Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu waliotangulia, kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa mara ya kwanza kabisa kuonekana kwenye Bunge lako Tukufu na mimi nikichangia Mpango wa Maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na azma ya Serikali ya hapa kazi tu, haijaishia kwenye maneno. Mwanzoni mwa mwezi huu Mheshimiwa Rais alizindua mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi Namba II megawatt 240, lakini mwishoni mwa wiki hii pia amezindua pia ujenzi wa flyover katika barabara ya kuelekea uwanja wa ndege na kama haitoshi juzi amezindua pia ukamilishaji wa Daraja la Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Watanzania wote, Waheshimiwa Wabunge na sisi wananchi, tufanye kazi moja ya kutwanga maendeleo, hakuna kazi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze sasa kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika mchango huu wa Mpango wa Maendeleo wa Pili. Katika Mpango huu nijielekeze moja kwa moja katika ukurasa wa 10, kadhalika ukurasa wa 28. Ukurasa wa 10 Waheshimiwa Wabunge, suala la nishati limezungumzwa kwa kirefu sana japo kwa maneno machache, nami niongezee sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnavyotambua Waheshimiwa Wabunge, Serikali ya Awamu ya Tano, kwa wananchi na Waheshimiwa Wabunge tunasema suala la nishati sasa ni la kufa na kupona. Tutake tusitake tutazalisha umeme wa kutosha kujenga viwanda vyetu. Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge, kwa ridhaa yako Naibu Spika kwa jinsi ambavyo wanaunga mkono kuelekeza nguvu za wananchi kwenye kuzalisha umeme wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 10 wa Mpango huu umezungumza kwamba mwaka 2016 tungefikisha megawatt 2,780, bado tunatembea 2016 inaendelea, lakini hata hivyo nguvu kubwa sasa inayoonekana niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge na wananchi, sasa hivi megawatt tunazozipata kwenye nishati asilimia kubwa ni kutokana na gesi asilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze Waheshimiwa Wabunge, kwa sasa hivi Kinyerezi peke yake tuna uwezo wa kupata zaidi ya megawatt 700. Hapo nyuma tulikuwa tunapata megawatt chini ya 300. Lakini kwa sababu tunataka gharama za umeme zishuke na haziwezi kushuka kama hatuzalishi umeme wa gesi na umeme wa maji, niseme tu kwenye upande wa umeme wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kina cha maji cha Mtera kinatosha, kinaongezeka, leo tuna milimita 697 kati ya 698 ambalo ni ongezeko kubwa linatupatia uhakika kwamba tutakuwa na umeme wa kutosha tunakoelekea. Kihansi kati milimita 1,190 tuna milimita 1,782, tunapungukiwa kidogo. Kidatu tuna milimita 471 kati ya milimita 478, kwa hiyo tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa ambayo nataka niwaeleze wananchi ni kupungua kwa gharama za umeme. Mwezi huu gharama za umeme zilizokuwa zinakwaza wananchi tumeondoa gharama za maombi ambayo ilikuwa ni shilingi 6,000.00. tumeziondoa, kadhalika tumeondoa gharama za kufanyiwa service (service charge) ambazo pia zilikuwa zinakwaza sana wawekezaji. Lakini wananchi wa vijijini sasa hivi gharama ambayo wanaweza kuwa nayo kimsingi kwa umeme wetu wa REA ni bure isipokuwa VAT ya shilingi 27,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni juhudi kubwa sana ya Serikali. Na niwahakikishie wananchi kwamba kwa sasa, niongezee japo kidogo jambo ambalo liliulizwa jana kwa Wizara ya Mambo ya Ndani, kwamba wazee wetu sasa hivi inaonekana kuwa wana macho mekundu kwa sababu ya kupuliza kwenye moto. Sasa hivi moto unaokuja sasa siyo wa kupuliza, ni wa umeme wa kukandamiza. (Makofi)
Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi kwamba kutakuwa na umeme vijijini, wataweza kujenga viwanda vidogovidogo kama ambavyo wanafanya nchi nyingine za Thailand na China. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba juhudi za maksudi zinaelekezwa kwenye umeme, pia juhudi za maksudi kuendeleza viwanda vidogo vidogo kwa kutumia umeme itaongezeka kwa kiwango kikubwa. Kama mnavyofahamu sasa hivi tunatarajia, kwenye bajeti yetu tutaeleza kwa upana zaidi, tunatarajia kwenye Awamu hii ya Tatu inayokuja tuunganishe umeme zaidi ya vijiji 6,000, ukiunganisha nguvu hiyo kwa wananchi wa vijijini kwa namna yoyote ile mwenye kuweza kusuka nywele kwa kutumia umeme atatumia umeme.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kalemani naomba umalize, muda wako umekwisha.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.