Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mimi niweze kuchangia kwenye hoja ya Wizara hii muhimu sana kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipende kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya katika Wizara hiyo, Naibu Waziri wake Dkt. Kigwangalla, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nianzie kwenye hili la madaktari. Mwezi uliopita tulikuwa na sherehe zetu za wazazi pale Kagera, mojawapo ya kazi yetu ni kwenda kutoa huduma katika hospitali. Hospitali ya Mkoa wa Kagera inahitaji Madaktari Bingwa 21, madaktari waliopo ni wawili. Sasa naiomba Wizara hii, nina imani hawa wakubwa niliyowapongeza ni wasikivu sana. Ukitafuta ratio ya 21 na mbili pale watu wanapata shida sana. Nawaamini, lakini nichukue nafasi hii kuomba kwamba kazi mnayofanya ni kubwa lakini hao wenzetu hospitali inalemewa na hawana mahali pa kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili tulikuta tatizo lingine pale, kama alivyosema aliyemaliza kuongea sasa hivi. Tuipongeze Serikali kwa mara ya kwanza pesa ya dawa ipo katika Halmashauri. MSD inafanya kazi kubwa lakini inawezekana imelemewa sasa. Isaidiwe, iongezewe nguvu ili dawa zipatikane ziweze kwenda kwenye vituo vya afya na hospitali zetu. Kila unayemuuliza hapa kwenye Halmashauri yake, pesa zipi, dawa hatujapata kutoka MSD.

Kwa hiyo, nina uhakika Mheshimiwa Ummy na Naibu kwa kazi mnayoifanya hebu elekezeni macho yenu kule kwenye MSD, kwa sababu MSD ndiye anafikisha dawa kwa Watanzania waliokuwa wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru hicho wanachokipata lakini kila mtu anakwambia nimeshapeleka hela sijapata dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niende kwenye hiyo hiyo MSD. Tunaomba MSD ule utaratibu mliotengeneza kidogo wa kuweka alama kwenye madawa ya Serikali, kila dawa ya Serikali iwe na alama yake ya nembo inayojulikana ili tuweze kuendelea kutunza dawa hizi zisiende kwenye maduka ya watu binafsi. Katika hilo naipongeza sana Serikali, lakini sasa yale maeneo ambako hamjaanza kuweka zile nembo ni vizuri zile alama ziwepo ili mtu akienda kuuziwa dukani anasema ile ni ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu kwa sababu bajeti iliyopita kwenye eneo la dawa ilikuwa kama shilingi bilioni 50 au 65, lakini mwaka huu wameenda zaidi ya shilingi bilioni 200 na mpaka leo Serikali yangu imeshaweza kutoa zaidi ya shilingi bilioni 120, ni kitu cha kupongeza sana kwa maana kwamba Serikali hii inajali afya ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie kwenye maendeleo ya jamii, ndugu zangu haya maendeleo ya jamii mbona wanyonge hivi? Kila Halmashauri utakayokwenda ukamkuta mtu wa maendeleo ya jamii hana hamu na kazi yake. Hapewi gari, hapewi huduma, haonekani kama ni mtumishi, kwa nini ndugu zangu? Hawa ni watumishi na wana haki kama idara zingine! Lakini wao wanakuwa ni watumwa fulani katika ofisi, hakuna mtu utamkuta amechangamka kwenye kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe, Wizara hii ni kubwa dawa zipo, mazuri yapo. Mheshimiwa Ummy hebu hamia hapo kwenye watu wa maendeleo ya jamii. Hawa ni watu muhimu sana katika taasisi yetu, shughuli zao ni nyeti sana. Lakini unakuta Mkurugenzi akisema lazima “ah wewe subiri” akifanya hivi “wewe ngoja bado kasma haipo.” Kwa nini hawa watu wawe wanyonge? Hebu tuwaongezee nguvu basi kama idara zingine zinavyofanya kazi ili na wao wawe na afya katika meza zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niongelee madaktari. Tunaipongeza Serikali, imesema inaajiri madaktari hao 258; mimi nafikiri tumpongeze Rais kwa uamuzi wa haraka. Hotuba ya wenzangu huku wamesema kwa nini watu wanasikia hamu kwenda kufanya kazi nje. Unajua ajira ni nafasi, zamani tulikuwa kila mtu anaweza kuajiriwa kwa nafasi zilikuwa chache, lakini leo lazima ikama iwepo, mshahara uwepo, na taratibu ziwepo ndiyo mtu aajiriwe. Sasa watu wameambiwa wanaenda Kenya na wanajua wanaenda kulipwa dola, kuna mtu atabaki? Habaki mtu ukishatamka dola.

Sasa Rais wetu tumpongeze kwa maamuzi ya haraka kwamba hawa waliokwishajitolea wanataka kwenda nchini nyingine kufanya kazi hebu tuwape ajira moja kwa moja watufanyie uzalengo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri badala ya kulaumu hebu tumpongeze Rais kwenye uamuzi huo. Rais hata kama mtu unatakiwa kupinga akifanya jema basi tumpongeze, na siamini kama kuna Mbunge yeyote wa upinzani atasema madaktari wanaoajiriwa kesho kutwa kwenye Jimbo langu wasije, yupo? Mtawapokea, sasa kwenye kuwapongeza tumpongeze Rais anataka kutuondelea ile kero.

Kwa hiyo mimi nimeona niseme lakini watani wangu wa upande wa pili kwamba hoja Rais akiajiri kote Watanzania tutapata faida ya wale wanaoajiriwa. Sasa msingi wa kubeza unapunguza nguvu ya wale watendaji wetu. Mimi niwaombe sana, mema anayofanya Rais wetu tumpigie makofi, yakiwa mapungufu mna haki ya kusema kwa sababu kazi yenu ni kurekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naendelea kusema kwamba akifanya mema Rais tumpongeze wala haina tatizo. Hata hivyo ninyi kukosoa ni jukumu lenu ndiyo maana mmekuja humu mkosoe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo mimi hoja zangu zilikuwa zinaishia hapo. Naunga mkono hoja, naendelea kuipongeza Wizara chapeni kazi, mko vizuri, fanyeni muungano, tuko nyuma yenu, Chama cha Mapinduzi kitawaunga mkono. Nakushukuru sana.