Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata hii nafasi ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hoja hii iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri aliyoitoa pamoja na mambo yote mazuri ambayo yameandikwa katika kitabu hiki cha bajeti. Kwa kweli hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimefarijika sana na jinsi ambavyo mmefanya uchambuzi wa masuala mbalimbali katika kitabu hiki, lakini pia nimefarijika na nimefurahishwa na jinsi ambavyo mnajiandaa kwenda kutekeleza Sera ya Elimu ya mwaka 2014.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera hii inataka kwamba tutakapofika mwaka 2020 watoto wetu wote watakaokuwa wanamaliza darasa la saba wataenda sekondari, kwa hiyo, inahitaji matayarisho ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi naomba nijikite katika kuongelea ubora wa elimu. Ubora wa elimu ni neno pana, ubora wa elimu una mambo mengi, tunaangalia miundombinu, walimu watakaotumika katika kufundisha, maabara, vitendea kazi na vitu vinginevyo, vitabu, mitaala na mambo mengine mengi, hayo yote kwa pamoja ndio yanajumuisha ubora wa elimu. Ni nini kimejitokeza? Sasa hivi mitaala yetu mingi haikidhi mahitaji ya soko, kuanzia shule za awali, shule za msingi mpaka vyuo vikuu katika maeneo mengi haikidhi mahitaji ya wahitaji, haikidhi mahitaji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko sokoni ni aina gani ya ujuzi unahitajika, ni aina gani ya elimu inahitajika, ni aina gani ya maarifa inahitajika, hiyo mitaala yetu lazima izingatie hayo. Kwa sasa hivi hali iliyopo mitaala mingi haizingatii hayo, mitaala yetu hii haiwaandai vijana wetu katika kupata maarifa ya kuweza kujitegemea, ndio maana watu wengi wanamaliza sasa hivi hawawezi kujitegemea. Hapa tuna kazi ya ziada ya kufanya, kama nchi lazima tufanye kazi ya ziada. Nadhani hili linahitaji participation ya wadau wote kushiriki katika kuhakikisha kwamba hii mitaala ambayo inakuwepo inakidhi mahitaji ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwenye upande wa vitabu, mimi naipongeza Serikali, mmetoa vitabu ambavyo bado vina mapungufu mengi, lakini angalau mmetoa, lakini mmetoa kwa ubaguzi. Utoaji wa elimu kwenye nchi hii siyo wa sekta ya umma peke yake, kutoa elimu lazima kujumuishwe sekta binafsi na wadau mbalimbali. Hivi vitabu mlivyotoa mnapeleka kwenye shule za umma peke yake, sasa shule za watu binafsi zinapata wapi vitabu? Shule zote zinatoa mchango mkubwa katika kuandaa wataalam na wanafunzi wetu. Hivi vitabu chapisheni, wekeni huko, hizo shule zinunue zitatusaidia sana katika kutoa elimu kwa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalisema kwa uchungu kwa sababu tarehe 5 Mei niliuliza swali hapa kwamba ni Watanzania wangapi ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Takwimu zilizoletwa kwenye lile swali zinaonesha asilimia 22.4 ya Watanzania hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Hiyo inatuonesha ni aina gani ya Taifa tunaenda kulijenga kama Watanzania wengi kiasi hicho hawajui kusoma wala kuandika. Tunaingiaje kwenye kujenga uchumi wa viwanda tukiwa na Watanzania wengi hawajui kusoma wala kuandika? Hapa kama nchi lazima tukae chini tutafakari na tuone namna gani tunaweka mikakati ya kuwasaidia Watanzania hawa ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka miaka ya nyuma tulisoma elimu ya watu wazima, ile mikakati iliyokuwepo ilitusaidia. Mimi nafikiri umefika wakati tuweke mikakati kila kijiji lazima kwenye shule zetu zile wale watu wote ambao hawajui kusoma, kuhesabu na kuandika wakafundishwe kwa lazima. Hatuwezi kujenga nchi kwamba eti wataenda wenyewe lazima wakafundishwe kwa lazima, tupate watu wote wanajua kusoma, kuhesabu na kuandika hapo ndiyo tutakwenda kujenga nchi yenye uchumi wa soko la kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa zetu inaonesha asilimia 80 na kuendelea watoto wetu kwenye shule za sekondari wanapata division four na division zero na hawa baada ya kumaliza wakiwa wamepata matokeo hivyo wanaenda wapi? Wanaenda kuchangiaje katika uchumi wa viwanda? Ndiyo maana tukasema lazima tuimarishe sekta binafsi tujenge vyuo vingi vya VETA viwachukue hawa viwafundishe, viwape ujuzi, viwape maarifa wakafanye kazi zitakazosaidia kufuatana na kiwango cha elimu walichonacho lakini hivi sasa ukisoma hotuba unaona mkakati bado haujatosha katika kujenga hivi vyuo vya ufundi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Jimboni kwangu, Jimbo la Vwawa na hasa Mkoa mzima wa Songwe hakuna Chuo cha VETA. Nilitegemea hapa useme kwamba Mkoa wa Songwe tunakwenda kujenga Chuo cha VETA sijaona na kule kuna Watanzania na shule nyingi. Baadae nitakuja kujenga hoja ya kushika shilingi kama sijapata majibu nini kinaenda kufanyika katika lile Jimbo la Vwawa na hasa Mkoa wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema hapa na kila siku tunapiga kelele, hivi kwa nini tuendelee tu kupiga kelele? Tumesema mtoto akipata mimba mwache akajifungue, akimaliza arudi kusoma, kuna tatizo gani? Kwani mtu akipata mimba maana yake asisome?

Maana yake aishie tu hapo? Huyo anaenda kujenga Taifa gani? Lazima huyu mtu akijifungua, akalea mtoto kidogo, arudi kusoma, hakuna haja ya kuweka masharti, kuna tatizo gani? Nadhani tufike mahali tuwe serious katika issues ambazo ni serious. Hawa watoto ambao wanaishia katikati lazima tuchukue hatua, watu wote wapate elimu ya msingi ndipo tutajenga Taifa zuri na lenye maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia motisha kwa walimu. Walimu katika maeneo mengi wamekata tamaa, hawawezi kutekeleza hii mitaala, hawawezi kutoa elimu bora wakiwa na frustrations. Mwalimu anaingia darasani anataka kufundisha anasema lakini ana malalamiko, hapana, tujenge mazingira mazuri, mahusiano mazuri katika kuhakikisha walimu wanakuwa na motisha na maslahi na madaraja yao yazingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Jimboni kwangu kuna walimu wengi madaraja yao yalisimamishwa, hawapati haki yoyote. Hebu liangalieni hilo ili angalau mambo yaende vizuri na tuweze kujenga Taifa ambalo ni zuri lenye manufaa na ambalo litatusaidia sisi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka pia nizungumzie suala la ile Idara ya Kudhibiti Ubora wa Elimu. Ile idara, nimeangalia kwenye bajeti, imepewa shilingi bilioni 30 na kitu hivi lakini katika zile fedha ni za mishahara, fedha za undeshaji ni shilingi bilioni 3.7 lakini kama watapewa, wanaweza wakafanya kazi kidogo. Sasa hivi ile idara haipewi fedha.