Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu niliochangia kwa kuongea, napenda pia niongeze mchango wangu kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia magari ya zimamoto katika viwanja vya ndege. Viwanja vingi vina changamoto kubwa sana ya magari ya kuzima moto kikiwepo na Kiwanja cha Nduli, Mkoa wa Iringa. Gari lililoletwa Mkoa wa Iringa lilitokea Kiwanja cha Tabora likiwa bovu na halijawahi kufanya kazi toka limeletwa. Hivyo kiwanja hakina gari la kuzimia moto, gari linalotumika ni la Ofisi ya Zimamoto kama kukiwa na ugeni wa viongozi na sasa hivi gari lile limepata ajali. Napenda kufahamishwa utaratibu unaotumika kupeleka haya magari katika viwanja au kama kuna vigezo vinavyotumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nizungumzie TCRA na mtambo wa TTMS. Nashukuru sana kwa uongozi wa TCRA kwa kutupatia semina ya uelewa wa taasisi yao ikiwemo na matumizi ya huu mtambo wa TTMS. Pamoja na huu mtambo kuwa ndiyo mtambuzi wa namna bora ya kupata taarifa za makusanyo ya makampuni ya simu ili Serikali iweze kutoza kodi stahiki kutokana na miamala ya fedha inayofanyika kupitia simu za mikononi, je, ni lini sasa ule mfumo wa Revenue Assurance Management System (RAMS) utafungwa? Tulipotembelea TCRA tuliambiwa kuwa wana mazungumzo na mkandarasi, nini mkakati wa Serikali kuhusiana na hilo? Napenda kujua kuhusu suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, niongelee kuhusu madeni ya TTCL. Pamoja na Serikali kumiliki hisa kwa 100% lakini bado shirika hili linatakiwa liendelee kujiendesha. Je, ni lini Serikali itaweka mkakati wa kuhakikisha madeni yote yanalipwa, sababu imeamua kulipa madeni yake? Wizara zote zilishafanya uhakiki wa madai, je, haya madeni ya TTCL Wizara wameshaanza kulipa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ni Internet Data Center. Niipongeza Serikali kwa ujenzi wa kituo hiki kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi kumbukumbu. Hata hivyo, ukiangalia katika bajeti zetu kuna baadhi ya Wizara na Taasisi za Serikali pia zinatenga bajeti kwa ajili ya kuwa na data center zao. Je, ni kwa nini kituo hiki kisitumike kwa taasisi zote za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ni TAZARA. Nataka kujua ni lini ule upungufu wa ile Sheria Na. 23 ya mwaka 1975 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 4 ya mwaka 1995 itafanyiwa marekebisho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.