Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Salum Mwinyi Rehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kwa kupata nafasi hii adhimu ili niweze kuchangia katika taarifa hii ya bajeti ya Wizara ya Habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kasi aliyoanza nayo katika Wizara hii na kuonesha nia kweli kuleta mabadiliko yaliyoachwa na mtangulia wake kwa Wizara hii ya Habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo nataka nitoe shukrani ya dhati kabisa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha Zanzibar kuweza kupata nafasi ya kuwa mwanachama wa CUF au Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CUF), nafasi ambayo ilikuwa imetafutwa kwa miaka mingi na kilio kikubwa kwa Wazanzibari kuweza kupata nafasi hiyo, nao kushiriki kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupata nafasi hiyo, bado naomba Wizara hii kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania TFF na kile cha Zanzibar ZFA kuendelea na jitihada hizo katika kutafuta nafasi ya FIFA ili nayo iwe mwanachama kama ilivyo Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nilichokuwa nakiomba, ushirikiano uliokuwepo baina ya ZFA, TFF na Wizara zetu mbili hizi za Michezo za Tanzania Bara na ile ya Zanzibar uweze kuendelezwa katika mtazamo wa kuisaidia Zanzibar au ZFA ili nayo timu zake zinazoshiriki katika mashindano hayo ya Afrika ziweze kuwa na nguvu, kwani kwa hivi sasa timu nyingi zilizokuweko kule Zanzibar, kwa mfano, ndani ya Jimbo langu nina zaidi ya timu 60, lakini nina wachezaji ambao tumechukua Tanzania Bara wanaweza kufika hata 300. Kwa hiyo hii fursa ya ushirikiano huu iliyokuwa imepatikana isikatikatishwe kwa vile Zanzibar sasa hivi imepata kuwa mwanachama wa CUF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninachotaka nikione kwamba kinaendelezwa ni suala zima la michezo hasa kwa vijana wadogo. Tuna mashindano ya Coca Cola na kuna mashindano mengine mbalimbali ya NSSF ambayo yanashirikisha timu kutoka Zanzibar na hizi Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli timu hizi au mashindano haya yanaleta chachu ya ushindani na kuibua vipaji vingi vya wachezaji mbalimbali kuonekana wale wa Zanzibar wanapata nafasi ya kuja kucheza timu za Tanzania Bara, lakini na wale wa Bara wanapata nafasi ya kuja kucheza kule Zanzibar. Naomba fursa hii iweze kusimamiwa na Wizara na kuwe na mashindano ya ushindani kweli ambayo yataweza kuwanufaisha pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumza ni programu zima ya kuendeleza vijana wetu. Zanzibar miaka ijayo tunategemea nasi kuanza maandalizi ya vijana kwa ajili ya AFCON kama ilivyo Serengeti Boys, mkakati ambao unatakiwa uungwe mkono pande zote mbili na kuwe na programu za kushirikiana ambazo zitaziwezesha kuwa na timu ambayo itaweza kufanya vizuri na kupata nafasi kama ilivyopata nafasi Serengeti Boys.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi hizi zinataka ziungwe mkono na wanachama wote, Wabunge, wadau mbalimbali wa ndani na nje ili leo hii tuione kwamba Serengeti Boys inavuka hapa tulipo na inatimiza lengo ambalo ilikuwa imetuahidi na iliyomwahidi Makamu wa Rais kwamba safari hii italeta kombe la Afrika la Vijana Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri akae na mwenzie, Mheshimiwa Waziri yule wa Zanzibar waangalie mkakati ukoje, kwa miaka mingine mitatu ijayo timu zetu hizi tutaweza kuziinua na kutengeneza timu ambazo zitaweza kuonesha ushindani na kupandisha kiwango cha mpira hapa Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi hapa tarehe mosi kulikuwa na maadhimisho ya siku ya habari ambayo yalifanyika kule Mwanza. Waziri alitoa kauli kali kidogo, nami kama mdau wa habari vilevile niliguswa na ile kauli. Sasa sijui iko vipi? Kauli ambayo ilipiga marufuku uchambuzi wa magazeti katika vyombo vyetu vya habari. Sasa tunauliza; Mheshimiwa Waziri, siyo Watanzania wote ambao wanaweza kuwa na uwezo wa kununua gazeti, lakini siyo Mtanzania yeyote anaweza kufikishiwa magazeti haya. Leo tutakapopiga marufuku uchambuzi ule wa habari, wengi wao tumewanyima haki ya kupata habari Watanzania. Kwa sababu Magazeti yale au uchambuzi ule wengi wetu tulikuwa tunasikiliza kupitia redio, kwa hiyo, hata vile wengine kununua…

T A A R I F A...

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nimeipokea hiyo taarifa. Naomba kuisherehesha. Fursa hii ya uchambuzi wa magazeti ndiyo sauti ya Watanzania wengi, inaweza kuwaambia kwamba ndani ya dunia hii au ndani ya Tanzania hii kuna taarifa hizi, hizi na hizi kwa leo; na kesho kuna taarifa hizi na hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aweze kulitathimini agizo lake hili, kwa kweli linawakosesha fursa kubwa Watanzania kupata habari ambazo zinapita katika vyombo vyetu vya habari hivi hasa asubuhi kwa uchambuzi wa magazeti mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mwenzetu alivyosema, kundi hilo la wasioona na kuna makundi mengine mengi tu ambao uwezo wa kununua gazeti hawana, lakini wanazihitaji taarifa. Hili lipitiwe tena upya na Mheshimiwa Waziri atoe kauli ili kuweza kuwapa fursa Watanzania kupata habari kama walivyokuwa wanapata habari hivi sasa. Nitamsikiliza kwenye majibu yake ili tuone kitu gani ambacho ataweza kutuambia Watanzania katika hili eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kuzungumza suala zima la Wasanii. Tanzania hii wanapozungumzwa Wasanii wanadhaniwa kwamba ni Wanamuziki na wale watu wa Filamu; lakini kuna kundi kubwa la wafinyanzi, wachongaji, waandishi wa vitabu mbalimbali, sijaona jicho la Mheshimiwa Waziri au Wizara yake kuweza kuangalia kundi hili na vipi wanavyoweza kuwasaidia kuinua vipaji vyao, lakini watu hawa wanaitangaza Tanzania katika Sanaa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kisiwa cha Brunei ni mteja mkubwa wa bidhaa za vinyago ambazo zinachongwa Tanzania. Taarifa nilizonazo, kwa miaka mitano iliyopita wamenunua bidhaa hizi zaidi ya Dola milioni 600, zinanunuliwa katika maeneo mbalimbali na yeye kule wameweka ma-shop mall ya vinyago hivi ambavyo vinachongwa katika maeneo yetu mbalimbali.

Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, eneo hili nalo jicho lake liweze kuelekea. Wakurugenzi au Wizara iwe na mpango maalum wa kuwatambua kwanza, lakini siyo kuwatambua tu kama ilivyokuwa wanatambuliwa wanamuziki ambao mpaka leo hawana walichokipa kutokana na mirahaba inayopatikana waweze kupewa support na Serikali na zile bidhaa zao zitangaze utalii wa nchi yetu na sanaa iliyokuwepo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba BASATA, bado haijafanya kazi ya kuwasaidia wanamuziki na wacheza filamu wa Tanzania.