Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano hususan katika mpango wake wa Makadirio ya Mapato na Matumizi wa mwaka unaofuatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo napenda kuanza nalo, maana nina mambo kama sita hivi ya kuzungumza kwa haraka haraka. Jambo la kwanza ni utekelezaji wa miradi ya barabara. Hii imekuwa ni kilio kwa Wabunge wote ndani ya Bunge, nami kama Mbunge wa Jimbo la Momba nimekuwa nikilalamikia hivi kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali ya kawaida tu ambayo hata Waheshimiwa Mawaziri wanasema, tumekuwa tukilalamikia juu ya ahadi wanazotoa Viongozi wetu Wakuu hususan Marais, zinachukua muda mrefu sana kukamilika. Nimezungumzia barabara ya kutoka Kamsamba, yaani Kibaoni – Kilyamatundu – Kamsamba unakwenda mpaka Mlowo zaidi ya kilometa 200. Aliahidi Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete mwaka 2009, lakini barabara ile mpaka leo imekuwa ni story ambayo haibadiliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia kitabu cha Mheshimiwa Waziri hapa, ukiangalia kwenye ukurasa wa 269, fedha iliyotengwa mle ndani, unakuta tu ni rehabilitation, sijui feasibility study, yaani shilingi milioni 120, shilingi milioni 200; kwenye zaidi ya kilometa 200, ni sawa na kazi bure. Kwa hiyo, tunataka Serikali iwe na mpango maalum kukamilisha hizi ahadi za Waheshimiwa Marais wanazozitoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuendana na barabara hiyo msisahau lile Daraja la Momba. Mmelitengea shilingi bilioni tatu, wananchi sasa tumeshachoka kusikia zile story za kila mwaka; fedha inatengwa, feasibility study, tuko site; tunataka daraja, hatutaki story hizo ambazo zimekuwa zikijirudia kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu kwa haraka haraka ni usimamizi wa huduma za usafiri na uchukuzi hususan majini na kwenye maziwa. Sana sana mnachokuwa mnazungumzia kila mara, Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa; lakini kuna maziwa madogo madogo yaliyoko kule kwetu, kwa mfano Ziwa Rukwa liko mpaka kule Momba; kuna Ziwa Manyara, watu wanakufa kule kila siku, maboti yanaua watu, lakini taarifa zake huku huwezi kuzikuta na hakuna hatua yoyote ambayo inakuwa ikichukuliwa na Wizara yako. Kwa hiyo, tungependa mnapotoa ufafanuzi muyajadili pamoja na maziwa haya madogo likiwemo Ziwa Rukwa na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya kuyajadili hayo machache ya Jimbo langu, nizungumze sasa masuala ya Kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia Shirika la Ndege (ATCL) ni kama vile hatujawahi kuwa na shirika nchi hii. Yaani ni kama vile ndiyo limeanza mwaka 2016, lakini ukweli ni kwamba Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati anaondoka madarakani aliacha ndege 11. Hii kila mtu anajua kwamba ziliachwa ndege 11 ambazo zilipotea katika mazingira ambayo hayaeleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nia njema inaonekana kwamba tunahitaji kufufua shirika letu la ndege na kuna sababu za msingi zimeelezwa, hakuna mtu anayebishana nayo; lakini kuna mambo tunahitaji kuwashauri kama wachumi. Kununua ndege cash kwa kulipa asilimia 100 siyo sifa nzuri sana kiuchumi tofauti na utaratibu ambao duniani watu wote wanatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nimeona kwenye bajeti mmetenga shilingi bilioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa ndege, ni jambo jema hakuna mtu anayekataa. Nunueni ndege kama utaratibu wa watu wengine wanavyofanya. Lipa ten percent, ndege inakuja nchini inafanya kazi. Kwenye hiyo fedha mnaweza kununua zaidi ya ndege kumi tofauti na sasa hivi mnavyotaka kwenda kulipa cash. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa sisi hatukatai, lakini tunachojaribu kuwashauri, jaribuni kufanya mambo kwa utaratibu wa kawaida wa kichumi ambapo fedha moja inaweza ikasaidia mambo mengine wakati jambo lingine na lenyewe linafanyika. Kwa hiyo, hicho ni kitu ambacho nasema ni muhimu tukawa tunakizungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tuelezeni kuhusu deni ambalo lilikuwa linaikumba ATCL, kwamba mnasema ndege zitakuja, hofu yetu ni kwamba kwa mfano hiyo ndege ambayo itakuwa inakwenda mpaka huko Uchina sijui wapi; tunafahamu kuna kesi Mahakamani kuhusu Shirika la ATCL, madeni yanayodaiwa; ikitokea sasa ndege ikaenda kule, ikakamatwa ikazuiwa kule, maana yake hasara kwa Taifa itaendelea kubaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunataka tujue kwa nini Serikali imechukua hatua ya namna hii kwa sababu mpaka sasa hivi hizi ndege zimekuwa zikinunuliwa kwa utaratibu mmoja tu; wa Mheshimiwa