Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia uzima na kunipa afya kuweza kusimama hapa ili kuchangia hoja ya Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kwa kweli kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Naibu wake, na jopo zima la wataalam katika Wizara yao kwa kazi nzuri sana wanayoifanyia nchi yetu na kuitendea haki sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, kipekee pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa dhamira njema sana ya kuhakikisha kwamba sekta ya afya hapa inakwenda kuboresha afya za wananchi walio wengi wa vijijini na hasa wale watu maskini ambao hawana uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamekwishafanyika na Mheshimiwa Rais wetu, kipekee naomba nilenge sekta ya afya, ametenda mengi lakini kubwa ambalo katika sekta hii naweza kulisema ameondoa tatizo sugu la uhaba wa vitanda katika Hospitali ya Muhimbili; ameweza kutoa amri na kurekebisha vitendea kazi ambavyo vilikuwa havifanyi kazi, na zaidi sana dhamira yake njema ya kuboresha sekta ya afya kwa kuinua hadhi hospitali mbalimbali, vituo vya afya na zahanati katika vijiji katika kuboresha afya ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Mkoa wa Manyara hatuna la kusema, tunatoa pongezi na shukrani nyingi sana kwa kuridhia kupandisha hadhi Hospitali yetu ya Haydom ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja akaitembelea, akaiona na akatoa pendekezo kwamba anakubali iwe Hospitali ya Rufaa ya Kanda, lakini vilevile akatoa jopo la wataalamu kuja kuangalia vigezo na ninaamini kwamba vigezo vinakidhi. Kubwa la kushukuru amemtuma Mheshimiwa Waziri wa Afya hivi karibuni, hana hata siku tatu ametoka Manyara kuangalia Hospitali ya Haydom kama inakidhi vigezo vya kuwa Hospitali ya Rufaa. Hongera sana Mheshimiwa Rais wetu, hongera Mheshimiwa Waziri Mkuu, hongera Mheshimiwa Ummy Mwalimu na timu yako nzima katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ametupandishia hadhi kituo chetu cha afya cha Dongobesh kuwa Hospitali ya Wilaya na hilo nalo ni katika harakati za kuboresha afya katika Mkoa wetu wa Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatoa shukrani nyingi, kwa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. Lakini sambamba na kupandisha hadhi ya Hospitali ya Haydom kuwa ya Rufaa ninatoa tahadhari na ombi kwa Serikali kwamba mara nyingi wakipandisha hadhi hospitali, huduma zinazotolewa kwenye hospitali hizo zinakwenda kupanda gharama. Tunaomba kwa dhamira hiyo hiyo ya kuboresha afya katika vijiji tunaomba wasimamie kwamba Hospitali ya Haydom itakapopanda hadhi kuwa ya rufaa, basi na huduma zitakazotolewa ziweze kuwa wananchi wetu wanazimudu kwa maana ya kwamba kutopandisha gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na habari njema hizi nilizotaja bado Mkoa wa Manyara una matatizo lukuki. Kubwa sana ni katika Wilaya za Simanjiro na Kiteto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Kiteto, mimi nimekuwa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya ya Kiteto kwa miaka mitatu. Wilaya haina gari la wagonjwa. Miaka yote niliyokuwa pale, gari ni moja iko garage kila wakati, miundombinu ya Wilaya ile ni mibaya sana, bila gari wananchi wanafia barabarani na sasa hivi tunasikia habari njema za kugawa magari kwenda katika Wilaya mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa moyo wa dhati Hospitali ya Kiteto iweze kupata gari ya kubeba wagonjwa ili iweze kuondokana na tatizo la usafiri kwa wagonjwa wetu. Tukizingatia Wilaya ile ni kubwa sana, miundombinu ni mibaya barabara ni za rough roads, tunakuomba Mheshimiwa Ummy iangalie Kiteto kwa jicho la ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika Wilaya ya Simanjiro, hapo ndipo fungakazi. Wilaya ya ile ni ya siku nyingi lakini hakuna Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba, leo, walivyosikia jina langu nachangia mchana, Mkurugenzi alinipigia simu. Akasema najua kwamba na Mbunge yupo mama tunaomba utoe kilio chetu kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Menyekiti, hakuna kituo cha afya pale au Wilaya yetu ya Simanjiro haina Hospitali ya Wilaya na hili ni tatizo kubwa sana. Wagonjwa wanatoka Orkesment kwenda kupata huduma ya afya Seliani – Arusha, kilometa karibu 200. Wanatoka Orkesment kwenda Mererani kilometa karibu 122, wataoka hapa wanakwenda KCMC kwa kilometa nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba, najua kwamba Wilaya imeshakuandikia barua toka Disemba, 2016 na ninadhani hapo nitashika shilingi pamoja na mambo mazuri na sifa niliyokupa.

Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Simanjiro iweze kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Urban cha Orkesment kuwa Hospitali ya Wilaya ili wananchi wale wapate huduma ya afya kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo sasa hivi ambapo hali ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo niendelee kuchangia kwamba huduma za afya hasa zahanati zetu za vijijini, katika Wilaya hizo nilizotaja ni za duni sana. Hata hivyo tumepata habari njema kwamba, Wizara ya Afya imetenga shilingi bilioni 251, hizo zinakwenda kuboresha huduma za afya. Pamoja na hayo, katika zahanati na vituo vya afya vingi vijijini hakuna madaktari, hakuna wahudumu wataalam wa afya kwa hiyo, hizo fedha zinakwenda kutumika kwa jinsi ambavyo haitaboresha afya za wananchi. Tunaomba sambamba na kutoa fedha kwa ajili ya huduma za afya, Serikali iangalie kupeleka wataalam, madaktari, wauguzi na wahudumu wenye taaluma katika Wizara ya Afya. Kituo kizima kinakuwa na mhudumu ambaye hana hata elimu yoyote na ndiye anayetegemewa kama daktari, kama muuguzi. Haya ninayosema ni ya kweli, tufanye utafiti tusaidie wataalam waende katika wilaya zetu hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haraka haraka nije kwenye sekta ya maendeleo ya jamii na mimi nioneshe masikitiko yangu kidogo katika sekta hii. Najua kwamba umefanya mengi na tumesikiliza jinsi ambavyo umetueleza mengi katika sekta ya afya na hata katika sekta ya maendeleo ya jamii, lakini niseme mengi bado yanaonekana kama nadharia. Tutakwenda kuboresha, tutasimamia, bado hatujapata hasa hasa ni nini kimefanyika, hatujaona sheria zinazokandamiza wanawake kuletwa hapa ili tuweze kuzirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuoni mikakati madhubuti ya kuondoa ajira haramu ya watoto wetu katika migodi na kadhalika. Hatujaona ni jinsi gani wazee wetu wanaenda kunufaika na hizi shilingi 251,000,000,000 za sekta ya afya. Kwa hiyo, mimi nitoe rai kwamba pengine ni vizuri Wizara ya Afya ni giant ministry, sekta ya maendeleo ya jamii ni kama imemezwa, nilikuwa nashauri na kwa kuzingatia kubana matumizi, pengine sekta ya maendeleo ya jamii ingeenda kwenye wizara ambayo si kubwa kama Wizara ya Afya ili iweze kutendewa haki na yenyewe iweze kuhudumia wananchi zaidi kwa jinsi ambavyo sasa hivi inahudumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni ombi ambalo niliona nilitoe na ni mawazo yangu, lakini ninazingatia suala la kubana matumizi. Ninaomba kwamba Waziri atakapokuwa ana-wind up atueleze sasa sisi wananchi wa Mkoa wa Manyara, kwanza pamoja na shukrani tulizompa, na asituone kwamba hatuna shukrani, lakini atutendee haki katika Wilaya zetu nyingine, hasa hizi za wafugaji za Simanjiro na Kiteto. Waheshimiwa Wabunge wa Wilaya nilizotaja, mimi ni Mbunge wa Viti Maalum, tunajenga nyumba moja, tusaidiane wala mtu asinielewe vibaya, lakini mimi pia nimepata kura zangu kutoka kwa wananchi Wilaya hizo, naomba tusaidiane kuhakikisha kwamba na Wilaya hizi zinapata huduma ambazo wananchi wengine wanapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ni gari la kubeba wagonjwa. Wilaya zetu hizi zina kilometa nyingi sana, hususan Wilaya ya Simanjiro ina square kilometer zaidi ya 20,000; unaweza kuangalia kutoka kituo cha afya hadi makazi ya wananchi ni zaidi ya kilometa 20, 30 hadi 50, nadhani utaona umuhimu wa kupeleka gari katika maeneo haya. Tunakuomba Mheshimiwa Ummy na tunakuamini, wewe unatosha na unatosha kabisa na chenji inabaki, naomba upeleke gari katika Hospitali za Kiteto na Simanjiro ili tuweze kuhudumia wananchi wetu na wenyewe wanufaike na huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, hongera CCM, hongera Serikali yangu ya CCM kwa kufanya haya, hasa Serikali ya Awamu ya Tano, wamefanya kazi kubwa na tunampongeza Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.