Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba ya Waziri wa Elimu. Kwanza nianze kwa kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake mzuri kabisa wa kuamua kujenga mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mabweni haya yamejengwa kwa shilingi bilioni 10 na yataweza kutosha kuwa-accommodate wanafunzi 3,840. Nimpongeze sana kwa jitihada hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, nimpongeze Waziri wa Elimu na Naibu wake na pia Katibu wa Wizara na watendaji wote wa Wizara ya Elimu kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu na kupitia elimu hiyo tuweze kupata maendeleo katika nchi yetu maana bila elimu hakuna maendeleo. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu kama walivyosema wenzangu ni msingi wa kila kitu. Elimu ndiyo msingi wa maisha, bila elimu hakuna maisha. Kwa hiyo, ili tuweze kupata elimu nzuri ni lazima kuwepo na mwalimu, miundombinu mizuri lakini pia ni lazima tuwe na vitabu vya kufundishia na kujifunzia. Mimi nizungumzie juu ya walimu, walimu tunao japo tuna upungufu lakini kuna changamoto nyingi ambazo wanakabiliana nazo na ndiyo maana unakuta sasa inapofika katika kupata ile outcome tunakuwa na matatizo kwa sababu hatujawaweka vizuri walimu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema Waheshimiwa Wabunge hapa juu ya madeni ya walimu. Haya madeni ndiyo kikwazo katika utoaji wa elimu bora. Kwa wale waliowahi kuwa darasani (walimu) wanajua, mwalimu ili aweze kufundisha vizuri ni lazima awe vizuri psychologically. Huwezi kutegemea mwalimu akafundisha vizuri na akawawezesha watoto kupata elimu nzuri kama psychologically yupo disturbed. Mwalimu anapokuwa na madeni, mwalimu anapokuwa na kero mbalimbali za kwake binafsi ni vigumu kufundisha vizuri. Anaweza akaingia darasani akajipanga kutaka kufundisha vizuri wanafunzi lakini akikumbuka tu deni wakati anaendelea na jukumu la kufundisha, tayari huyu mwalimu hataweza kufundisha vizuri wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuipongeze Serikali mmeanza kulipa lakini bado speed ya ulipaji wa haya madeni sio nzuri sana. Tumeambiwa hapa na Kamati imetoa taarifa kwamba madeni ya walimu ambayo wanaidai Serikali mpaka sasa ni shilingi trilioni 1.6 na madeni yaliyolipwa ni shilingi bilioni 33.1 ambayo ni sawa tu na 32%, speed hii bado ni ndogo. Tuiombe Serikali iweze kulipa madeni haya. Tunajua madeni yanazidi kuongezeka kwa sababu wanapopandishwa madaraja madeni yanaongezeka na kwa kuwa yanaongezeka ni vizuri yalipwe mapema haya mengine ambayo yapo ili kupunguza sasa walimu wengi ambao wanakuwa frustrated. (Makofi)

