Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia katika hii Wizara ya Miundombinu. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri pamoja na Wizara yote katika miradi ambayo inaendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam. Pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika sekta ya miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nianze mchango wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kitabu cha Wizara ya Miundombinu lakini kuna barabara ambazo naona zinaweza zikatusaidia katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam, mwaka 2014 hizi barabara ziliainishwa kwamba zitaanza kujengwa mwaka 2015, lakini kwa sasa hivi nimeangalia nimeona tu kwamba wamesema ndiyo wanataka kufanya tathmini, ina maana hawajaweka hata hiyo bajeti ya tathmini au kujua ni lini zitaanza kujengwa. Barabara ambayo inatoka Kimara inapitia Jimbo la Kibamba na pia inakuja mpaka Banana lakini pia inakwenda mpaka Kitunda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie hizi barabara, kwa sababu hizi barabara za Dar es Salaam, inaweza ikaonekana Dar es Salaam kwamba kuna barabara nyingi zinatengenezwa lakini Dar es Salaam kuna foleni kubwa, hii barabara kama ikitengenezwa inaweza ikatusaidia wakazi wa Dar es Salaam ili foleni iweze kupungua. Kwa sababu, watu ambao wanatoka Mbezi wanatumia hii barabara kupitia Jimbo la Segerea na baadaye wanapitia Ilala kwa ajili ya kukwepa foleni na kuongeza hata watu wafike makazini mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho nilikuwa nakiangalia nilijua Mheshimiwa Waziri atakiweka ni fidia ya wakazi wa Kipunguni Kata ya Kipawa. Mwaka 2016 kwenda 2017 nilisimama nikaongea kuhusu hii fidia ya wakazi wa Kata ya Kipawa, ambao wamehamishwa kwa ajili ya kupisha upanuzi wa Airport, lakini naona hapa Mheshimiwa Waziri hajaweka bajeti wala hajawazungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wakazi tangu mwaka 1995 wako pale wanasubiri kuhamishwa na wanasubiri malipo yao. Mpaka sasa hivi hawajalipwa na hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea na hakuna kitu chochote wanachokijua kwamba Serikali itawalipa lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiingia katika Kata ya Kipawa, Mtaa wa Kipunguni sehemu ya hawa wakazi wanapokaa imeshakuwa kama vile watu wamehama kwa sababu watu hawawezi kufanya maendeleo yoyote wameambiwa wanasubiri malipo yao. Kuanzia mwaka 1995 mpaka leo hakuna kitu chochote walicholipwa na kuna watu wengine ambao walikuwa wanasubiri hizi pesa wameshakufa na wengine ni wastaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu nilishakwenda na Naibu Waziri tukafanya mkutano na hawa wananchi, akasema kwamba wampe miezi mitatu, lakini sasa hivi ni zaidi ya miezi nane, hakuna jibu lolote ambalo Mheshimiwa Naibu Waziri wala Mheshimiwa Waziri amelitoa. Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kuniambia ni lini hawa wakazi wa Kipawa wataweza kulipwa pesa zao. Kwa sababu kwanza sheria inazungumza watu wasiondoke walipwe fidia ndiyo waweze kuondoka, lakini wale watu wameondoka na mpaka sasa hivi hawajui kinachoendelea. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kumalizia kwenye bajeti yake aniambie ni lini atawalipa wakazi wa Kipawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nataka kuzungumzia bomoa bomoa ambayo imepita Majimbo ya Ukonga, Segerea na Ilala. Nina masikitiko makubwa sana kwa Mheshimiwa Waziri, hawa wakazi ambao wamekaa walikuwa wamejenga pembeni ya reli, tunayo Serikali kuanzia Serikali ya Mtaa, Serikali ya Kata lakini wamewachia hawa watu wamejenga na baadaye mmekuja kuwabomolea, hata mlivyowabomolea hamjafuata utaratibu Mheshimiwa Waziri. Mtu amekaa kwenye nyumba yake miaka 50 unamwamsha saa 10 ya usiku akupishe unabomoa, jamani hiyo siyo haki! Kwanza tunawaonea sana wananchi, saa kumi ya usiku kuwatoa watu kwenye nyumba zao, wengine wana wagonjwa, wengine wanaumwa na wengine ni wazee mnaenda kuwabomolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishafanya kikao na wakazi ambao waliambiwa wajiandae watabomolewa kwa sababu ya kupisha reli ya kisasa ambayo inajengwa. Nami nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, hakuna mtu yeyote awe anatoka Jimbo la Segerea au Ilala ambaye anakataa maendeleo, lakini watu wanakataa ile process waliyotumia, jinsi walivyokwenda. Walisema kwamba tunawapa miezi mitatu ili waweze kujiandaa waondoke, lakini kabla ya hata siku kumi tangu wametoa barua wameenda saa kumi ya usiku kuwavunjia nyumba zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo reli wenyewe wameweka jiwe kwamba mwisho wetu mtu asijenge hapa, lakini wamebomoa wameenda wamelipita mpaka lile jiwe walilojiwekea wenyewe. Tunajua Sheria ya Manispaa inasema kwamba wakazi wa Mjini wanatakiwa kukaa mita 15 na wa Kijijini ni mita 30, watu wa reli wameenda wamebomoa mita
30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri atuambie kwamba ni sheria gani imetumika kuwavunjia wakazi wa Mnyamani Buguruni, Ukonga pamoja na Ilala kwako Mheshimiwa Zungu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu hawa wakazi mpaka sasa hivi hawana sehemu ya kukaa, wako nje na hawajui kama mtawalipa au hamtawalipa. Kwa sababu sasa hivi kumezuka tabia, kila mtu ambaye anaenda kufanya kitu ambacho siyo kizuri anasema maagizo yametoka juu, ni uwongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie jamani hawa ni watu wetu, tumesema kwamba tunawasaidia watu wanyonge. Sasa tunawasaidiaje watu wanyonge kwa kuwavunjia nyumba zao. Mheshimiwa Waziri naomba akija kujibu haya mambo anieleze wakazi hawa aliowavunjia kupisha hii reli ya kati ametumia sheria gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kuongelea ni miradi ya DMDP ambayo ilitakiwa barabara zijengwe Kiwalani pamoja na Minazi Mirefu. Leo ni mwaka wa nne, kila mwaka tukikaa hapa tunapanga kwamba tutaanza kujenga mwaka kesho na mpaka sasa hivi nimeangalia kitabu hakuna bajeti ya miradi ya DMDP kuhusu hizo barabara za Kiwalani pia barabara za Minazi Mirefu. Watu hawa wamekuwa wakikaa kwenye barabara ambazo siyo nzuri kwa muda mrefu. Sasa hivi ni miaka karibu 15 wanaahidiwa kwamba huu mradi utaanza, ulikuwa uanze mwaka jana mwezi wa Nane lakini mpaka sasa hivi haujaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapo, Mheshimiwa Waziri naomba majibu.