Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Binafsi nitoe pole kwa misiba iliyolipata Bunge letu kwa kipindi cha mwaka huu. Kipekee nikushukuru kwa upendo wako kwa Wabunge hata tunapokuwa na matatizo unakuwa mstari wa mbele kutusaidia. Naomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za Marehemu mahali pema peponi. Mheshimiwa Sitta, Mheshimiwa Hafidh na Mheshimiwa Dr. Elly Macha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuungana na Wabunge wenzangu katika kuangalia changamoto mbalimbali za miundombinu ya maeneo mbalimbali katika nchi yetu ikiwa ni pamoja na Mkoa wangu wa Songwe ambao ni mkoa mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto za barabara katika Mkoa wa Songwe, mfano, barabara inayounganisha Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Momba inayoanzia Chapwa, kupitia Vijiji vya Nanole, Chiwezi, Msambatu, Chindi, Msagao hadi Chitete. Naomba Waziri anapohitimisha aniambie ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya barabara hii ili kusaidia maendeleo ya Mkoa mpya wa Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imepitiwa na barabara kuu ya Tanzania kwenda Zambia kwa takribani urefu wa kilometa 50 kati ya eneo la Doma na Mikumi na kwamba barabara hii ilianzishwa kabla ya mwaka 1964 kabla Hifadhi ya Taifa ya Mikumi haijatangazwa. Wakati barabara hii haijawekwa lami, magari yalikuwa machache na yalipita kwa mwendo mdogo. Baada ya barabara kuwekwa lami magari yaliongezeka sambamba na mwendokasi hivyo kusababisha ajali na vifo vingi vya binadamu na wanyamapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto hizo, TANAPA mwaka 1999 waliainisha na kujenga matuta maeneo yenye mapito ya wanyama. Jumla ya matuta 12 yalijengwa na alama za barabarani kuwekwa katika kilometa 50 zilizo za hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zilizokusanywa na TANROAD mwaka 2012 katika kituo cha Doma zilionesha kuwa kulikuwa na magari 1,750 kwa siku yanayopita katika barabara hii ambayo asilimia 60 yalikuwa ni magari ya mizigo na mabasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aina hii ya magari ndiyo inayosababisha ajali za kuwagonga wanyama. Hifadhi kwa kushirikiana na TAWIRI mwaka 2014 walihesabu na kubaini idadi ya magari imeongezeka na kuwa 1,991 kwa siku. Matokeo ya utafiti 2014 yanaonesha ifikapo 2025 gari
zinazopita hifadhi zitakuwa 4,699 kwa siku. Idadi hiyo ya magari ni kubwa sana kuweza kuimudu kwa siku hivyo, ni lazima tuchukue hatua madhubuti kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua mikakati ya Serikali kwa bajeti hii ya 2017/2018 kuhusu ujenzi wa barabara mbadala ya Melela – Kilosa – Mikumi yenye urefu wa kilometa 141.78 ili kupunguza idadi ya magari yanayopita katika hifadhi na kuokoa uwepo wa Hifadhi ya Mikumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Ahsante.