Mheshimia Mwenyekiti, hali iliyopo sasa hivi na ukizingatia kuna mambo haya ya vyeti fake na ukaguzi na walimu wengine wameambiwa kuna baadhi ya vyeti havipo halali na hawajajua hatma yao. Kwa hiyo, hali iliyopo sasa hivi kwenye mashule walimu wengi hawafundishi bali wanahudhuria madarasani wanaofundisha ni wachache. Wengi wao wamekuwa disturbed na haya madeni na vyeti fake. Kwa hiyo, naomba Serikali yangu Tukufu tujaribu kujipanga kulipa madeni haraka lakini pia na hili zoezi la vyeti fake hili liweze kukamilishwa haraka ili walimu waingie darasani wafundishe wasiingie darasani kuhudhuria tu vipindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali na Waziri nafikiri anaelewa vizuri naposema mambo haya. Nafikiri atayashughulikia vizuri ili walimu wetu waweze kuendelea kufundisha na hatimaye tuje kuweza kutoa elimu bora. Tusipofanya hivyo, tutaendelea kuwaweka wanafunzi shuleni wanashinda wanacheza, wanakula chakula, wazazi wanafikiri watoto wanasoma kumbe hawasomi. Hata walimu wakuu wanafikiri walimu wanaingia darasani kumbe humo darasani hawafundishwi, mwisho wa siku matokeo yake yatakuwa ni mabaya. Kwa hiyo, niombe tukamilishe hili zoezi la vyeti fake lakini pia tukamilishe kulipa madai ya walimu ili walimu wetu hawa waweze kufundisha vizuri darasani na watoto wetu waweze kupata elimu nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine upande wa walimu pia, kuna upungufu mkubwa sana wa walimu katika shule zetu za msingi ukilinganisha na sekondari. Shule nyingi hazina walimu wa kutosha, vivyohivyo na hii inaathiri matokeo, inaathiri mwisho wa elimu kwa ujumla. Kwa hiyo, tuombe mamlaka zinazohusika ziajiri walimu. Tumeshaona kwenye hili zoezi la vyeti fake nalo limeondoa walimu wengi sana hasa wa shule za msingi. Ukiangalia idadi kubwa ya walimu wenye matatizo ya vyeti fake ni wale walimu wanaofundisha shule za msingi, kwa maana hiyo tufanye replacement haraka ili ku-rescue situation inayoendelea kwenye hizo shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa elimu maalum kwenye shule zetu hasa shule zetu za msingi. Kwa mfano, kwenye Halmashauri yangu mimi tuna shule moja pale ya Matembwe ambayo yenyewe ni shule jumuishi, inachukua wanafunzi ambao wana ulemavu tofauti tofauti, lakini tuna mwalimu mmoja tu anayefundisha kwenye ile shule. Kwa hiyo, tuombe tupeleke walimu wa kutosha na pia vifaa vya kutosha kwenye elimu hii jumuishi ili watoto hawa ambao wana ulemavu tofauti tofauti waweze kupata haki yao ya msingi, haki yao ya kupata elimu kama watoto wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema juu ya drop outs hasa hizi kesi za mimba kwenye shule zetu. Ukiangalia shule nyingi ambazo watoto wanapata mimba ni zile shule za kutwa, shule hizi za kata. Kwa nini wanapata mimba? Ni kwa sababu ya ukosefu wa mabweni. Watoto wengi wa kike wanatembea umbali mrefu sana na tunajua watoto wetu wa siku hizi hawawezi kutembea kama tulivyokuwa tunatembea sisi zamani. Kwa hiyo, kinachotokea ni kwamba wanatumia usafiri wa bodaboda maeneo mengine wanatumia taxi. Hawa wanaowapeleka shuleni ili waweze kuwahi vipindi ndio hao wakati mwingine wanawageuka kuwashawishi watoto kuingia kwenye hivyo vitendo vya ngono na mwisho wa siku wanapata mimba na wengine wanapata maambukizi ya UKIMWI na wengine wanaamua kuacha shule kwa sababu tayari wameshapata wapenzi na wanaenda kuolewa. Tunaipongeza Serikali kwa mpango huu wa kujenga mabweni.

Naomba pia katika Jimbo langu na katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Njombe na shule za kata za kutwa ambazo watoto wengi wanatembea umbali mrefu, katika ule mpango wa ujenzi wa mabweni basi na mimi nipate mabweni ili tuwaokoe watoto hawa ambao wanatembea umbali mrefu tuwakinge na mimba ambazo wanaweza wakazipata kutokana na vishawishi wanavyovipata njiani wanapoenda kwenye shule hizi za sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia umbali unachangia wanafunzi wetu kufeli. Wanatumia muda mwingi kutembea kwenda shuleni, anapomaliza kipindi anafikiria kuanza kutembea kwenda nyumbani na akifika nyumbani anakutana na shughuli za nyumbani kwa sababu ni watoto wa kike wanapewa shughuli za pale nyumbani za kupika, kutafuta maji, za kutafuta kuni lakini mwisho wa siku utakuta huyu mtoto anapoteza muda mwingi wa kusoma. Kumbe akibaki bwenini anapata muda mwingi wa kusoma na kufanya discussion na wenzake jioni mwisho wa siku atakuja kufaulu vizuri. Kwa hiyo, nashauri tujenge mabweni kwenye shule zote hizi za sekondari ili watoto wetu waweze kusoma vizuri na hatimaye waweze kupata elimu bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitishwa sana kwenye suala la vitabu. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuamua kutoa kitabu kimoja nchi nzima cha kufundishia (text book). Nipongeze kwa jitihada mlizochukua, lakini nisikitike kwa kutoa vitabu ambavyo vina makosa, ni aibu kubwa sana wakati tuna wataalam wameajiriwa, wanafanya editing ya hivi vitabu, inakuwaje vitabu vingi namna hii vinakuwa na makosa mengi ya spelling, ya kisarufi na makosa mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe ndugu yangu, dada yangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako, tukae na watu wa editing ili tujue nini kimetoea? Maana tumetumia fedha nyingi na itatakiwa tubadilishe tutatumia gharama kubwa, watuambie ni kwa nini wamekubali kutoa vitabu hivi ambavyo vina makosa? Haijawahi kutokea katika miaka yangu yote ya kusoma kwangu na katika maisha yangu yote kupata mwaka ambao vitabu vimetoka na makosa mengi namna hii, zaidi ya vitabu vya masomo karibia matano, sita, vina makosa!

Kwa hiyo, hebu tukae tujue kuna nini kimetokea? Inawezekana hao watu wanaohusika na editing walitaka kuhujumu tu Serikali ili kuonesha kwamba Serikali yetu haifanyi kazi vizuri. Nakuamini dada yangu, naomba kakae na hii Kamati au Kitengo kinachohusika na mambo ya editing ya vitabu ili tujue ni kwa nini wametoa vitabu vyenye makosa namna hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana, naunga mkono hoja.