Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii nikushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwa hotuba yake hii aliyoileta kwenye Bunge letu hili. Nampongeza vilevile Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya kuinua elimu ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza sana Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa taarifa yao ambayo kwa kweli ilikuwa inajieleza vizuri, sana na nimetoa ushauri ambao mimi binafsi nauona ni ushauri wa msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Confucius ambaye ni Mwanafalsafa wa Kichina aliwahi kusema maneno haya, akasema kwamba ukitaka kupanga kwa ajili ya mwaka mmoja, basi panda mpunga. Ukitaka kupanga kwa ajili ya miaka 10 basi panda miti na ukitaka kupanga kwa ajili ya miaka 100 ijayo, basi mwelimishe mwanao au mtoto wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ndiyo moyo wa Taifa hili. Taifa lolote ili liweze kuendelea na tafiti zimeonesha, kuna uhusiano wa moja kwa moja wa ukuaji wa elimu na ukuaji wa uchumi; hivi vitu vinakwenda pamoja. Taifa ambalo limeendelea kielimu kwa vyovyote vile linajikuta linaendelea vilevile kiuchumi. Kwa hiyo, tunajadili Wizara ambayo ni muhimu sana kwa nchi yetu; na kwa kweli namwomba Mheshimiwa Waziri aendelee kuchapa kazi kwa sababu bila hivyo Taifa letu hili tutachelewa sana kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa kutoa elimu bure kwa Watanzania. Uamuzi huu, unaweza ukaonekana wa kawaida kwa sababu ni kawaida, hata mbuzi huwa haoni umuhimu wa mkia wake mpaka uondoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikupe taarifa kwamba kabla ya elimu bure, Wilaya ya Bukombe watoto waliokuwa wanaandikishwa darasa la kwanza mpaka la saba walikuwa 45,000 peke yake. Baada ya kuanzishwa kwa elimu bure, sasa hivi watoto walio darasa la kwanza kwa elimu ya msingi yote, wanafika 75,000. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba wapo watoto wengi zaidi ambao walikuwa wanaacha shule, walikuwa wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya michango na ada hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunahitaji kumtia moyo Mheshimiwa Rais, tuitie moyo Serikali iendelee kuwekeza zaidi kwenye elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia hotuba ya Mheshimiwa Waziri na yako mambo ambayo nataka nichangie kidogo. Jambo la kwanza ni ukaguzi wa elimu. Suala la ukaguzi wa elimu lilishaelezwa kwa kila aina ya lugha, hapa Bungeni na nje ya Bunge. Ukaguzi wa Elimu wa Tanzania una hali mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi ku-suggest na vyombo vingine viliwahi kupendekeza kwamba ili ukaguzi wa elimu uweze kuwa imara ni lazima tuutoe kwenye mikono ya Wizara uwe wakala wa kujitegemea. Serikali ilishawahi kuahidi hapa Bungeni kwamba inaanzisha mchakato wa kufanya ukaguzi kuwa wakala wa ukaguzi. Ahadi hiyo nimesoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu sasa hivi, wala hakuna kinachozungumziwa, kana kwamba hakuna kitu kilichowahi kusemwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano. Kwenye kijarida cha elimu (ninacho hapa), cha Januari hadi Machi, mwaka 2013, ukurasa wa nne, Mheshimiwa Waziri wa Elimu alisema yafuatayo: “Katika jitihada zake za kuipa mamlaka zaidi na uwezo na hivyo kuongeza ufanisi katika ukaguzi wa shule na Vyuo vya Ualimu, Serikali inakusudia kuibadili Idara ya Ukaguzi wa Shule iliyoko chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuwa Wakala wa Kujitegemea. Imeandikwa humu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, Kamati ya Bunge lako iliyokuwa inaongozwa na Mheshimiwa Margaret Sitta mwaka wa fedha 2013/2014, ilikuja na mapendekezo hayo hayo ya kuifanya ukaguzi kuwa Wakala Maalum wa Elimu na Waziri wa Elimu wakati huo, mimi sijawa Mbunge, nilikuwa nje, kwa sababu mimi ni mdau wa elimu, aliahidi kuwa jambo hilo linafanyiwa kazi. Nataka kujua Mheshimiwa Waziri, hivi hili jambo limeishia wapi? Hivi hili jambo lilikuwa tu ni kwamba tumalize kipindi hicho cha bajeti hiyo, halafu maisha yaendelee? