Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mwanne Ismail Mchemba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Wizara hii kwa uchungu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kwa mara nikisimama hapa huwa nasikitika, nasikitika sana kwa kuusahau Mkoa wa Tabora. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayofanya. Mheshimiwa Waziri mimi nina sababu ya kumpongeza. Mwaka 2006 alifanya kazi ambayo Tabora hawatamsahau, nataka nimkumbushe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Chuo cha Nyuki Tabora, chuo hiki kiliondolewa kikapelekwa Arusha. Mwaka 2006 nilimwomba sana Mheshimiwa Waziri na mimi nilikuwa Mbunge na yeye wakati ule alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, akakubali akakirudisha. Pamoja na kurudisha mimi nikawa Mwenyekiti wa Bodi, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, tangu 2006 hakuna mabadiliko. Niliomba sana ukarabati wa jengo la utawala ambalo lilikuwa na maabara ndani yake, jengo hilo limejengwa tangu 1949, kwa hiyo ujue umuhimu wa chuo hicho tangu Mkoloni. Mimi simlaumu, inawezekana wataalam nao wana matatizo na Tabora. Kupeleka Chuo cha Nyuki Tabora kulikuwa na sababu za msingi sio upendeleo, kule tunarina asali yaani sisi ni wafugaji kabisa wa nyuki na Tabora kuna miti ambayo inaitwa miombo ambayo ina maua mazuri, lakini nashangaa bado kinapigwa danadana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora kuna asali ya nyuki wadogo kwa hiyo wanapokitangaza Chuo cha Nyuki cha Tabora maana yake unatangaza na biashara ya asali lakini wameondoa, hakuna ukarabati wowote. Nimeangalia kwenye kitabu hapa. Mwaka jana ilitengwa shilingi milioni 500 lakini mwaka huu shilingi milioni 200 lakini ni pamoja na Chuo cha Misitu Arusha. Sasa hapo sijajua kama kweli Tabora watapata siyo rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la kusikitisha sana na ambalo linauma, tulikuwa na TAWIRI-Tabora, kituo cha wataalam wa utafiti kuhusu nyuki na mizinga ya kisasa yenye tija, nacho wamekiondoa wamekipeleka Arusha, hivi Waziri anajua hilo? Kwa hiyo, nimekuja mwaka huu nianze tena kumwomba kituo cha utafiti kirudi Tabora, hivi inawezekana? Nimwombe Mheshimiwa Waziri, namheshimu na najua kazi anayoifanya lakini kuionea Tabora nachukia sana, hiyo itasababisha na mimi nimchukie. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hilo tu mpaka gari imeondolewa imepelekwa Arusha, Waziri ana habari hiyo? Watafiti wa TAWIRI wako pale lakini wameondoa mpaka komputa. Mimi nilienda wakati ule kutembea nikakuta wanafunzi wa Arusha wanakuja kuchukua practical Tabora. Nikauliza swali humu ndani, hivi inakuwaje gharama hii, wanataka Arusha wanakuja Tabora? Wameacha kabisa na kukitangaza kwani miaka ile walikuwa wanakuja watu kutoka Ethiopia, Zimbabwe kujifunza sasa hivi wamewaondoa, sababu ni nini, hawaitaki Tabora? Leo nimwombe Waziri anisaidie kwa nini wanaidharau Tabora na kwa nini wanahamisha vitu vilivyowekwa Tabora kupeleka Arusha? Wote tuhamie Arusha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika kitabu hiki hiki cha bajeti hela za ukarabati zimeenda Njiro lakini Tabora hakuna, ukisoma humu unaona kama ukarabati upo lakini haupo. Naomba Waziri akija kuhitimisha alizungumzie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna wazabuni wanadai hebu aangalie hilo ni haki yao lazima walipwe. Wanadai madai yao ya 2016, Waziri akisimama hapa lazima aseme kitu chenye uhakika, naomba afuatilie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nahamia Malikale kwenye suala zima la utalii. Watu wanaidharau Tabora lakini ina kumbukumbu nyingi. Ukizungumzia utalii Tabora kwamba haupo, zamani nilikuwa silalamiki sana kwa sababu miundombinu ilikuwa hakuna, leo Rais kaleta ndege kwa hiyo lazima niseme ili vile vivutio ambavyo wamevisema kwenye taarifa ya Kamati na yeye mwenyewe amesema kwamba tujitahidi ila sijui lugha ya kwenda kuongelea kutafuta watalii kwa sababu ingekuwa kama kuna sehemu ya kwenda kujifunza mimi ningeenda kutafuta watalii ili waende Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora kuna kumbukumbu ya Livingstone na Stanley na ukiongelea Tabora unaongelea na Kigoma-Ujiji, hivi navyo siyo vivutio hivyo? Tabora kuna eneo ambalo alikaa Livingstone walipokutana na Stanley wakitokea Kigoma eneo la Kuyara, nayo ni kivutio cha utalii. Nimwombe Waziri atume delegation yake iende ikaone halafu baada waitangaze. Pia Livingstone alikaa Ujiji karibuni miaka 27, njia aliyopita ni Tabora na aliacha alama. Jamani naomba niwarudisheni shule ili mjue historia ya Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora kuna majengo ya Wajerumani kama ilivyo Amboni (Tanga), kuna kumbukumbu ziko pale lakini nani atazisemea? Leo bajeti ya Wizara ya Maliasili imeanza leo na mimi naitangaza Tabora kama sehemu ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna njia ya watumwa kwa sababu ilikuwa watumwa wakitoka Kigoma wanakuja Tabora wanakwenda Bagamoyo. Juzi tulipokuwa kwenye semina, Tabora haimo kwenye hiyo kumbukumbu ya Malikale, sasa leo naitangaza Waziri aikumbuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hilo tu, tuna kumbukumbu nzito sana katika dunia hii ya Hayati Baba wa Taifa. Wanafunzi wanasoma shuleni lakini hata utalii wa ndani unatosha kuwapeleka Tabora. Baba wa Taifa alisoma Tabora Boys, akafundisha Mirambo lakini wakati wa kupigania usalama wa nchi na uhuru umeanzia Tabora, jamani hii nayo inataka mtu kwenda shule kwa ajili ya kuitangaza tu Tabora? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uhuru huo ulisaidia pia kuwa na karata tatu za kuunda Serikali pale Tabora… Mwaka 1958, wenzangu wananiunga mkono, hiyo historia inatakiwa isomeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pale Tabora kuna shule ya msingi inaitwa Town School, ndipo alipokuwa anakutana na Wanyamwezi wakarimu sana, wanamfundisha, anajificha… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.