Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii jioni hii ya leo. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe kwa kazi nzuri ambayo anaifanya na ameonyesha kwamba yeye ni mwanamichezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nachukua nafasi hii kumpongeza sana Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ndugai kwa kutupa ushirikiano mkubwa, hasa timu yetu ya Bunge Sports Club. Pia nimpe pongezi nyingi Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu yeye siyo tu kutupa ushirikiano, amekuwa ni mchezaji mahiri ambaye anapokosekana, basi inatupa shida. Kwa nafasi hii pia, nawapongeza sana timu yetu ya Lipuli Sports Club ya Iringa ambayo imepanda daraja. Naomba Mungu awajalie ili wahakikishe kwamba tunaendelea na tuweze kuchukua ubingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuchangia sana sana leo nitajikita kwenye kutoa ushauri zaidi, kwa sababu tumekuwa tukichangia mara nyingi kwenye Wizara hii ambayo kwa kweli ina wapenzi wengi kuliko Wizara nyingine. Kwa sababu wanamichezo wapo wengi kuliko wanachama wa vyama vyetu vya kisiasa, lakini bado haijatendewa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ambayo Wizara hii imepitishiwa ni shilingi bilioni kama 28. Fedha hii haitoshi kwa sababu Wizara hii imebeba mambo mengi. Wizara hii mwaka 2016 tofauti na mwaka 2015 ambapo walipata fedha nyingi kuliko mwaka huu; sasa mimi sina hakika kama tuna dhamira ya kutaka kweli kupambana na mambo ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba tutawalaumu TFF kwamba hatufiki mbali, tutawalaumu michezo mingine lakini Serikali bado haijaamua kwa dhati kwamba tumeamua sasa michezo iwe kazi. Sasa hivi bado michezo ni baada ya kazi, lakini ingekuwa ni kazi, basi ingetengewa bajeti ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja niliuliza swali hapa Bungeni kwamba kwa nini michezo isifutwe? Wengi hawakunielewa, wengi walifikiria kwamba huyu jamaa vipi, amechanganyikiwa? Wengine wakafikiria labda sijui nafikiria kitu gani, lakini nilikuwa na maana tu kwamba kama kweli tunataka kuendeleza michezo kwa bajeti hii, hatutafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri kwamba kama kweli tumedhamiria kuisaidia Wizara hii na Mheshimiwa Mwakyembe na Naibu wake waonekane wamefanya kazi, basi tuhakikishe Bodi ile ya Michezo ya Kubahatisha inahamia kwenye Wizara hiyo. Mheshimiwa Waziri wa Fedha bila kufanya hivyo Mheshimiwa Mwakyembe hutafanya lolote, utaondoka hutafanya chochote ambacho unaweza ukajivunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwa sababu sheria inasema, fedha ambayo inatoka kwenye Bodi hiyo ni ile ya mchezo wa Bahati Nasibu ya Taifa, lakini kwenye Bodi ile kuna michezo mingi kama betting, kuna casino ambazo zinaingiza fedha nyingi. Zile zinakwenda Wizara ya Fedha, inayokwenda pale ni kutoka kwenye mchezo wa Bahati Nasibu ya Taifa ambao unachezwa mara moja au mara nyingine hauchezwi kabisa kwa mwaka. Kwa hiyo, nafikiri tuhamishe Bodi hiyo iende iwe chini ya Wizara ya Michezo, kutakuwa kuna fedha ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tuvunje Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ma tuanzishe kitu kinaitwa Shirikisho la Michezo la Taifa. Ukishaweka shirikisho, maana yake itakuwa ni rahisi kutafuta vyanzo vya pesa; lakini leo Baraza la Michezo wako hoi, hawana kitu chochote. Na mimi nilikuwa Mjumbe wa Baraza na najua yaani hapo unawasukuma tu, lakini hatuna dhamira ya kweli ya kuinua michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri tutoke. Mwaka 2016 nilishauri nikasema niko tayari mkitaka niwasaidie kuandika kitu hicho kizuri, kwa sababu nilishafanya utafiti, ninazo nondo za kutosha, hamtakwama. Msiogope kupata ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye TFF. TFF nawaomba pamoja na kuwa fedha ambazo mnapata ni kidogo, lakini hebu wekeni mambo vizuri, kwa sababu malalamiko kwa TFF sasa hivi yamekuwa ni makubwa, vilabu havifanyi chaguzi, Mabaraza ya TFF mikoani imekufa, ni migogoro. Kwa hiyo, tusitegemee kama tutakuwa na timu nzuri. Kwa hiyo, nashauri hebu jikiteni kwa wanachama wenu, wapeni uelewa waweze kuelewa wapi tunatoka na wapi tunakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumekuwa tunafanya vibaya na timu yetu ya Taifa. Ukiangalia ligi ya Tanzania kwa Afrika Mashariki ndiyo ligi bora sawa sawa na Uingereza. Ligi bora kwa sababu gani? Kanuni za mchezo wa miguu kwa nchi yetu zinaruhusu kuwa na wachezaji wengi kwenye vilabu. Kwa hiyo, unakuta timu ya Taifa ligi ni nzuri, lakini unapokwenda kuchangua timu ya Taifa huwezi kupata wachezaji wazuri, kwa sababu wachezaji wale wengi ni wa nje ya nchi yetu kama ambavyo ligi ya Uingereza ilivyo. Ligi ya Uingereza ni nzuri, lakini hawana timu ya Taifa nzuri. Kwa hiyo, naomba warekebishe hizo kanuni ili tuweze kupata timu nzuri ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu academy. Tunasisitiza kwamba kila timu iwe na academy na watu binafsi waanzishe academy, lakini kuanzisha ni gharama kubwa. Kwa hiyo, nafikiria tujikite zaidi kwenye mashindano ya UMISHUMTA, UMISETA, SHIMIWI na michezo mingine, zile ndiyo academy zetu ambazo sisi wengine tumetokea huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, njia ni ndogo tu, wachezaji wa mpira wa Tanzania wana chama chao, nami bahati nzuri ndio nilikuwa Rais wa kile chama kinaitwa SPUTANZA. Kupitia SPUTANZA wangeweza kupata wachezaji wale ambao wamestaafu wakagawanywa kwenye mashule yote.

Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI anasikia pale, mkashirikiana wale wachezaji wakagawanywa shule zote Tanzania, hata kwa posho ndogo, ungeona mabadiliko ambayo yangetokea kwenye michezo, lakini leo hii ni taabu kwa sababu huwezi kuwaajiri na fedha hazipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Chuo cha Michezo kiko Malya. Chuo kile kinapata kila mwaka bajeti ndogo. Sasa kuna haja ya kuanzisha Chuo kingine hasa Mikoa ya Nyanda za Juu ya Iringa, Mbeya, Rukwa tukawa na chuo kingine kule. Kile chuo watu hata hawakitambui, hata Makete tungeweza kuanzisha kwa sababu ya hali ya hewa nzuri, lakini sehemu inayofaa kabisa ni Kilolo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii niwapongeze sana wachezaji wa zamani. Leo Kitwana Manara amewawakilisha wote hapa. Hebu niseme, tuweke utaratibu wa kuwaenzi hawa watu. Leo hii kuna mtu kama Jela Mtagwa, amewekwa mpaka kwenye stamp ya nchi hii, lakini leo ukimwona unaweza ukatoa machozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu kama Athuman Chama, anaugua pale anakosa hata pesa, hivi kwa nini sasa Serikali, Mheshimiwa Mwakyembe usifanye mpango wakapata hata bima ya afya tu? Tutakuwa tumewaenzi wachezaji wote wa zamani, kitu ambacho kiko ndani ya uwezo wako. Kwa sababu haiwezekani ukawa unashangilia wakati anafanya vizuri, wakati akishachoka na yeye tunashindwa kumsaidia, kwa hiyo tuwasaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo yuko Sambu ametufanyia vitu vizuri, tumtunuku hata Bima ya Afya. Inawezekana hata Bima ya Afya yule hana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa kweli nisingependa kuchukua muda mrefu, niseme tu Mheshimiwa Mwakyembe na Mheshimiwa Naibu wako, hebu zungumzeni na wadau wa michezo kwenye mikoa, wanawahitaji. Piteni pale mzungumze nao, wanaweza wakashauri kitu kizuri. Tuko wapi? Tumetoka wapi? Tunatakiwa kwenda wapi? Kwa sababu wameachwa, hawana watu wa kuwasikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.