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa elimu hauwezi kuendelea kwa mfumo tulionao. Wakaguzi wana hali mbaya; Wakaguzi hawana kila kitu, kuanzia rasilimali mpaka uwezo wa rasilimali watu. Wakaguzi ni wachache, shule ni nyingi. Lazima sasa tuangalie utaratibu mpya wa kuhakikisha kwamba Walimu hawa na wao tunaweza kuwapatia fursa ya kukaguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iliwahi kusemwa iwepo Bodi ya Wataalam wa Walimu. Hii Bodi kwenye kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaiona. Hivi hata hivi vyeti feki tunavyozungumza, kama kungekuwa na Bodi ya Kudhibiti Walimu ingekuwa imeweza kuligundua hilo mapema. Hili lilishawahi kuahidiwa humu humu Bungeni na Mheshimiwa Shukuru Kawambwa wakati ule akiwa Waziri kwamba Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha Bodi ya Walimu. Hii bodi iko wapi? Mbona na yenyewe siioni! Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja kujibu, atusaidie kutupa majibu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa na wengi ni suala la vitabu. Nami nataka nizungumze kidogo hapa, nimevisoma hivi vitabu. Mheshimiwa Waziri ameeleza kwenye hotuba yake ukurasa wa 21, amesema kwamba vitabu hivi vina makosa ya kimaudhui na hivyo uchambuzi wa kina unafanyika ili vitabu vilivyochapishwa mwaka 2016/2017, kubaini endapo vina dosari; nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, vitabu hivi siyo tu kwamba vina makosa ya kimaudhui, vina makosa mengi, wala havifai kupelekwa sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu tu aliyechapisha pengine ni Serikali, anapata kigugumizi. Mwaka 2016, Mei hapa hapa Bungeni, Mheshimiwa Waziri alitueleza kwenye hotuba yake ukurasa wa 55, kipengele cha tatu, akasema hivi:

“Mheshimiwa Spika, vimeandikwa na kuchapishwa vitabu nakala 6,862,000. Akasema hivi, katika vitabu hivyo, vitabu 2,807,000 vimebainika kuwa na makosa na kwa hiyo, wamemwambia aliyevichapisha avirudishe akavichape upya.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vilivyochapishwa na Serikali vina makosa lukuki. Nitakupa mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu cha kwanza cha English, Form Four, kina makosa 34 kwa uchambuzi wangu. Kina makosa ya mpangilio; yaani ukurasa wa kwanza kwenye jedwali (table of content) lenyewe lina makosa. Anasema Preface iko roman (ii) ukienda kwenye kitabu iko roman (iii), ukiangalia chapter one, anasema iko ukurasa wa nne, ukienda kwenye kitabu ndani, iko ukurasa wa kwanza. Ni makosa mengi ambayo siwezi kuyaeleza! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitabu cha Kidato cha Tatu, kina makosa 12 ya kimantiki na nimwambie Mheshimiwa Waziri, siyo makosa ya kimaudhui, ni makosa ya kimantiki, makosa ya kimaudhui, makosa ya kiuandishi. Kwenye mwongozo wao walionao, huu hapa ninao. Unataka kitabu chochote kilichozidi kurasa 100 kifungishwe au kiwe binded kwa kutumia gundi, lakini ninacho kitabu kiko hapa, kina zaidi ya kurasa 100 lakini kimegundishwa kwa pini. Hata ubora wa vitabu vyenyewe haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anahangaika kutafuta fedha kwa ajili ya watoto wa Tanzania. Haiwezekani Mheshimiwa Rais atenge shilingi bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya watoto. Baba anatoa fedha kwa ajili ya watoto wake wapate chakula kizuri, wanaenda kupewa matango pori! Nyumba hii ambayo ni ya kwetu sisi Wabunge, Nyumba hii ya Mheshimiwa Ndugai na Mheshimiwa Tulia Ackson ikubali mambo haya yatendeke mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atuambie, ni shilingi ngapi zimetumika? Tumeambiwa zaidi ya shilingi bilioni 100 zimetumika kuchapisha vitabu vibovu hivi. Hizi fedha ni kama zimepigwa kiberiti na sasa hivi viko kwenye mzunguko vinafundisha watoto kuwapatia maarifa ambayo ni substandard. Tunapeleka wapi Taifa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie, Walimu wa Tanzania baada ya kuliona hili waliweka pembeni vitabu vyenu wakaachana navyo, wakaanza kufundisha kwa maarifa yao wanayoyajua. Hivi hata wingi wa neno sheep; neno sheep peke yake, kuna wataalam ambao wanakaa kupitia vitabu hivi, nimewasoma. Kuna mtaalam wa curriculum, kuna wataalam wa kutoka Vyuo vya Ualimu, kuna wataalam wanaotoka NECTA, kuna wataalam wa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.