Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuimarisha elimu na ushiriki wa wazazi na jamii. Wazazi na jamii kwa ujumla ni wadau muhimu sana katika kusimamia suala la upatikanaji wa elimu bora. Ni vizuri tuwape fursa ya kutoa michango yao ya kimawazo.

Vilevile wazazi na jamii wanatakiwa waelewe majukumu yao kwa ufasaha juu ya mchango wao kwenye elimu, kwa mfano kuchangia chakula shuleni, ujenzi na kadhaliaka. Wanafunzi wana haki zao za msingi wanapokuwa shuleni ikiwa ni pamoja na haki ya kulindwa, haki ya kupata elimu bora, kutobaguliwa na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naiomba Serikali ijenge mabweni katika shule. Hii itasaidia wanafunzi wa kike kutobakwa njiani wanapokuwa wanaenda shule. Wakati umefika Tanzania kuwa na bodi maalum ya kusimamia sera za elimu. Kuna baadhi ya wazazi wanawashawishi watoto wao wasifanye vizuri kwenye mitihani ili wa-fail wapate kuolewa au wanakuwa hawana uwezo wa kuwasomesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iongeze bajeti ili kuboresha elimu. Pia Serikali ihakikishe kwamba wanafunzi wanapata chakula bora shuleni. Hii inawapa vishawishi watoto kwenda shule na kuwa na akili kwa sababu wanakula chakula bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ijenge madarasa ya kutosha; lakini pia katika shule zetu kuna upungufu wa vyoo vya wanafunzi na baadhi ya shule kukosa walimu wa kike. Je, ni lini Serikali itaboresha na kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora katika Shule za Umma ambazo ndizo zinazowahudumia wanafunzi wengi katika Taifa hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya walimu wanaofundisha katika shule za pembezoni wanaishi katika mazingira magumu. Hawana miundombinu, hawana makazi mazuri kwa ajili ya kuishi na miundombinu ambayo siyo rafiki kwao. Kwa sasa fani ya ualimu siyo wito ni ajira kama ajira nyingine. Ni vizuri kuajiri walimu wenye sifa ya ualimu wenye weledi. Siyo ualimu kwa ajili ya mshahara. Vilevile kuna upungufu wa ofisi za walimu. Baadhi ya walimu kukosekana mafunzo shuleni (kazini) lakini pia kutopandishwa madaraja; walimu kutolipwa kwa wakati, stahiki zao, (walimu wanaohamishwa, kustaafu, pesa ya usafiri).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mikopo ya elimu ya juu (vyuo vikuu); Serikali inapaswa kutekeleza kwa vitendo mkataba wa utoaji nafasi sawa ya elimu kwa wote. Serikali inatakiwa kuhakikisha kuwa elimu inakuwa 6% ya pato la ndani. Tanzania haijaweze kufikia lengo hilo kwa miaka mitatu mfululizo ambapo bajeti yetu ya elimu ni 17%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba bajeti iongezeke ili kumudu gharama za udhamini wa wanafunzi wote nchini wenye sifa ya kudahiliwa katika vyuo vikuu. Kwa kuwa elimu ni haki ya msingi ya kikatiba ni vyema Serikali iache sera ya kibaguzi ya kuhusisha wazazi kuchangia elimu ya juu ambayo mpaka sasa imekuza tabaka la wasionacho na wenye nacho kwa ubashiri unaofanywa na Bodi ya Mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utambuzi wa wanafunzi wenye sifa ya kupata mikopo, kwa mfano; takwimu za mwaka 2015/2016 ni wanafunzi 21,500 ambayo ni asilimia 24 tu kati ya wanafunzi wote 88,000 wenye uhitaji wa mikopo walidhaminiwa mikopo. Wanafunzi asilimia 76 hawakudhaminiwa mikopo. Serikali inapaswa kutekeleza kwa vitendo utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu bila ubaguzi wowote, kwani kila mtu ana haki ya kupata mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile robo tatu ya wanafunzi wahitaji wanakosa mikopo na siyo kwa sababu hawana sifa ni kwa sababu ya usiri uliopo Bodi ya Mikopo. Naiomba Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kuweka utaratibu endelevu wa kukusanya fedha za mikopo kwa wanufaika waliodhaminiwa mikopo ili kuongeza wigo wa kuwadhamini wanafunzi wa vyuo vikuu nchini na siyo kukusanya fedha kwa nguvu na kinyume cha sheria kama ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepandisha makato kutoka asilimia nane hadi 15 ili kuharakisha makusanyo ya mikopo kinyume na utaratibu na sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kodi kwenye shule binafsi, Serikali ipunguze kodi kwenye shule za private kwa sababu shule hizi zinasaidia Serikali. Vilevile shule hizi za private zifanyiwe ukaguzi mara kwa mara kwani kuna baadhi ya shule zinakiuka maadili (hazipo kwenye viwango) na Serikali ihakikishe wanafunzi wa shule za private wanapewa mlo ulio kamili, kwani wazazi wanakuwa wanalipa ada nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu ya watu wazima bado ni tatizo. Watanzania wengi ambao wanaishi pembezoni hawana elimu. Waelimishwe kuhusu suala la elimu na faida zake. Watu wazima wakipatiwa elimu itasaidia kupunguza umaskini na ujinga katika nchi yetu. Ni vizuri Serikali irudishe mfumo kama wa zamani. Jioni watu wazima wapatiwe elimu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma wanafunzi wakitoka shule jioni wanaenda kusoma watu wazima.