Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri, pamoja na watendaji wake wote kwa matayarisho mazuri na ya kitaalam ya hotuba ya Wizara hii. Nawaombea Mungu awape uwezo na mashirikiano katika utendaji wa kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia hotuba hii naomba kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu ujenzi wa mabweni nchini. Napenda kupongeza Serikali yetu kwa juhudi kubwa inayofanya katika ujenzi na ukarabati wa mabweni. Juzi tumeshuhudia Mheshimwa Rais akizindua mabweni katika Chuo cha Dar es Salaam. Ushauri wangu katika suala hili ni kwamba mabweni yawe na miundombinu salama ili kuepuka madhara ambayo mara nyingi yamekuwa yakijitokeza. Pia mabweni yawe na milango zaidi ya mmoja ya kutoka na hata milango ya dharura. Vilevile mabweni yawe na vizimia moto ili kudhibiti madhara ya umeme unapoleta hitilafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu Chuo Kikuu cha Dodoma ni miongoni wa vyuo bora katika nchi yetu. Chuo hiki kina eneo kubwa na sekta nyingi lakini bado inaonekana kuwa wanafunzi wanaojiunga katika chuo hiki ni kidogo kutokana na ukubwa na uwezo wa chuo. Hii inatokana na mabweni ambayo hayaridhishi. Hivi sasa competition ya vyuo ni kubwa sana hapa nchini. Vyuo binafsi vinaonekana vina nafasi kubwa ya kupata wanafunzi wa kujiunga na vyuo vyao kuliko chuo chetu cha Dodoma kutokana na mabweni hafifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, aniambie ni asilimia ngapi ya wanafunzi waliojiunga mpaka kufikia mwaka huu kutokana na mahitaji ya chuo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni kuhusu Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam. Taasisi hii ni taasisi inayofanya kazi zake vizuri na kwa ubora sana. Tunaiomba Wizara izidi kuboresha ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi hii inajishughulisha pamoja na mambo mengine kutoa mafunzo katika ngazi tofauti kama vile ufundi sanifu na uhandisi. Namwomba Mheshimiwa Waziri atueleze sifa za kujiunga na mafunzo hayo ambayo hakuyaeleza katika hotuba yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.