Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Suala hili linalozungumzwa hapa la sekta ya elimu ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yoyote ile, siyo Tanzania peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi hapa na Waheshimiwa Wabunge na mengine kwa kweli yanahusu masuala ya maadili. Na mimi nitapingana kidogo na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ambao ni wanaharakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo sheria nyingi sana hapa nchini nzuri sana, mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 ndipo yalipotokea mapinduzi makubwa sana ya sayansi na teknolojia, tukawa na tv na simu na hizi zimeleta matatizo makubwa sana kwenye mmomonyoko wa maadili ya vijana wetu. Kutokana na mmomonyoko wa maadili ulivyokuwa unatishia haki za wanawake na haki za watoto. Mwaka 1998 ilitungwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, Sura ya 101 ya Sheria za Tanzania. Sheria hiyo ni muhimu sana, isipokuwa tatizo letu sisi hapa Tanzania, tuna sera na sheria nzuri lakini zimekuwa hazitekelezwi. Matokeo yake tunakuwa tunapigia kelele jambo ambalo linaweza likadhibitiwa na sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ilirekebisha baadhi ya vifungu kwenye Penal Code (Sheria ya Kanuni ya Adhabu) na ikaweka utaratibu mzuri wa namna ya kushughulika na masuala ya maadili kwa ujumla. Makosa yanayofanywa na mwanaume, yanayofanywa na mwanamke, yamewekwa vizuri sana na adhabu zake zimewekwa vizuri sana, lakini utekelezaji hafifu wa sheria hiyo ndiyo maana unakuta baadhi ya Wabunge hapa wanasimama wanaanza kupiga kelele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tumepitisha sheria hapa ambayo inadhibiti mtu yeyote anayedunga (anayempa) mimba mwanafunzi, anayeozesha mwanafunzi, anayekwenda kwenye harusi ya mtoto mwanafunzi adhabu zake ni kifungo cha miaka 30. Sasa hata hatujasimamia utekelezaji wa sheria hiyo tunasimama hapa tunasema watoto wenye mimba waruhusiwe kusoma, sawa, lakini tukipitisha hapa sheria ikasema kwamba watoto wanaopata mimba shuleni waendelee kusoma maana yake ni kwamba wote watapata mimba...

Na hiyo itakuwa ni hatari, aidha, wote au walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifuatilia vizuri hizi sheria zenyewe zinadhibiti. Kwa mfano, kwenye Ilani ya Uchaguzi tumesema kwamba mtoto aanze kusoma darasa la kwanza mpaka amalize form four. Huyo mtoto ambaye atamaliza form four yuko chini ya miaka 18 ni yupi? Taratibu tukizifuatilia vizuri, anayedunga mimba miaka 30, ambaye anaacha shule naye vilevile atafutiwe adhabu kwa sababu tunapitisha sheria hapa tuwe na utaratibu mtu aanze darasa la kwanza hadi amalize form four. Akimaliza form four ameshafika miaka 18 basi hapo tutakuwa tumetatua tatizo la mimba mashuleni na kila kitu.

Kwa hiyo, naomba sana iwe tu kwa yule aliyebakwa, kama kuna ushahidi kwamba amebakwa, hapo kwa kweli inabidi tuwe na hatua zile za kuruhusu kwamba aendelee na shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie masuala ya Jimbo langu la Sikonge. Kule kwetu Sikonge, naomba Mheshimiwa Waziri asikie, bado tunahitaji shule mpya, zile shule ambazo zilijengwa kwa mpango wa MMEM zilitusaidia sana lakini bado tuna maeneo mengi yanahitaji shule mpya kabisa na sisi Halmashauri hatuna uwezo wa kujenga shule mpya na Serikali imeondoa utaratibu wa kujenga shule mpya, hapa ametamka shule sijui tatu au nne katika maeneo maalum. Mimi naomba aiweke Sikonge katika utaratibu wa Serikali kusaidiwa kujenga shule mpya, tuna maeneo takribani
30 ambayo yanahitaji shule mpya. Watoto wetu wanatembea kilometa tisa, kumi, kufuata shule na ni wengi. Kwa hiyo, naomba sana Serikali izingatie, iturudishie mpango wa MMEM maalum kwa ajili ya Wilaya yetu ya Sikonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mafunzo ya ufundi. Sisi Sikonge tuna maeneo mazuri mawili, naomba Wizara ya Elimu iwasiliane na Halmashauri yangu ili kusudi tuone potential hizo mbili, mojawapo kijengwe Chuo cha Ufundi cha VETA. Tayari tumeshawekeza baadhi ya fedha katika maeneo hayo, ni suala la kuendeleza tu, kuna chuo cha FDC pamoja na Kituo cha Vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo napenda kuongelea ni mgawanyo wa walimu. Baadhi ya maeneo hapa nchini yamekuwa yanaathirika sana katika matokeo kwa sababu ya mgawanyo wa walimu ambao hauko sawa. Kuna baadhi ya maeneo ya nchi hii yana ziada ya walimu na baadhi ya maeneo yana upungufu mkubwa wa walimu. Kwetu sisi Tabora tuna upungufu mkubwa sana wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana katika maeneo ambayo yana ziada ya walimu wapunguzwe waletwe Tabora na maeneo mengine ya nchi ambayo yana upungufu wa walimu yafanyiwe hivyo hivyo kama ambavyo napendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kusema mengi sana, haya yanatosha, ahsante sana.