Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu katika nchi yetu. Kwanza, niipongeze hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo imetolewa na Waziri Kivuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitazungumzia Hifadhi ya Mikumi ambayo imepitiwa na barabara kuu ya Tanzania – Zambia yenye urefu wa kilomita 50 ambayo ilianzishwa mwaka 1964 kabla ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Barabara hii imekuwa na ongezeko la magari mwaka hadi mwaka. Kwa takwimu za mwaka 2012 idadi ya magari yalikuwa yanapita katika hifadhi ni 1,750 sawa na asilimia 60 ambayo yalikuwa yakipita kwenye kilomita 50 ndani ya hifadhi. Mwaka 2014 magari yaliongezeka hadi kufikia 1,991 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hili ni kubwa na maoteo yanaonesha ifikapo mwaka 2025 magari yanayopita katika Hifadhi ya Mikumi yanaweza kufika 4,699 kitu ambacho ni hatari sana kwa kukua kwa Hifadhi ya Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna madhara ya kiikolojia ambayo yanaweza kutokea kwa magari hayo kupita ndani ya hifadhi. Pamoja na madhara hayo ya kiikolojia kuna ajali nyingi zinatokea ikiwa ni pamoja na vifo vya wanyama na binadamu. Kumekuwa na ajali nyingi, nina takwimu kidogo hapa za mwaka 2011 - 2015. Nikiangalia katika takwimu zangu zinaonesha mwaka 2011 idadi ya vifo vya wanyama ilikuwa 125 katika Hifadhi ya Mikumi lakini 2012 idadi ya wanyama waliogongwa ni 111, mwaka 2013 ni wanyama 132, mwaka 2014 ni wanyama 354 na mwaka 2015 ni wanyama 237.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa wale wanyama tu ambao wanaonekana barabarani lakini wanyama wengine wanagongwa wanaenda kufia ndani ya hifadhi. Kwa idadi hiyo kubwa ni lazima hatua zichukuliwe. Barabara hii imekuwa ni changamoto kubwa na hatua zisipochukuliwa basi tunaweza kupoteza uhai wa Hifadhi ya Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwa Wizara. Wizara ya Maliasili na Utalii wanaweza kukaa na Wizara ya Miundombinu ili waangalie namna gani ya kuboresha barabara ya Melela – Kilosa - Mikumi yenye urefu wa kilomita 141.75 kwa kiwango cha lami ili tuweze kupunguza idadi ya magari ambayo yanapita ndani ya hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kitu kingine ninachoweza kuishauri Wizara ni kufanya utafiti kwa nchi nyingine ambazo barabara zinapita ndani ya hifadhi na tunaweza kuona namna gani wao wanafanya na tuweze ku-implement kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kwa TANAPA kama wanaweza kutoa tozo za magari yanayopita hifadhini yaani kutoza magari badala ya abiria ili tuweze kupata mapato yanayotokana na magari yanayopita hifadhini wakati tukiendelea kufanya tafiti mbalimbali kwenye nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato yanayopotea kutokana na magari kupita kwenye barabara ya Mikumi ni makubwa sana. Tafiti za mwaka 2012 zinaonyesha hifadhi inapoteza shilingi bilioni 4.7 kwa tozo za abiria lakini Serikali inapoteza shilingi bilioni 1.4 kwa tozo kwa ajili ya magari. Kwa hiyo, ukiangalia ni fedha nyingi sana kama Wizara tungeweza kuzingatia kutoza hizi tozo basi tungeweza kupata mapato mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoke kwenye barabara ya Mikumi, niingie kwenye kimondo ambacho kipo Wilaya ya Mbozi katika Mkoa wa Songwe. Katika Mkoa wangu wa Songwe kuna kitu kinaitwa kimondo, sidhani kama Wabunge wengi wanakifahamu labda kwa kukisikia lakini ni kivutio pekee sana kwenye Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Kivutio hicho kina changamoto nyingi sana na kinasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Ukiangalia miundombinu katika kivutio kile hairidhishi, majengo ya Ofisi ni chakavu sana, kimondo kile hakina uzio ili kusaidia ukusanyaji wa mapato lakini pia vyoo haviridhishi hivyo kusababisha wageni wengi kutofika katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka katika mchango wangu uliopita nilisema kwamba eneo lile liboreshwe hata tuweze kuweka camp site ambazo wasafiri wanaokwenda nchi za Malawi na Zambia wanaweza kufanya camping katika eneo lile na tukaweza kuongeza mapato. Kwa hiyo, nashauri Wizara itenge fedha kwa ajili ya miundombinu ya eneo la kimondo ili kuweza kuvutia wageni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naunga mkono hoja ya kupunguza tozo kwenye biashara za utalii. Tozo zimekuwa nyingi sana kwenye Wizara hii na wafanyabiashara wengi wanakwama kutokana na tozo. Vilevile pamoja na tozo hizi hakuna one stop center ya kulipia hizi tozo ili wafanyabishara waweze kufanya biashara zao kwa urahisi. Hii inasababisha hata uwekezaji wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kupungua sana na kusababisha wawekezaji kushindwa kuja kuwekeza katika mikoa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo utalii wa utamaduni na utalii wa fukwe. Utalii wa utamaduni umekuwa ni kivutio kikubwa sana kwa wageni wanaotembelea kwenye maeneo yetu ya uhifadhi. Unapotoka kwenye maeneo ya hifadhi, wageni wengi wamekuwa wakilazimika kwenda kwenye maeneo ya vijiji ili kuona utalii wa kitamaduni lakini utalii huu haujaboreshwa vizuri, hivyo huwafanya wageni wengi kutofurahia aina hii ya utalii wa utamaduni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna utalii wa fukwe, fukwe zetu nyingi bado hazijaboreshwa, sio nzuri, hazivutii. Kwa hiyo, tumekuwa tuna tatizo kubwa la wageni kutumia fukwe zetu, ni chafu, takataka ni nyingi, zinanuka na hazina huduma nzuri. Kwa hiyo, nadhani Wizara ijikite katika utalii huu ambao pia wageni wengi sasa wanapochoka kuangalia wanyama wanapenda kuona utalii wa namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia hili suala la hawa wanaokwenda kufanya field kwenye hoteli za kitalii. Kumekuwa na changamoto kubwa sana ya vijana wetu kwenda kufanya field, imekuwa sasa ni mtindo wa kawaida kwa watu wenye hoteli kuwatumia vijana hawa kwa idadi kubwa kuwafanyia kazi na baadaye kutokuwapa ajira. Imekuwa kama ni kawaida kwa wao kupewa kazi za field wanapomaliza wanachukua watu wengine lakini ukiangalia idadi ya watu wanaofanya field na idadi ya waajiriwa ni ndogo na kuwafanya vijana hawa kukata tamaa, kulipwa fedha kidogo na wengine hawalipwi wanaambiwa ni field. Kwa hiyo, vijana wetu hawa wamekuwa wakitumika sana kwenye hoteli hizi za kitalii.

Mheshimiwa Mwenyekti, kwa hiyo, naomba Wizara ije na sera au mpango wa kuona ni namna gani hawa vijana wanapomaliza vyuo wanapokwenda kwenye field, wangapi wanaajiriwa na wangapi wanaondoka. Kwa sababu inakuwa kama ni mtindo sasa wao kutumika tu kuwapatia faida wale ambao wana hoteli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani na nashauri muichukue na kuifanyia kazi. Ahsante sana.