awanyanga’anye hizo nanii zao kwani lazima?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.