Rais kununua na kuzileta ndani ya nchi, lakini ule utaratibu wa kishirika wa kiuendeshaji ambao unaweza kuwaathiri huko nje kutokana na deni ambalo shirika lilikuwa nalo tangu awali utatupeleka wapi? Kwa hiyo, tungependa tupate ufafanuzi juu ya hili jambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza jambo la tatu kwa haraka haraka kuhusu Shirika la TAZARA. Kila mwaka tumekuwa tukilalamika kuhusu TAZARA, kwamba TAZARA haifanyi kazi vizuri, sasa hivi ukiangalia kwenye rekodi zao wanasema mwaka huu angalau umebeba mizigo tani laki moja. Wakati Shirika la TAZARA linaanza lilikuwa linabeba mizigo tani milioni moja kwa mwaka, sijui kama umenielewa, lakini leo tunajisifu kwa tani laki moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa jibu ni moja tu, kwamba nchi mbili wanachama, zinategeana juu ya hili shirika, ndiyo maana hili shirika haliwezi kuendelea. Kila siku mgogoro kwenye hili shirika umekuwa ukisemekana ni management, lakini ukweli ni kwamba hapa kuna kutegeana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama mnashindwa, kuna plan B vilevile. Mnaweza mkazungumza na Zambia pamoja na Tanzania mkakubaliana kwamba sisi tunafikiri hii reli kutokea Tunduma mpaka Dar es Salaam, sisi watu wa Tanzania tuwe tunaihudumia wakati huu kuna matatizo. Watu wa kutokea Tunduma mpaka kwenda New Kapiri Mposhi kule wahudumie watu wa Zambia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu mizigo siyo tu ile inayotoka Kongo, kuna mizigo ambayo inatoka Mbeya pale kuja Dar es Salaam; kuna mizigo inayopitia Iringa na maeneo mengine; tunaweza tukaitumia hii kama sehemu mojawapo ya reli ya kati, yaani mkavunja mkataba, kila mmoja wa kipande chake akatumia huku na wao watu wa Zambia wakatumie kule. You can go on that way, inaweza kusaidia kuliko sasa hivi mnatumia fedha nyingi na shirika halionekani likienda mahali popote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka nizungumzie hapa, nimeona kwenye hotuba, Serikali inataka kufufua Shirika la TTCL. Shirika hili lilikuwepo tangu mwaka 1993, lakini kwenye records hapa wanasema tunataka tutoke wateja laki mbili mpaka kufika milioni moja; mpaka mwaka 2020 wanahitaji kufikisha wateja milioni nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Master plan ya investment yao, fedha wanazohitaji ni Dola 663,000 kwa miaka hiyo mitano ili wafikie wateja milioni nne lakini ukiangalia Kampuni dogo kabisa la Hallotel ambalo limeanza Oktoba, 2015 wenyewe within mwaka mmoja na kidogo wame-invest dola bilioni moja, wana wateja 2.7 million.
Mheshimiwa Naibu Spika, mindset ya Watanzania bado imekaa ile ile kwamba sisi ni Serikali, tutaliendesha Shirika Kiserikali; sasa imegeuka mashirika yote Serikali ihudumie; haiwezekani! Kwa hiyo, lazima tu-change mtazamo huu ambao umeenda; na ndiyo maana unakuta hata Shirika la ATC sasa hivi linakwenda katika huo mtazamo wa Kiserikali Serikali, siyo mtazamo wa Kikampuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi biashara ni ushindani! Sasa huwezi kwenda kwenye ushindani wa kimawasiliano unaona kuna Vodacom pale, kuna Tigo, kuna Airtel halafu na wewe unakuja TTCL kwanza una-invest kidogo, pili hamna marketing strategies ambazo unaweza uka-penetrate kwenye market, lakini mtu atakuja atasema hawa Hallotel wanatumia mkongo wetu. Yes, wanatumia minara ya TTCL, lakini at the end of the day gharama yao wao Hallotel iko chini kuliko gharama ya wao wanaomiliki huo mtambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapo unakuwa unajiuliza, hapa utakuwa unafanya nini katika hili Taifa? Yaani we don’t think big! Bado mitazamo yetu kufikiri juu ya biashara ni mitazamo ya kijima. Tunafikiri bado kule nyuma kwamba Serikali inaweza kufanya kila kitu, lakini sasa hivi dunia inaendeshwa na market forces; soko huru ndiyo linaloamua juu ya uendeshaji wa uchumi wa nchi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda haya mashirika na hizi taasisi ndogo ambazo tunataka Taifa lifanye biashara, zisibaki na huu mtazamo; hii mindset ya sasa kwamba kila kitu Serikali ita-inject fedha pale, kwamba Serikali ndiyo itaendesha hiyo kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Shirika la ATC, Serikali ikitoa mkono maana yake na Shirika lenyewe linakufa kwa sababu mtazamo wetu si ule ambao kwamba tunaweza kujiendesha wenyewe tukafika kule tunapotakiwa, kwa sababu sasa hivi kila kitu tunataka investment ya Serikali. Kwa, kwa hiyo, ni lazima tubadilishe mtazamo wetu dhidi ya haya mashirika ambayo Serikali inahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, nashukuru na naomba kuwasilisha.