Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, sana kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi swali langu la kwanza kwenye Wizara hii ningependa kuuliza, hivi nchi hii tuna Chuo cha Waamuzi wa Michezo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza hivi kwa sababu uamuzi ni tatizo kubwa sana. Waamuzi wamekuwa wakilalamikiwa sana mpaka wakati mwingine mtu unafikiria hivi hawa waamuzi au wanahongwa rushwa au wanapewa maelekezo na mtu fulani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati alilalamikiwa sana Waziri wa Mambo ya Ndani kwamba labda anatoa maelekezo, pengine labda kweli au wanamsingizia, lakini inawezekana. Sasa mambo kama haya naomba sana Wizara hii ituambie hivi tuna Chuo cha Waamuzi ambapo kuna curriculum inafundisha uamuzi wa mpira wa miguu, mpira wa pete, volleyball na michezo mingine kwa ujumla?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza kwa Mheshimiwa Waziri atakaposimama atueleze uamuzi wa michezo katika nchi hii curriculum yake iko wapi? Kama hakuna basi kama Taifa inatakiwa tuanzishe curriculum ya uamuzi michezo au chuo maalum cha watu kujifunza uamuzi badala ya kutegemea mafunzo ya muda mfupi kutoka kwa waamuzi ambao wana-experience na watu wengine wanatoka nje ya nchi wanakuja hapa wanafundisha brushing, hilo ni tatizo kubwa sana kwenye michezo.

Suala hili Mheshimiwa Waziri atakaposimama alieleze vizuri na hata Waziri wa Mambo ya Ndani naye kwa sababu anatajwatajwa asimame maana timu zinakwenda zinafungwa hovyo hovyo kwa sababu inaaminika bingwa huwa hapatikani kwa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu programu za michezo mashuleni na vyuoni ni jambo la muhimu sana Wizara hii kwa kushirikiana na Waziri wa Elimu na TAMISEMI wasimamie programu hizi. Nchi nyingi zimefanikiwa sana katika michezo kwa kupitia programu za michezo mashuleni na vyuoni. Kuna wakati zilifutwa, lakini nashukuru Serikali wamerudisha tena lakini uratibu wake hauendi vizuri sana kwa sababu gharama ni kubwa, wanaogopa gharama. Mimi naomba sana kwa kushirikana ndani ya Serikali Wizara kama mbili au tatu wahakikishe programu za michezo mashuleni na vyuoni zinafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ambalo napenda kuzungumzia ni academy za michezo au vyuo vya michezo. Nasikia kule Mwanza kuna Chuo cha Michezo lakini hicho chuo kimoja tu hakitoshi kwa nchi nzima hii. Nchi hii ni kubwa sana, mikoa yetu inahitaji angalau chuo kimoja kila mkoa, hicho kingefaa lakini sasa kwenye mpango wa maendeleo wa Wizara hii hakuna hata pendekezo. Mimi nadhani ili tuwe serious tutoe vijana ambao watashindana katika ngazi za kimataifa ni muhimu sana vyuo vya michezo vya watoto wadogo viwepo angalau kimoja kila mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuzungumzia ni suala la utamaduni, mwenzetu mmoja nimemsikia amezungumzia ngoma za asili. Hili suala la ngoma za asili limeachwa nyuma kabisa, sio kwenye television tu peke yake hata kwenye redio, zamani RTD ilikuwa kuna programu maalum kabisa ya ngoma za asili siku hizi hamna. Watu wanacheza miziki ya Marekani labda wataishia kucheza bongo fleva lakini ile tumbuizo asilia hakuna. Hilo ni tatizo kubwa sana. Wale wanaotoa leseni kwenye vipengele vya maelekezo ndani ya leseni wanatakiwa wawaambie na wafuatilie vituo vya television na redio lazima wazingatie kucheza ngoma zetu za asili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kuhusu ngoma za asili ni kuhakikisha kunakuwa na programu maalum hasa wakati ambao ni wa mapumziko vijijini. Kuna wakati ambao wakulima wameshavuna, zamani kulikuwa na matamasha ya ngoma za asili katika kila Wilaya, angalau wakati ule hasa hasa mwezi wa sita au wa saba wakati watu wamevuna hawana kazi nyingi za shamba, kipindi kile kingekuwa sasa kila Wilaya inaratibu tamasha la ngoma za asili ili kuhakikisha kwamba tunaendeleza utamaduni wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo naamini Mheshimiwa Waziri atatolea ufafanuzi na atazingatia kwenye kwenye hotuba yake.